Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Rashid Abdallah Shangazi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mlalo

Primary Question

MHE. RASHID A. SHANGAZI aliuliza:- Je, ni lini Wilaya ya Lushoto itaanza tena kupokea matangazo ya Redio ya Taifa (TBC)?

Supplementary Question 1

MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Pamoja na majibu ya Serikali ambayo yanatia matumaini, nina maswali madogo ya nyongeza.
Swali la kwanza, wakati redio ya TBC wanatumia mawimbi ya short wave na medium wave mawasiliano yalikuwa mazuri. Je, hawaoni kwamba kuhamia kwenda digital inaweza ikawa ni changamoto hata kwa maeneo mengine yaliyoko pembezoni katika Taifa letu? (Makofi)
Swali la pili, kwa kuwa kwa mujibu wa Katiba Ibara ya 18(b) tunayo haki ya kupokea na kupata taarifa, sasa anawaambia nini wakazi wa Mlalo ambao wako pembezoni mwa nchi jirani ya Kenya ambao hawapati habari za Taifa lao na je, hawaoni kwamba hii inahatarisha usalama wa Taifa? (Makofi)

Name

Juliana Daniel Shonza

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naomba nichukue nafasi hii ya kuweza kumpongeza kwa dhati kabisa Mheshimiwa Rashid Shangazi kwa namna ambavyo amekuwa akifuatilia kwa umakini kabisa matatizo ya wananchi wa Jimbo la Mlalo.
Mheshimiwa Naibu Spika, niseme kwamba baada ya kupokea majibu mazuri kabisa ya Serikali nilitegemea kwamba Mheshimiwa Shangazi atakuwa hana maswali ya nyongeza. Kwa sababu ameuliza maswali mawili, naomba nimjibu kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, siyo kweli kwamba kuhama kutoka kwenye mfumo wa analogy kwenda kwenye digital imepelekea kuweza kupunguza usikivu wa redio hii ya TBC. Changamoto kubwa ambayo ilikuwepo ni kwamba mitambo mingi ambayo ilikuwa inatumika ilikuwa ni mitambo ambayo imechoka, mibovu ukizingatia kwamba mitambo hiyo ilikuwa ni ya muda mrefu sana.
Kwa hiyo, hata linapokuja suala zima la kutafuta vipuri kwa ajili ya kufanya marekebosho ya mitambo hiyo, ilikuwa ni ngumu sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nimtoe hofu Mheshimiwa Rashid Shangazi kwamba tatizo hilo kwa sasa hivi TBC imelichukua kwa kina na inalifanyia kazi na mpaka sasa hivi katika mikoa ya Arusha, Dodoma, Mwanza pamoja na Kigoma tumeanza utaratibu wa kuboresha mitambo hiyo ili kuhakikisha kwamba matangazo haya ya TBC Taifa pamoja na TBC FM yanawafikia wananchi kama ambavyo inatakiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye swali lake la pili, ametaka kujua umuhimu wa chombo hiki cha Taifa, TBC kwa maeneo ambayo ni ya mipakani. Mheshimiwa Shangazi, Serikali hii ya Awamu ya Tano inatambua kabisa kwamba wananchi wote ambao wanakaa maeneo ya mipakani wana haki ya kupata taarifa kama ambavyo wananchi wengine wanakaa katika maeneo mengine.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuzingatia hilo, kuna mkakati wa TBC ambao umeshaanza kufanyika katika maeneo ya mpakani, nikianza na eneo la Rombo, lakini ukienda na eneo la Namanga, Tarime pamoja na Kakonko, tayari ufungaji wa mitambo mipya ya TBC umeanza kufanyiwa kazi. Tunaamini kwamba mitambo hii itakapokamilika, kwa kiasi kikubwa sana itasaidia kumaliza tatizo hili za usikivu kwa chombo hiki cha TBC.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile Mheshimiwa Shangazi aliuliza kwa upande wa Lushoto. Kama ambavyo nimejibu kwenye jibu langu la msingi, ni kwamba tayari shilingi milioni 50 imeshatengwa kwa ajili ya kumaliza tatizo la usikivu katika Wilaya hiyo ya Lushoto.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimhakikishie kabisa Mheshimiwa Shangazi kwamba eneo hili la Kwamashai ambalo limechaguliwa kuhakikisha kwamba mtambo huu unawekwa, ni eneo ambalo limefanyiwa utafiti wa kina na imeonekana kabisa kwamba mtambo huo ukijengwa hapo, basi maeneo yale ya Lukozi, Mnazi pamoja na Lunguzi ambako imepakana kwa ukaribu kabisa na kijiji ambacho kiko kwenye nchi ya Kenya watapata matangazo ya TBC kama inavyotakiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. (Makofi)