Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Peter Joseph Serukamba

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kigoma Kaskazini

Primary Question

MHE. PETER J. SERUKAMBA aliuliza:- Maji ni tatizo kubwa kwenye Jimbo la Kigoma Kaskazini:- Je, Serikali ina mpango gani wa kutatua tatizo hilo?

Supplementary Question 1

MHE. PETER J. SERUKAMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majawabu mazuri ya Naibu Waziri wa Maji, nina maswali madogo mawili ya nyongeza.
Swali la kwanza, Mradi wa Kalinzi huu ni mwaka wa tatu mfululizo zinawekwa fedha kwenye bajeti hazijawahi kuja, naomba leo Waziri alieleze Bunge lako, sasa fedha zilizotengwa mwaka huu zitakuja ili mradi huu uweze kutekelezwa?
Swali la pili, tunalo tatizo kubwa sana la mazingira, vijiji vyote alivyovitaja vinategemea kupata maji kwenye mito na ikifika kiangazi karibu yote inakauka, kwa hiyo tatizo linarudi kuwa palepale. Sasa, Serikali haioni imefika wakati kutumia maji ya Lake Tanganyika ili yaweze kuchukuliwa ili kupeleka maji kwenye vijiji vyote hivi?

Name

Eng. Isack Aloyce Kamwelwe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Katavi

Answer

NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imekuwa inatenga fedha kila mwaka kama alivyosema, lakini kutokana na matatizo ya upatikanaji wa fedha, na sisi sote ni mashahidi, uchumi umekumba dunia yote, kwa hiyo hali ya upatikanaji wa fedha ulikuwa kidogo mgumu. Lakini kwa sasa baada ya kuanza Serikali ya Awamu ya Tano ambayo inakusanya fedha vizuri nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba sasa fedha itapatikana.
Mheshimiwa Naibu Spika, na pili kwenye Programu ya Uendelezaji wa Sekta ya Maji ambayo tunashirikiana na wadau, mwezi Januari mwaka huu tayari tumeanza Programu ya Pili na tuna ahadi za kutosha za kupatiwa fedha kutoka kwa wadau tunaoshirikiana nao.
Kwa hiyo, nikuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba mradi huo sasa utatekelezwa na utafiti umeshakamilika kama nilivyojibu kwenye swali la msingi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali la pili ni kweli kwamba kipindi cha kiangazi maeneo mengi ya Jimbo lako, mito ile inayotiririsha maji inakauka. Lakini pia wewe mwenyewe ni shahidi kwamba sasa hivi kuna mradi mkubwa wa maji ambao tunajenga Mji wa Kigoma na tunachukua maji kutoka Ziwa Tanganyika na mpango huo kwa sasa Wizara ya Maji inataka kutumia vyanzo vyote vya maji ambavyo viko karibu na miji ambayo imepata bahati ya kuwa karibu na vyanzo vizuri vya maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo tumeanza mradi wa maji Mjini Kigoma, na kadri jinsi tutakavyokuwa tunakwenda, yale maeneo ambayo hayatakuwa na chanzo kizuri cha maji tutaendelea kutumia maji ya Lake Tanganyika kufika mpaka kwenye maeneo yenu.

Name

Kiteto Zawadi Koshuma

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. PETER J. SERUKAMBA aliuliza:- Maji ni tatizo kubwa kwenye Jimbo la Kigoma Kaskazini:- Je, Serikali ina mpango gani wa kutatua tatizo hilo?

Supplementary Question 2

MHE. KITETO Z. KOSHUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru kwa kunipa nafasi hii ya kuuliza swali fupi la nyongeza.
Wilaya ya Ilemela ilikuwa ina mradi ambao ulikuwa unatakiwa kukamilika mwaka 2014, mradi huu ambao ulitakiwa kuwanufaisha Kata za Wilaya ya Ilemela ikiwepo Kata ya Kayenze, Sangabuye, Shibula, Monze na Buswelu ambayo ni Kata Mama ya Wilaya ya Ilemela.
Je, ni lini mradi wa tenki hili la kutoa maji Wilaya ya Ilemela utakamilika?

Name

Eng. Isack Aloyce Kamwelwe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Katavi

Answer

NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kuna mradi umekuwepo Wilaya ya Ilemela na ulishindwa kukamilika. Tulipata matatizo kidogo baada ya kuanza Programu ya Sekta ya Maji Awamu ya Kwanza iliyoanza mwaka 2007, programu ilizinduliwa na Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Nne, lakini kwa sababu fedha nyingi tulikuwa tunapata za wafadhili, ule mchakato wa manunuzi, kwa mfano mwaka 2007 ndiyo programu ilianza, lakini kuja kupata no objection ya kuanza kusanifu tuliipata Disemba mwaka 2009, utekelezaji wa miradi ukaanza mwaka 2012. Kwa hiyo, hicho ndiyo kitu ambacho kilifanya miradi mingi isikamilike.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa tunatoa ahadi kwamba miradi yote ambayo haikukamilika tunaanza nayo tukamilishe ndiyo tunaingia kwenye miradi mipya. Mheshimiwa Mbunge nikuhakikishie kwamba Kata zako zote za Wilaya ya Ilemela katika Programu ya Pili ya Mpango wa Maji itafikiwa na itakamilika.

Name

Frank George Mwakajoka

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Tunduma

Primary Question

MHE. PETER J. SERUKAMBA aliuliza:- Maji ni tatizo kubwa kwenye Jimbo la Kigoma Kaskazini:- Je, Serikali ina mpango gani wa kutatua tatizo hilo?

Supplementary Question 3

MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa sababu matatizo ya maji katika jimbo langu yanafanana sana na Jimbo la Kigoma Kaskazini, ninapenda nimuulize Mheshimiwa Waziri swali la nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni lini Serikali hii itakamilisha Mradi wa maji katika Mji wa Tunduma kwa sababu imekuwa inaahidi mara nyingi kwamba itatengeneza maji na hata wakati Mheshimiwa Rais anaomba kura kwa wananchi pia alisema kwamba ataweza kuwaletea maji haraka iwezekanavyo ndani ya mwaka mmoja mradi utaanza kutekelezwa. Leo hii kuna kampuni ambayo tayari imekubali kujenga…
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mwakajoka, swali si umeshauliza? Nadhani swali umeshauliza, kwamba huo mradi utakamilika lini?
MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa nataka nikumbushe kidogo kwa sababu kuna kampuni leo imekuja hapa na mradi ule umeshapitishwa na Wizara lakini tunashangaa Wizara ya Fedha hawataki kukubali mradi ule uanze kujengwa haraka. Kwa sababu mradi ule ulitakiwa uanze kujengwa mwanzoni mwa mwaka huu lakini mpaka sasa hivi hakuna kinachoendelea. Tunataka kupata majibu.

Name

Eng. Gerson Hosea Lwenge

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wanging'ombe

Answer

WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa Serikali ya Awamu ya Tano imedhamiria kuwapatia wananchi wote maji safi na salama kwa kiwango cha asilimia 85 ifikapo mwaka 2020. Kwa hiyo, naomba nikuhakikishie, hayo unayoyazungumza ni historia, Serikali inakwenda kutekeleza Mradi wa Maji Tunduma ambao nina uhakika na tuwashauri wananchi wa Tunduma waiamini Serikali ya Awamu ya Tano. Ahsante.