Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Amina Saleh Athuman Mollel

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. AMINA S. MOLLEL aliuliza:- Mkataba wa Kimataifa kuhusu haki za watu wenye ulemavu (UNCRPD) wa mwaka 2006 Ibara ya tisa (9) unazungumzia haki za watu wenye ulemavu kupata habari kwa kuwa kumekuwa na changamoto za kisheria hususani katika nyaraka zenye hati miliki:- Je, ni lini Serikali itaridhia Mkataba wa Kimataifa wa mwaka 2013 Marrakesh Treaty ambao unalenga kuondoa vikwazo mbalimbali vinavyozuia walemavu wasioona waweze kupata habari katika mifumo inayokidhi mahitaji yao?

Supplementary Question 1

MHE. AMINA S. MOLLEL: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante na nashukuru kwa majibu hayo yanayoonesha jitihada za Serikali katika kusaidia watu wenye ulemavu. Pamoja na hayo nina maswali mawili ya nyongeza. Kama alivyoeleza Mheshimiwa Naibu Waziri, ningependa kujua sasa (time frame) ni lini mchakato wa kukusanya maoni ya wadau utakamilika na kwa kuwa ni miaka minne sasa na wenzetu wa Kenya tayari wameshasaini mkataba huo.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili; kutokusainiwa kwa mkataba huu wa Marrakesh kumesababisha watu wenye ulemavu wasioona kushindwa kwenda na wakati na kuendelea kuwa maskini na hasa kutokana na kukosa fursa mbalimbali za kujiongezea kipato, fursa hizo ambazo zinapatikana kwenye maandishi zinazohusu maendeleo ya nchi lakini pia ulimwengu kwa jumla.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba majibu hayo.

Name

Eng. Stella Martin Manyanya

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Nyasa

Answer

NAIBU WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimshukuru sana Mheshimiwa Mollel kwa jitihada kubwa anayoifanya lakini pia yeye mwenyewe atakuwa shahidi, Mheshimiwa Rais wetu amekuwa ni mdau mkuu namba moja katika masuala yanayohusu watu wenye ulemavu na ndiyo maana unaona hata kwenye Baraza tayari kuna watu wenye ulemavu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa misingi hiyo jambo hili tunalichukua kwa uzito mkubwa na tutahakikisha kwamba mapema iwezekanavyo baada tu ya kumaliza hili zoezi wanaloendelea nalo lipelekwe kwenye vikao vya wataalam na kikao cha Makatibu Wakuu na hatimaye liende kwenye Baraza la Mawaziri. Mheshimiwa Waziri wangu amekuwa akilifuatilia sana suala hili na najua nadhani umeona hata anakuja kusisitiza kwamba tutafanyia kazi haraka iwezekanavyo ili watu wenye ulemavu wapate haki zao.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile nikijibu swali la pili ni kwamba, tunatambua watakapoweza kupata machapisho ya aina mbalimbali bila vikwazo itawasaidia pia hata wao kuona namna ya kuweza kuondokana na umaskini. Kwa hiyo, naomba sana ajue kwamba suala hili tumelichukua kwa uzito mkubwa ikizingatiwa kwamba wote sisi ni walemavu watarajiwa. (Makofi)