Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

George Malima Lubeleje

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mpwapwa

Primary Question

MHE. GEORGE M. LUBELEJE aliuliza:- Mpango wa MKURABITA ni muhimu katika kuwaletea wananchi maendeleo lakini unakabiliwa na tatizo kubwa la ukosefu wa fedha na hivyo kushindwa kuendesha shughuli za urasimishaji kwa ufanisi. Je, Serikali ina mpango gani wa kuanzisha mfuko wa urasimishaji utakaokuwa maalum katika Serikali za Mitaa ili kutatua tatizo la ukosefu wa fedha za kuendeleza shughuli za urasimishaji?

Supplementary Question 1

MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri sana ya Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora, nina maswali mawili.
Swali la kwanza, kwa kuwa MKURABITA katika Wilaya ya Mpwapwa walichagua vijiji viwili; Kijiji cha Inzomvu na Kijiji cha Pwaga, lakini kwa upande wa Kijiji cha Pwaga mambo ni mazuri, mradi ulitekelezwa, masijala ilijengwa na wananchi walipewa Hati za Kimila. Lakini katika Kijiji cha Inzomvu hakuna kilichofanyika, baada ya kupima mashamba wananchi walipewa mafaili tu wakaenda nayo majumbani, hakuna chochote na ofisi ya masijala haipo.
Swali la pili, Mheshimiwa Waziri utakubaliana na mimi kwamba ipo haja sasa ya Serikali kuleta muswada hapa ili tubadilishe chombo hiki MKURABITA ambao unategemea zaidi fedha za mfadhili na fedha za Serikali ni kidogo sana ili tubadilishe uwe mfuko wa urasimishaji ili wadau wengi waweze kuchangia na chombo hiki kiwe na fedha za kutosha ili wananchi wengi waweze kunufaika?

Name

Capt. (Mst). George Huruma Mkuchika

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Newala Mjini

Answer

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimefurahi kusikia kwamba Mpwapwa iliingia katika majaribio, walipata vijiji viwili, kijiji kimoja kinafanya vizuri kingine hakijafanya vizuri. Nimuombe tu ndugu yangu, Mheshimiwa George Malima Lubeleje apange muda anaoona yeye inafaa ili mimi na yeye twende katika kijiji hicho ambacho kimesahauliwa na mimi nikajifunze nikajue kimetokea nini, nichukue hatua ili vijiji hivyo pacha viweze kufanana katika utekelezaji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja kwamba kuletwe muswada utakaobadilisha chombo hiki, Serikali inapokea rai hii, lakini nataka nieleze kwamba kama nilivyosema tangu mwanzo tunakusudia kuanzisha Mfuko Maalum wa Urasimishaji, wakati wa kuanzisha mfuko maalum wa urasimishaji ikionekana haja iko ya kubadili sheria, suala hilo litazingatiwa na taratibu za kubadilisha sheria zinafuata ngazi kwa ngazi, itatekelezwa kadri Serikali itakapoona inafaa.