Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Issaay Zacharia Paulo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mbulu Mjini

Primary Question

MHE. ZACHARIA P. ISSAAY aliuliza:- Wilaya ya Mbulu haina barabara ya lami kutokana na kuzungukwa na Bonde la Ufa kuanzia Karatu, Mto wa Mbu, Babati – Hanang hivyo, kufanya magari makubwa kutoka Uganda, Kenya na Dar es Salaam kuzunguka umbali mkubwa ili kufika Mbulu Mjini. Je, Serikali ina mpngo gani wa kutekeleza ahadi yake ya kuweka lami katika barabara ya Karatu – Mbulu – Hydom - Mkalama – Lalago Shinyanga ili kurahisisha usafiri katika njia hiyo?

Supplementary Question 1

MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri na hatua kubwa inayochukuliwa na Serikali yetu.
Je, kutokana na gharama kubwa inayotumika ya matengenezo ya kawaida katika barabara hii inayounganisha mikoa minne kwa kiwango cha changarawe na kwa kuwa katika majibu ya msingi Mheshimiwa Waziri hakueleza mkataba huu unaisha lini, Serikali haioni umuhimu sasa wa kuharakisha kazi hii ya usanifu ili barabara hii ipate kutengenezwa?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili. Mheshimiwa Rais aliahidi ahadi nyingi wakati wa kampeni kama sehemu ya utatuzi wa changamoto za wananchi. Katika Halmashauri ya Mji wa Mbulu aliahidi kilometa tano kwa barabara ambazo zinamilikiwa na Serikali za Mitaa wakati ule. Kwa kuwa sasa barabara zile zimehamia kwa TARURA, je, ni nani atakayetekeleza ile ahadi ya kilometa tano katika barabara zile kwa kuwa Mamlaka za Serikali za Mitaa sasa haziko tena kwenye utaratibu wa kuzihudumia?

Name

Elias John Kwandikwa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ushetu

Answer

NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Mbunge kwa kufuatilia sana hii barabara muhimu ambayo inaunga mikoa mingi.
Mheshimiwa Naibu Spika, niseme kwamba kwanza barabara hii pia inafuatiliwa na Waheshimiwa wa mikoa hii. Mheshimiwa Flatei Massay naye anaifuatilia sana barabara hii tumezungumza, lakini wako Wabunge wa Mkoa wa Singida, wako Wabunge wa Simiyu wanafuatilia hii barabara muhimu sana. Na sisi upande wa Serikali, ili kuharakisha ujenzi wa barabara hii, tumeanza ujenzi katika Mto Sibiti, sehemu ambayo ilikuwa ni mbaya sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, lengo la Serikali ni kuhakikisha kwamba kwa sasa kwanza wananchi wanapita. Wakipita katika barabara hii kwa mtu ambaye anaenda Karatu tuna-save zaidi ya kilometa 400, kwa mtu anayekuja Singida tuna-save zaidi ya kilometa 200; tuna-save muda, lakini pia tuna-save gharama mbalimbali.
Mheshimiwa NAibu Spika, ili kuharakisha ujenzi wa barabara hii, Serikali imechukua hatua kuhakikisha kwamba ujenzi wa daraja utakapokamilika mwishoni mwa mwaka huu, tutakuja kwenda haraka katika ujenzi wa barabara hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu ahadi za kilometa tano, ninajua kwamba nchi nzima ziko ahadi ambazo sisi kama Serikali tunaendelea kuzitekeleza, ikiwepo ahadi ambayo imetolewa huko Mbulu.
Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge avute subira, tumejipanga tunaendelea kuratibu kuona kwa kiasi sasa tunapoenda nusu ya kipindi cha miaka mitano tumetekeleza ahadi ngapi ili tuweze kukamilisha ahadi hizi ambazo Mheshimiwa Rais aliahidi. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge avute subira. (Makofi)