Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Naghenjwa Livingstone Kaboyoka

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. NAGHENJWA L. KABOYOKA aliuliza:- Je, ni lini Serikali itatengeneza miundombinu ya maji katika Hifadhi ya Mkomazi ili kuzuia wanyamapori kuzurura kwenye makazi ya wananchi wakitafuta maji na kuharibu mazao yao?

Supplementary Question 1

MHE. NAGHENJWA L. KABOYOKA: Mheshimiwa Spika, ahsante, nina maswali mawili ya nyongeza kwa Mheshimiwa Naibu Waziri.
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, mwaka jana mwezi Julai tulikwenda na Mkurugenzi Mkuu wa TANAPA kutembelea vyanzo vya maji kutoka Milima ya Shengena ambayo inatiririsha maji mengi ambapo yanapita siyo mbali sana na hifadhi hii ya Mkomazi kwa upande wa Same Mashariki. Naye akaridhia kwamba kweli yale maji yangeweza kuchukuliwa na kusaidia sana ambapo yatakuwa ni maji ya kudumu kuliko haya mabwawa ambayo yanakauka mara kwa mara. Sasa nimuulize Mheshimiwa Waziri, je, kitu gani kimefanya ule mpango usitekelezwe na badala yake wanakwenda tena kuchimba mabwawa wakati tumeshaona mabwawa kwanza ni hasara kubwa na pili maji yake yanakauka kila mara? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili, je, Waziri yuko tayari kutuma wataalam wake wakatembelee tena hii mito hasa Mto wa Hingilili ambao ndiyo unashusha maji mengi na kulinganisha na tathmini yake na kuchimba mabwawa ni ipi rahisi? Ahsante. (Makofi)

Name

Eng. Ramo Matala Makani

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tunduru Kaskazini

Answer

NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, kuhusu swali lake la kwanza, anatoa taarifa juu ya ziara yake na Mtendaji Mkuu wa Mamlaka za Hifadhi za Taifa Nchini (TANAPA) kwenye Milima ya Shengena ambapo analiambia Bunge lako Tukufu kwamba waliweza kuona uwezekano kwamba eneo lile ni chanzo cha maji ambacho kingeaminika zaidi na kwa hiyo anataka kujua kwa nini Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii isingetumia chanzo kile badala ya vyanzo hivi ambavyo tumevieleza hapa vya kutumia maji kutoka ardhini.
Mheshimiwa Spika, masuala haya ambayo ni ya kisayansi msingi wake mkubwa ni utafiti na baada ya ziara anayoizungumzia, kilichofanyika ni kuangalia faida na hasara yaani cost benefit analysis na baadaye gharama za kuweza kutekeleza mradi ule wa kujenga miundombinu na kukusanya maji kutoka kwenye Milima ya Shengena na kuyafikisha kwenye maeneo yanayohitajika, katika hatua za awali, ilionekana kwamba gharama zake kwa sasa hivi hayawezi kuwa yanaweza kumudu kibajeti kuliko kujenga kisima au visima hivi tulivyovieleza hapa sasa hivi.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kwa kuwa hicho ni chanzo ambacho ni kweli kama alivyosema Mheshimiwa Mbunge kingeweza kuwa ni cha kuaminika na cha kudumu zaidi lakini kikwazo ni suala la uwezo wa kibajeti hatujafunga hilo dirisha. Hilo dirisha bado liko wazi lakini tusingeweza kukaa sasa kusubiri kufanya jambo kubwa na la gharama kubwa badala ya kufanya lile linalowezekana kwa sasa hivi.
Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge akubaliane na Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii kwamba kwa sasa tutaendelea kutumia njia hii ya visima vifupi na visima virefu wakati tukiwa tunaangalia uwezo wa kibejati utakapokuwa umepanda basi tutatekeleza lile la pili.
Mheshimiwa Spika, swali lake la pili kwa kweli linamezwa na swali la kwanza kwa sababu alitaka kujua kama tunaweza kutuma wataalam kwenda kuangalia ile mito ambayo iko kule na kuweza kuona kama inaweza kutumika kama vyanzo vya maji.
Mheshimiwa Spika, jibu lake ni lilelile tu kwamba katika mito anayoitaja hata kama tukienda sasa hivi itakuwa ni suala la kulinganisha gharama na kwamba Wizara imeona hatua hizi zinazochukuliwa kwa sasa hivi ni za mpito ambazo zinaweza kushughulikiwa na uwezo wa kibajeti uliopo, lakini njia zile nyingine za kudumu zaidi za muda mrefu zitaangaliwa hapo baadaye baada ya uwezo wa kibajeti kuwa umepanda.