Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Shabani Omari Shekilindi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Lushoto

Primary Question

MHE. SHABANI O. SHEKILINDI aliuliza:- Jimbo la Lushoto linakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa maji hususan katika maeneo ya Ubiri, Makanya, Kwemashai, Gare, Mlola, Mbwei, Malibwi na Kilole:- Je, ni lini Serikali itawapatia wananchi hao majisafi na salama ili waondokane na adha hiyo?

Supplementary Question 1

MHE. SHABANI O. SHEKILINDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi iliniweze kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Kwanza kabisa nimshukuru Naibu Waziri kwa majibu mazuri na pia nishukuru kwa kutupatia bilioni 1.66.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mamlaka ya Maji katika Mji Mdogo wa Lushoto ilipatiwa fedha kwa ajili ya kujenga tenki la lita za ujazo 650,000 na banio katika eneo la Kindoi, lakini mpaka sasa mradi ule bado haujaanza. Nilifuatilia kwa Mkurugenzi wa Tanga UWASA alisema taratibu tushazikamilisha hivyo tunasubiri kibali kutoka Wizarani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa wananchi wamesubiri mradi ule haujaanza kwa muda mrefu sasa, naamini wananchi wananisikia na kuniona. Je, ni lini Mheshimiwa Waziri kibali hicho kitapatikana ili Mkandarasi aanze kazi mara moja, kwani mradi ule ukikamilika utaendelea kuhudumia Kata za jirani ambayo ni Ngulu na Ubiri?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa Wilaya ya Lushoto ina vyanzo vingi vya maji pamoja na mito inayotitririka maji kutoka milimani. Je, Serikali ipo tayari kwa sasa kuhakikisha inatumia vyanzo hivyo pamoja na maji yanayotiririka kutoka milimani kujenga mabwawa na kutumia vyanzo hivyo ili kuwapatia wananchi wa Lushoto maji safi na salama na hasa kutimiza dhana nzima ya kumtua mama ndoo kichwani; hasa kina mama wa Kwekanga, Kwemakame, Mkuzi, Mazashai, Mazumbai, Ngwelo, Miegeo, Handei, Masange, Kwemashai, Gare pamoja na Magamba Coast? (Makofi/Kicheko)

Name

Jumaa Hamidu Aweso

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Pangani

Answer

NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nampongeza Mheshimiwa Shekilindi kwa jinsi anavyofuatilia huduma ya maji katika Jimbo lake; na kwamba nishakwenda Lushoto, mazingira ya Lushoto ni mazuri, ni milima milima upo uwezekano mkubwa kabisa kuwapatia wananchi wa Lushoto maji safi na salama kwa zaidi ya asilimia mia moja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza la Mbunge linahusu kibali, nitahakikisha kabla ya Bunge hili kukamilika kibali kitatolewa; kwa hiyo naomba sana tuwasiliane ili kibali kitolewe na utekelezaji wa mradi uendelee.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali la pili, ni kweli kuna vyanzo vingi vya maji Lushoto na tutahakikisha kwamba tunaweka mabanio ya kutosha kule milimani na kuweka mabomba kwa sababu maji ni ya mserereko hayana gharama kubwa na pale itakapobidi tutajenga hadi mabwawa ili maji yawe ya kutosheleza.