Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Fakharia Shomar Khamis

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. FAKHARIA SHOMAR KHAMIS aliuliza:- Baadhi ya wafanyakazi wamejiunga na Mfuko wa NSSF na hukatwa sehemu ya mishahara yao kwa ajili ya kuwekeza ili iwasaidie baada ya kustaafu. Je, mpaka sasa ni wafanyakazi wangapi wamejiunga na Mfuko huo? Je, ni wafanyakazi wangapi wamestaafu kazi na kulipwa fedha zao na Mfuko huo? Je, ni nani analipwa faida inayopatikana kwa fedha za Mfuko huo kutoka benki zinakowekwa?

Supplementary Question 1

MHE. FAKHARIA SHOMAR KHAMIS: Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwanza sina budi kumshukuru Mhehsimiwa Naibu Waziri kwa maelezo yake mazuri yenye fasaha na yenye kueleweka lakini nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, napenda kujua kwa sasa hivi Mfuko huo unatoa riba ya kiasi gani kwa wastaafu kama gawio lao?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, ingawa jibu la swali langu kipengele (c) ameelezea mapato yanayopatikana kwa wadau lakini hakuelezea mapato yanayopatikana kutoka kwenye miradi inayoendeshwa na taasisi hiyo jinsi yanavyowafaidisha wadau. Napenda kujua wadau wa Mfuko huo wanafaidika nini kutokana na miradi hiyo ya ujenzi wa majumba na kadhalika? (Makofi)

Name

Anthony Peter Mavunde

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Dodoma mjini

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA: Mheshimiwa Spika, katika swali lake la kwanza ameuliza ni riba kiasi gani wastaafu hawa wanapata. Kwa mujibu wa utaratibu wa mfumo wa hifadhi ya jamii katika nchi yetu, tunatumia kitu kinaitwa defined benefits ambapo mwanachama hulipwa kutokana na michango yake na mafao mbalimbali hupatikana kutokana na mfumo huu.
Mheshimiwa Spika, kuhusu riba ambayo anaipata msaafu kimsingi ni kwamba pensheni anayoipata mstaafu inatokana na michango ambayo amechangia lakini mstaafu huyu anakatwa asilimia 10 ya mshahara lakini mchango wa mwisho kwa maana mafao anayopata ya mwisho ni zaidi ya asilimia 72.5 ya mshahara wake wa miaka mitatu ya mwisho. Kwa hiyo, utaona ni kwa kiasi gani ile fedha ambayo ameiwekeza anakuja kuipata baadaye mara nyingi zaidi ya kile ambacho amekiweka. Anakatwa asilimia 10 lakini malipo yake ya mwisho ni asilimia 72.5 ya mshahara wa miaka mitatu.
Mheshimiwa Spika, swali lake la pili alitaka kujua mapato ya miradi hii inawanufaisha vipi wanachama ambao wamechangia. Katika mfumo huu wa uwekezaji ambapo Shirika la NSSF linafanya uwekezaji katika miradi mbalimbali, fedha inayopatika kwa maana ya mapato ndiyo hiyo ambayo huwa inaingizwa kwenye kikokotoo cha mwisho cha kumpa faida mwanachama ambaye amechangia. Pia tunayo miradi ya dhahiri ambapo kupitia miradi hii, unaona kabisa imeleta manufaa makubwa kwa Watanzania.
Mheshimiwa Spika, mfano, tunalo Daraja la Kigamboni ambalo ni matunda ya uwekezaji wa NSSF, daraja lile limetoa ajira lakini vilevile limeongeza mapato kwa shirika na vilevile watu wengi sasa wamerahisishiwa njia ya kwenda Kigamboni kwenda kufanya uwekezaji mkubwa ambao umeongeza tija katika Taifa letu.
Vilevile tuna uwekezaji katika kiwanda cha Mbigili na Mkulanzi pale Morogoro. Katika maeneo ambayo yametengwa, asilimia kubwa ya wananchi ambao wengine ni wanachama na wengine siyo wanachama watapata fursa kutokana na uwekezaji huu kupata mapato kupitia kiwanda kile cha sukari ambacho kinajengwa pale Morogoro.