Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Cecil David Mwambe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ndanda

Primary Question

MHE. CECIL D. MWAMBE (K.n.y MHE. UPENDO F. PENEZA) aliuliza:- Je, Serikali imeweka mikakati gani kuimarisha huduma za umeme, maji, afya na elimu katika maeneo ya vijijini ili kuongeza uzalishaji katika maeneo hayo na kuzuia wimbi la watu kukimbilia mijini?

Supplementary Question 1

MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nitakuwa nina maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri kwamba Serikali imejipanga kuhakikisha wanafikisha umeme pamoja na maji hasa zaidi kwenye shule pamoja na sehemu zingine za kutolea huduma za kijamii, lakini ningependa kwa uhakika kabisa aseme kwamba ni lini Serikali itatimiza suala hili kwa sababu ni muda mrefu wamekuwa wakiliongea kila mara bila kuwa na tarehe ya uhakika kwamba itakapofika wakati fulani tutakuwa kwa kweli tumetekeleza, bado shule nyingi pamoja na vituo vya afya vinakosa huduma ya umeme pamoja na maji?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kuna vijiji vingi sana, kama anavyosema kwamba Serikali imeazimia kupeleka umeme kwenye vijiji vyote zaidi ya 7,000, lakini ukipita Jimbo la Ndanda kwa mfano Vijiji vya Nangoo, Liputu, Ndolo pamoja na Mdenga vinapitiwa na umeme wa msongo wa megawati 33. Sasa Waziri angetusaidia kutueleza ni lini kwa hakika Serikali sasa wako tayari kushusha umeme ule kwa ajili ya matumizi ya watu wale walioko chini ya hizi waya ambazo kwao ni hatari kwa maisha?Ahsante.

Name

Joseph George Kakunda

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Sikonge

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA): Mheshimiwa
Mwenyekiti, katika maswali yake mawili ya nyongeza aliyouliza Mheshimiwa Cecil Mwambe, Mbunge wa Ndanda yeye mwenyewe ni shahidi anafahamu kwa sababu ameshiriki kupitisha bajeti hapa anajua mipango ya Serikali ilivyo. Sina shaka kwamba anatambua kwamba ahadi iliyoko kwenye Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano inaendelea kutekelezwa vizuri na tuna uhakika vijiji vyote nilivyovitaja kwenye jibu la msingi vitapata umeme pamoja na vitongoji vyake kama ambavyo Wizara ya Nishati imeahidi, na mikakati iko wazi na yeye mwenyewe Mheshimiwa Mbunge ni shahidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la maji, Mheshimiwa Waziri wa Maji ametoa ahadi hapa Bungeni kuhusu kutekeleza awamu ya pili ya Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji, na hii itaongezeka kasi zaidi pale ambapo tutaanza kutekeleza miradi ya maji vijijini kupitia ile Wakala wa Maji Vijijini ambao utafanya kazi sawasawa na REA inavyofanya kazi. Kwa hiyo, ndugu yangu Mwambe ondoa shaka katika swali lako la kwanza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, huu umeme ambao umepita kwenye vijiji alivyovitaja na msongo anaujua ameutaja, mimi kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nishati namuahidi kwamba mikakati ya Serikali itatekelezwa na wanavijiji aliowataja hao watapata umeme.

Name

George Malima Lubeleje

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mpwapwa

Primary Question

MHE. CECIL D. MWAMBE (K.n.y MHE. UPENDO F. PENEZA) aliuliza:- Je, Serikali imeweka mikakati gani kuimarisha huduma za umeme, maji, afya na elimu katika maeneo ya vijijini ili kuongeza uzalishaji katika maeneo hayo na kuzuia wimbi la watu kukimbilia mijini?

Supplementary Question 2

MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ili na mimi niulize swali moja la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa katika mipango yote ya kujenga shule za sekondari, shule za msingi, zahanati, vituo vya afya tunasahau sana huduma za maji, umeme pamoja na afya. Sasa nataka niulize swali kwa Mheshimiwa Waziri na bahati nzuri sana Mheshimiwa Jafo, Waziri wa TAMISEMI Mpwapwa anaifahamu vizuri sana. Katika bajeti ya mwaka 2018/2019; je, Serikali itakuwa tayari kutenga fedha kwa ajili ya kuhakikisha kwamba vituo vya afya, zahanati, shule za msingi, sekondari zote Jimbo la Mpwapwa zinapata huduma ya maji, umeme na afya?

Name

Dr. Selemani Said Jafo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kisarawe

Answer

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba nimpongeze Naibu Waziri wangu kwa majibu mazuri sana aliyoyatoa hapo awali. Pia naomba kujibu swali la Mheshimiwa Lubeleje kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli ukiangalia hali halisi ya Jimbo la Mpwapwa changamoto hizo alizozungumza Mheshimiwa Mbunge ni kweli, lakini hata hivyo tunachokifanya ni kuhakikisha kwamba tunawapatia huduma ya maji. Nafahamu kwamba Jimbo la Mpwapwa, Wilaya ya Mpwapwa ina changamoto kubwa. Tumeweza kuhakikisha kwamba; kwa mfano ile miradi sita na Mzee Lubeleje anafahamu tulivyokuwa kule Mima pamoja katika ujenzi wa Kituo cha Afya, mtandao wa maji ambao kwa muda mrefu wakandarasi walikuwa mradi huo walikuwa hawajaanza sasa wakandarasi wote sita wako site.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jukumu letu kubwa ni kwamba maji yale yatakapotoka katika jamii kuna water points tutazipeleka katika taasisi hizi za Umma kwa ajili ya kuhakikisha kwamba vituo hivyo vinapata maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu mpango wa REA mnafahamu kwamba Wizara ya Nishati imezungumza wazi katika mpango wa REA Awamu ya Tatu kwamba itahakikisha katika sehemu zote za umma hasa vituo vya afya, shule pamoja na taasisi za dini zote zitapatiwa umeme kupitia katika mpango wa REA III. Isipokuwa katika hili niwaombe Waheshimiwa Wabunge katika ajenda hiyo lazima tuanze maandalizi ya awali ya kuweka wiring katika maeneo hayo, kwa sababu umeme ukishafika hapo ni lazima taasisi yenyewe iwe imeshafanya wiring ili kuhakikisha kwamba huduma hiyo inapatikana vizuri. Ahsante sana.