Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Mbaraka Kitwana Dau

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mafia

Primary Question

MHE. MBARAKA K. DAU (K.n.y- MHE. HAWA M. CHAKOMA) aliuliza:- Kisiwa cha Mafia kina vivutio vingi vya utalii kama viumbe wanaoishi kwenye maji, mikoko na kadhalika lakini vivutio hivyo havijatangazwa vya kutosha:- Je, Serikali ina mkakati gani wa kutangaza utalii wa Kisiwa cha Mafia?

Supplementary Question 1

MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Mafia ina vivutio vingi sana akiwemo huyu samaki wa ajabu anayeitwa Potwe au whale shark. Vile vile Mafia kuna maeneo mazuri sana ya scuba diving, sports fishing na kuna fukwe tulivu. Pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri Mafia kama Wilaya mpaka leo haina Afisa wa Utalii. Sasa swali la kwanza, ni lini Serikali itatupatia Afisa wa Utalii katika Wilaya ya Mafia?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, ni lini Serikali itaruhusu
au itaifungulia ile hoteli ambayo Mheshimiwa Simbachawene alikuja akaifunga ya Chole Mjini, ambapo wananchi wanapata pale ajira, Serikali inapata kodi na wale wawekezaji pale walikuwa wanasomesha vijana wengi katika kisiwa cha Chole, sasa ni nini tamko la Serikali juu ya kuondoa tofauti zilizokuwepo ili ile hoteli iendelee kufanya kazi? Ahsante.

Name

Eng. Ramo Matala Makani

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tunduru Kaskazini

Answer

NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, kuhusu swali lake la kwanza nakubaliana na yeye na Serikali inatambua kwamba, Mafia ni Kisiwa tajiri cha vivutio vya utalii; na kwa kweli Mafia ni mojawapo ya maeneo nchini ambayo yataiwezesha Serikali kufikia malengo yake ya ku-diversify, kutanua wigo wa aina ya vivutio, lakini pia kutanua wigo wa kufanya utalii maeneo mengi zaidi nchini kuliko maeneo machache ambayo yanaendelea hivi sasa. Kwa hiyo, ule umuhimu wa Mafia tayari Serikali inaufahamu na inaufanyia kazi.
Mheshimiwa Spika, lakini kuhusiana na hoja yake ambayo ni ya msingi kabisa ya kwamba ili tuweze kufikia malengo katika hayo ni vema tukawa na Afisa Utalii kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Mafia, nakubaliana naye. Hata hivyo, nimshauri tu Mheshimiwa Mbunge kwamba suala hili ni vema akaenda kulipeleka kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Mafia ili waweze kuangalia kwa namna gani wanaweza kuingiza kwenye ikama nafasi hiyo ya Afisa Utalii.
Mheshimiwa Spika, kuhusu swali lake la pili la hoteli aliyoitaja, hoteli ya Chole pale Mjini Mafia, licha ya faida zote alizozitaja ni kweli Serikali inafahamu kulikuwa na fursa za ajira za wananchi na faida nyingine kama ambavyo ameweza kuzigusia, lakini kulikuwa na changamoto za kimsingi ambazo ni za kisheria na ndiyo maana Mheshimiwa Waziri alipokwenda kule Mheshimiwa Simbachawene alichukua hatua aliyoichukua na kuweza kusimamisha uendeshaji wa hoteli ile.
Mheshimiwa Spika, lakini ametoa maoni ambayo nayapokea na hivyo ndivyo ambayo tunafanya hivi sasa kufanya mawasiliano kati ya Wizara ya Maliasili na Utalii na Wizara ya TAMISEMI. Mawaziri wawili hawa wanaendelea kulijadili na kulitazama ili hifadhi za malikale ziweze kutumika kwa mujibu wa sheria inayotakiwa, lakini pia shughuli za utalii zifanyike kwa mujibu wa sheria tulizojiwekea.