Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Khadija Nassir Ali

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. KHADIJA NASSIR ALI aliuliza:- • Ni vifaa gani muhimu vimewekwa kwenye vifungashio vya akinamama wakati wa kujifungua (delivery kit) takribani 500,000 zinavyokusudiwa kusambazwa na Serikali? • Je, ni kwa nini Serikali inasuasua kwenye usambazaji wa delivery kits kama mkakati ulivyo? • Je, ni kwa kiasi gani agizo la Mwandoya la Serikali la kuanzisha huduma za upasuaji kwenye vituo vyote vya afya nchini limetekelezwa?

Supplementary Question 1

MHE. KHADIJA NASSIR ALI: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu ya Serikali, nina maswali mawili ya nyongeza.
Kwanza, ni lini Serikali itatoa ruzuku ya moja kwa moja kwa kinamama wanaojifungua ili kuondoa kadhia hii?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, Ilani ya Chama cha Mapinduzi ilielekeza kujenga vituo vya upasuaji kila kata. Je, ni lini Serikali itatekeleza agizo hili kibajeti? Nashukuru. (Makofi)

Name

Dr. Hamisi Andrea Kigwangalla

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nzega Vijijini

Answer

NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, kwanza nampongeza Mheshimiwa Khadija Nassir Ali kwa kuuliza swali la kisera ambalo limetupa fursa ya kufafanua mambo mbalimbali ambayo ni kipaumbele kwa Wizara yetu kwa sababu yanahusu kupunguza vifo vya wakinamama wajawazito na watoto na yeye kama Mbunge mwanamama nadhani anaguswa na mtazamo wetu kwamba hiki ni katika vipaumbele vyetu pale Wizarani.
Mheshimiwa Spika, ruzuku kutoka Serikali kuu kwenda Serikali za Mitaa kwamba ni lini itatoka? Nadhani hakufanya mazingatio ya kutosha kwenye majibu yangu ya msingi kwa sababu tayari hapa hapa tu nimezungumza tuna zaidi ya bilioni 66 ambazo tunazipeleka kwenye Halmashauri mbalimbali nchini kwa ajili ya kufanya maboresho kwenye vituo vya kutolea huduma za afya nchini. Na hiyo ni ruzuku kutoka Serikali kuu.
Mheshimiwa Spika, vilevile kwenye bajeti ya afya Fungu Namba 52 tumeweka bajeti ya dawa mbalimbali ambazo zinaenda kusaidia kupunguza vifo vinavyotokana na sababu mbalimbali za uzazi. Kwa mfano, tumeweka bajeti ya Uterotonic drugs kama Oxycontisin ambapo tunapeleka kwenye Halmashauri moja kwa moja, kwenye vituo vya kutolea huduma za afya.
Mheshimiwa Spika, pia tumeweka bajeti mahususi ya kutoa dawa za magnesium sulphate ambazo zinasaidia kutibu ugonjwa wa eclampsia (kifafa cha mimba) ambazo hizi ni katika sababu kubwa ambazo zinapeleka kupoteza maisha wakati wa uzazi.
Mheshimiwa Spika, pia Serikali Kuu inasaidia sana kwenye kuimarisha mfumo wa upatikanaji wa damu salama kwenye vituo vyote vya afya nchini na hii ni moja kwa moja tunatoa sisi tunapeleka msaada kule chini. Kwa hiyo, ruzuku tunatoa na tunatoa kwa kiasi kikubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba nisisitize hapa kwamba Wabunge wenzangu wote na Halmashauri zote nchini watambue jukumu la kupunguza vifo vinavyotokana na uzazi ni la kwao wenyewe kwenye Halmashauri husika. Ni lazima tufanye uwekezaji kwenye vituo vya kutolea huduma za afya, hakuna namna nyingine. Sisi Serikali kuu tunasaidia tu kujenga uwezo wa vituo vyetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, la pili, Ilani ya CCM haizungumzii kujenga vituo vya upasuaji kwenye kila kata, Ilani ya CCM inazungumzia ujenzi wa vituo vya afya (health centers) kwenye kila kata na zahanati kwenye kila kijiji. Ilani ya uchaguzi inakwenda sambamba na Mpango wa Maendeleo wa Afya ya Msingi wa mwaka 2007/2017 ambapo Halmashauri zote nchini zinapaswa kujenga vituo vya afya kila Kata na zahanati kwenye kila kijiji.
Mheshimiwa Spika, kwa msingi huo, jitihada bado zinaendelea kwenye Halmashauri mbalimbali nchini na sisi kama nilivyosema kwenye majibu yangu ya awali, tunaendelea kujengea uwezo lakini pia ku-support halmshauri zetu kutimiza azima hii iliyowekwa kwenye Ilani ya uchaguzi ya CCM. (Makofi)