Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Leah Jeremiah Komanya

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. LEAH J. KOMANYA aliuliza:- Kutokana na msongamano mkubwa wa wagonjwa wa saratani katika Hospitali ya Ocean Road pamoja na gharama kwa ndugu wa wagonjwa ya kuwaleta na kuwauguza ndugu zao. Je, Serikali haioni haja ya kuanza kutoa huduma hiyo katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando?

Supplementary Question 1

MHE. LEAH J. KOMANYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na juhudi nzuri za Serikali, takwimu zinaonyesha kuwa, asilimia 60 ya wagonjwa wanaohudumiwa Hospitali ya Ocean Road wanatoka Kanda ya Ziwa, lakini katika huduma zinazotolewa kwa sasa katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando zipo changamoto kubwa ikiwemo uhaba wa fedha wakati wa ku-service ile mashine. Hospitali yenyewe haijitoshelezi na kusababisha huduma hiyo kusitishwa wakisubiri fedha na kuendelea kuleta usumbufu kwa wagonjwa katika Hospitali ya Ocean Road. Je, Serikali haioni haja ya kupeleka ruzuku ya kutosha katika kitengo cha saratani kilichopo Bugando?
Swali langu la pili, tafiti zinaonesha kuwa maji yaliyoachwa kwenye gari lililopo kwenye jua na yakakaa kwa muda mrefu katika vyombo vya plastiki inaonyesha inapopata joto kuna chemical zinatoka kwenye plastiki aina ya dioxin ambazo zinaonyesha kuna uwezekano wa kupata saratani hususani saratani ya matiti. Je, Wizara ina mikakati gani ya kutoa elimu kwa wananchi?

Name

Dr. Hamisi Andrea Kigwangalla

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nzega Vijijini

Answer

WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII (K.n.y. WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA WAZEE NA WATOTO):
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, kwanza kuhusu ruzuku kuongezwa kwa ajili ya kituo cha tiba ya saratani kilichopo Kanda ya Ziwa kwa maana ya Hospitali ya Rufaa ya Bugando ndiyo kwanza kimeanza kufanya kazi, kwa hiyo, tunatarajia uwepo wa changamoto mbalimbali ambazo zitajitokeza mpaka pale ambapo kita-stabilize. Kwa hivyo, ninaomba niichukue hii kama changamoto na tutatazama changamoto hii inasababishwa na nini ili wakati wa mchakato wa bajeti inayokuja, tuone ni kwa kiasi gani tunahitaji kuongeza ruzuku kwenye kituo hiki ili kiweze kutoa huduma bora zaidi katika mwaka wa fedha unaokuja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na swali lake la pili ambalo linahusu plastics ambazo zinatumika kuwekea maji ambayo yakikaa kwenye jua kwa muda mrefu inasemekana yanaweza yakasababisha saratani, hili ni jambo ambalo limekuwa likisemwa kwenye mitandao mara nyingi lakini halina ukweli wowote ule na naomba niwatoe wasiwasi Waheshimiwa Wabunge pamoja na wananchi wote kwamba Serikali iko makini na haiwezi kuruhusu kitu chochote kile ambacho kinauzwa kwa ajili ya matumizi ya binadamu na kikawa na madhara kikaingia kwenye soko, kwa sababu tunafanya uchunguzi pia tunafanya udhibiti wa bidhaa zote ambazo zinaenda kutumika kwa wananchi kupitia taasisi yetu ya Tanzania Foods and Drugs Authority (TFDA) - (Mamlaka ya Chakula na Dawa) ambapo mambo yote haya yakisemwa ama yakizungumzwa kwenye jamii huwa tunayafanyia utafiti wa kimaabara na hatimaye kuthibitisha kama yana ukweli ama hayana ukweli ndani yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hili analolisema Mheshimiwa Komanya tulikwishalifanyia kazi na tukabaini ni uzushi na halina ukweli wowote ule na kwa hivyo hakuna sababu ya kuendelea kuwatia wasiwasi wananchi.

Name

Abdallah Ally Mtolea

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Temeke

Primary Question

MHE. LEAH J. KOMANYA aliuliza:- Kutokana na msongamano mkubwa wa wagonjwa wa saratani katika Hospitali ya Ocean Road pamoja na gharama kwa ndugu wa wagonjwa ya kuwaleta na kuwauguza ndugu zao. Je, Serikali haioni haja ya kuanza kutoa huduma hiyo katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando?

Supplementary Question 2

MHE. ABDALLAH A. MTOLEA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali moja la nyongeza.
Hospitali ya Ocean Road ambayo ndiyo maarufu na inafanya kazi kubwa ya kuhudumia wagonjwa hawa wa saratani ndiyo hospitali ya siku nyingi na miundombinu yake pia ni ya kizamani lakini idadi ya wanaopata huduma hapo imeongezeka maradufu. Mbali na hayo hospitali ile haifikiki kirahisi kwa sababu iko pembeni na vituo au barabara za usafiri wa umma kwa maana ya daladala. Hivyo, wananchi wanatakiwa kutembea umbali mrefu kwa zaidi ya kilometa moja kufika hospitalini pale umbali huu si rafiki kwa mgonjwa au watu wanopeleka wagonjwa hospitali. Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga hospitali nyingine kubwa ya kisasa jijini Dar es Salaam ili kuzihamisha huduma hizi za magonjwa ya saratani ziweze kufanyika katika kituo kimoja kikubwa na cha kisasa?

Name

Dr. Hamisi Andrea Kigwangalla

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nzega Vijijini

Answer

WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII (K.n.y. WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA WAZEE NA WATOTO):
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa hatuna mpango kwa kweli wa kujenga kituo kingine cha kutoa tiba ya saratani katika Jiji la Dar es Salaam, kwa sababu kituo cha Ocean Road kinajitosheleza na kinajitosheleza kwa maana ya kutoa huduma kwa Kanda nzima ya Mashariki na hata wagonjwa wanaotokea Kanda ya Kati wanaweza wakapata huduma zao pale Ocean Road.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sababu ni moja kituo kile hakipaswi kuwa kama hospitali ya kwenda kila siku, kile kituo ni kituo cha rufaa. Kwa sasa kilikuwa ni kituo pekee cha rufaa cha Kitaifa lakini kwakuwa toka tumeingia Awamu ya Tano tumeanzisha utaratibu wa kufungua vituo vingine kwenye satelites/kwenye Kanda zote kwa maana ya Kanda ya Kusini pale Mbeya, Kanda ya Ziwa pale Bugando na Kanda ya Kaskazini pale KCMC ndio maana sasa tunakichukulia kituo hiki cha Ocean Road kama cha Kanda hii ya Mashariki na Kanda zozote zilizo karibu na Dar es Salaam.
Mheshimiwa Mwenyekiti, huduma ile ya saratani inayotolewa pale ni ya rufaa ni huduma ya ngazi ya juu kabisa, kwa hivyo kwa vyovyote vile hatuwezi kusambaza huduma hizi kila sehemu kwamba tuweke na upande mwingine, hapana. Hospitali kubwa zipo nyingi Dar es Salaam ikiwemo ile mpya ya Mloganzila ambayo itatoa huduma nyingine zozote pembeni lakini siyo huduma za saratani kwa sababu gharama za kuanzisha kituo cha saratani ni kubwa sana. (Makofi)