Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Richard Phillip Mbogo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nsimbo

Primary Question

MHE. RICHARD P. MBOGO aliuliza:- Katika mpango wa matumizi bora ya ardhi kwa Mkoa wa Katavi uliofanywa na Halmashauri ya Mpanda mwaka 2004 kwa kushirikisha ngazi ya Mkoa na ngazi ya Wizara, zililipwa sehemu za Hifadhi za Misitu North East Mpanda (JB94) na Msanginia (JB215) na ramani mbalimbali kuidhinishwa ikiwemo 48870, 48893 na 40250. Je, ni lini Serikali itabadili mipaka hiyo kwa mujibu wa Sheria ya Misitu ya 2002 (Namba 14) Kifungu cha 28?

Supplementary Question 1

MHE. RICHARD P. MBOGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
Pamoja na majibu ya Serikali, ningependa niikumbushe Serikali kwamba wakati Halmashauri ya Wilaya Mpanda inafanya mpango wa matumizi bora ya ardhi ilizingatia mahitaji ya wananchi pamoja na maendeleo yao kwa wakati huo, kwa sasa hivi tunavyozungumza Wilaya ya Mpanda, Mkoa wa Katavi idadi yake ya wananchi imeongezeka. Haya matangazo ya Serikali, Tangazo Na. 447 ya mwaka 1954 Na. 296 ya mwaka 1949 hayaendani na uhalisia na hali ilivyo chini kutokana na ramani hizi kuidhinishwa na Wizara ya Ardhi mwaka 2008 na zilianza kuidhinishwa na ngazi ya Mkoa mpaka na Wizara ya Ardhi kwa Kamishna wa Upimaji na Ramani. Kwa sasa hivi tunaenda kwenye nchi ya viwanda na maeneo mengi yanahitaji wakulima kwa ajili ya kulima mazao mbalimbali na Mkoa wa Katavi tuna mkakati wa kuanzisha zao la korosho. Kulingana na matangazo ya Serikali yanatofautiana na ramani zilivyo, uhalisia na mahitaji ya wananchi. Je, Mheshimiwa Waziri yuko tayari hii Kamati ya Ushauri ya Taifa juu ya Misitu iambatane na Mbunge wa Jimbo la Nsimbo baada ya Mkutano huu wa Tisa kwenda kuangalia hali halisi ili waweze kumshauri Waziri na waweze kubadilisha mipaka kwa mujibu wa kifungu cha 29 cha Sheria ya Misitu ya mwaka 2002?
Swali la pili, kutokana na uhitaji mkubwa wananchi kwa maeneo haya na masika tayari imekwishaanza na tunajua Waziri wa Maliasili na Utalii kwa mujibu wa Sheria ya Misitu ya mwaka 2002 yeye ndiye mwenye dhamana ya kutoa kauli. Je, yuko tayari kuwaruhusu wananchi katika Kijiji cha Matandarani na Igongwe Kata ya Isalike waweze kupata maeneo ya kujihifadhi kwa kulima, wakati Kamati ya ushauri ikiendelea kupitia maeneo na kuweza kumshauri Waziri?

Name

Japhet Ngailonga Hasunga (CPA)

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Vwawa

Answer

NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza tuko tayari baada ya Mkutano huu wa Tisa kumalizika Kamati ya Ushauri itapita maeneo yote ambayo yana migogoro nchi nzima ili iweze kumshauri Mheshimiwa Waziri na aweze kutoa maamuzi sahihi.
Swali la pili, kuhusu kulima ni kweli wananchi wale nimefika katika lile eneo wana matatizo mengi, lakini ninaomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge tulipokaa na Mheshimiwa DC pamoja na Mwenyekiti wa Halmashauri walikubali kwamba wametenga eneo la ekari zaidi ya 700 ambalo sasa linatolewa kwa wananchi wale ili waweze kuendelea na hizo shughuli. Kwa hiyo, hatutaweza kuruhusu kwa sasa hivi waendelee na shughuli hizo kwa sababu tayari wameshaondolewa na ukiwaruhusu kupanda zao la korosho ambalo ni la muda mrefu mpaka lije lianze kuvunwa itakuwa ni muda mrefu sana, kwa hiyo tutakachokifanya ni kuwapeleka katika hayo maeneo ambayo tayari yameshatengwa na Serikali ili waendelee na shughuli zao zile ambazo zipo.