Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Mwita Mwikwabe Waitara

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tarime Vijijini

Primary Question

MHE. MWITA M. WAITARA aliuliza:- Katika Mtaa wa Mongolandege, Kata ya Ukonga, kuna daraja la Mongolandege ambalo huunganisha Jimbo la Ukonga na Jimbo la Segerea. Aidha, daraja la Mto Nyebulu huunganisha Kata ya Buyuni na Kata ya Chanika Magengeni. Je, ni lini Serikali itajenga madaraja hayo muhimu ili kurahisisha huduma za kijamii katika maeneo yaliyotajwa?

Supplementary Question 1

MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Kwanza nifanye marekebisho kidogo kwenye majibu, hili Daraja la Mongolandege lipo kwenye Mto Msimbazi sio Mto Mzinga, lakini vilevile kwa majibu haya, naomba niulize maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, kwa sababu Serikali inakiri kwamba mvua ilinyesha ikaleta madhara makubwa na Daraja la Mongolandege na Mto Nyebulu unatenga maeneo mawili tofauti kwenye huduma za jamii yaani upande mmoja ndiyo kuna shule ya sekondari, msingi, afya na huduma zote za kijamii na upande mwingine wananchi wanakaa pale. Katika hali hiyo mvua ikinyesha huwa ni kisiwa, wanafunzi hawaendi shule mpaka mvua iishe.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujua ni kwa nini Serikali isijitahidi mwaka huu wa fedha ifanye usanifu na fedha itengwe kwa ajili ya kazi hii? Maana kwenye majibu yake anasema wataangalia na baadaye bajeti itengwe.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa sababu eneo hili ni muhimu na wananchi wanapata shida, tunaweza kupata huduma ya dharura ya daraja la muda katika maeneo yote mawili ili huduma ziendelee hasa wakati wa mvua tunapoelekea mwezi Aprili? Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.

Name

Josephat Sinkamba Kandege

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kalambo

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Naibu Spika, uwezekano wa kuweza kutenga fedha kipindi hiki ambacho bajeti tayari imeshapitishwa na Bunge lako Tukufu jambo hili litakuwa na ukakasi mkubwa sana. Tutakubaliana na Mheshimiwa Waitara kwamba ili daraja hili liweze kujengwa kwa kina lazima usanifu ufanyike ili isije ikatokea kama yale yaliyotokea mwanzo.
Mheshimiwa Naibu Spika, namuomba Mheshimiwa Mbunge avute subira na leo nilikuwa nafanya mawasiliano na TARURA, kwa kuanzia kwa ajili ya usanifu itatengwa jumla ya shilingi milioni 100 na ujenzi kwa ajili ya kuanza, tutatenga jumla ya shilingi milioni 300. Kwa hiyo, asipate shida, naomba nimhakikishie kwamba jambo hili liko kwenye mikono salama.
Mheshimiwa Naibu Spika, juu ya suala la daraja la dharura. Ni wazo jema, ni vizuri tukajua wapi tunaweza tukalipata daraja la muda, lakini baada ya kwenda site kutazama uhalisia wa jambo lenyewe likoje. Kwa sababu huwezi ukasema daraja la muda linafananaje bila kwenda site kujua uhalisia ukoje. Nashukuru.