Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Andrew John Chenge

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bariadi

Primary Question

MHE. ANDREW J. CHENGE aliuliza:- Sera ya Serikali ni kuunganisha Makao Makuu ya Mikoa kwa barabara za kiwango cha lami. Mkoa wa Simiyu haujaunganishwa na mikoa jirani ya Singida na Arusha. Je, Serikali ina mpango gani wa kuifanyia upembuzi yakinifu na usanifu wa kina barabara ya Bariadi – Kisesa – Mwanhuzi hadi Daraja la Mto Sibiti na hatimaye ijengwe kwa kiwango cha lami?

Supplementary Question 1

MHE. ANDREW J. CHENGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipatia nafasi hii na nimshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri. Natambua juhudi za Serikali zinazofanyika kwa kuunganisha Mkoa wa Simiyu na Mikoa jirani ya Singida na Arusha. Nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza ningependa kufahamu kama huo mpango mkakati wa miaka mitano alioutaja Mheshimiwa Waziri, unashabihiana vipi na Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2015 na 2020?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, je, Mheshimiwa Waziri atakuwa tayari kwenye bajeti ya mwaka 2018/2019 kuingiza sehemu ya barabara hiyo ya Moboko – Mwandoya – Kisesa - Bariadi kwa upande wa Mkoa wa Simiyu; na mto Sibiti – Mkalama – Nguguti - Iguguno na Singida ili sehemu hizi mbili za barabara hii muhimu ziweze kufanyiwa kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina? Ahsante. (Makofi)

Name

Elias John Kwandikwa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ushetu

Answer

NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kumpongeza sana Mheshimiwa Chenge kwa namna ambavyo anapigania hii barabara iweze kujengwa, lakini kwa maendeleo kwa ujumla katika Mkoa huu wa Simiyu.
Vilevile niseme kwamba barabara hii ambayo anaizungumza Mheshimiwa Chenge ni muhimu sana kwa mikoa mingi ikiwemo Kagera, Mwanza, Shinyanga, Mara kwa sababu barabara hii itakapojengwa itawezesha watu wote katika mikoa hii ninayoitaja kupita na kupunguza umbali katika eneo hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu kwamba kama alivyosema katika swali lake la kwanza, kwamba katika mpango wa miaka mitano, tunashughulikia hii kwa sababu imetajwa pia katika ilani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu kwamba Mheshimiwa Andrew Chenge mwenyewe anafahamu kwamba tumeshaanza ujenzi katika Mto Sibiti na kazi hii itakamilika mwishoni mwa mwaka huu na ule utaratibu wa uratibu wa usanifu wa barabara hii, fedha nyingi sana zimetengwa. Zimetengwa Euro milioni 2.8 ili kuweza kukamilisha kazi hii. Niseme tu kwamba ili kazi ikamilike kuendana na kipindi hiki cha miaka mitano na utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi, ziko consultancy nne ambazo zimeungana pamoja ili kuhakikisha kazi inakamilika kwa haraka. Kwa hiyo, utekelezaji wa Ilani utakwenda sambamba na kazi kubwa sana ambayo inaendelea kufanyika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili kuhusu kuingiza hii sehemu kwenye usanifu katika kipindi hiki cha mwaka wa fedha, ushauri wako huu muhimu nauchukua ili wakati wa process ya bajeti hii inaendelea, tulifanyie kazi itakapowezekana, tutaweka fedha ili kuanza usanifu wa vipande hivi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kipande hiki cha barabara kutoka Mkalama kwenda Singida, iko barabara nyingine ambayo inatoka upande wa Sibiti, inapita Msingi kwenda Ulemo hii pia itawezesha watu wa maeneo yale waweze kupita kiurahisi wakitokea Mkoa wa Simiyu.
Mhesimiwa Mwenyekiti, niseme tu kwa wananchi wa Meatu, Simiyu watakuwa na access nzuri kwenda kutibiwa Haydom. Kwa hiyo, sisi kama Serikali tunatambua umuhimu wa barabara hii na ndiyo maana tumeiweka katika ilani na tutaitekeleza ili wananchi waweze kupata manufaa makubwa zaidi. Ahsante.