Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Martha Jachi Umbulla

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. MARTHA J. UMBULLA aliuliza:- Vifo vya akinamama na watoto kwa takwimu za hivi karibuni Mkoani Manyara vinatisha:- Je, Serikali inatoa kauli gani ya mwisho ili kukabiliana na janga hili ikiwepo kuimarisha Vituo vyote vya Huduma ya Mama na Mtoto Vijijini bila kujali uwezo wa wanawake kulipia au kutolipia huduma hiyo?

Supplementary Question 1

MHE. MARTHA J. UMBULLA: Mheshimiwa Spika, nashukuru. Kwanza nimshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake ya jumla kuhusu swali hili. Pamoja na hayo nina maswali mawili ya nyongeza, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, kwa kuwa takwimu za vifo vya akinamama vinavyotokana na uzazi katika Mkoa wa Manyara vinaongezeka mwaka hadi mwaka. Kwa mfano, mwaka 2015 tulikuwa na vifo 38, mwaka 2016 vifo 49 na nusu mwaka tu ya 2017 tayari vifo 23.
Kwa kuwa Mheshimiwa Naibu Waziri katika majibu yake amesema wameanzisha Benki ya Damu katika Mikoa ya Geita, Simiyu, Mara na Kigoma na sijasikia Mkoa wa Manyara; na kwa kuwa pia amesema wamejengea uwezo Wahudumu wa Afya nchi nzima bila kutaja Manyara. Je, Mheshimiwa Naibu Waziri atakubaliana nami kwenda katika Mkoa Manyara kuangalia hali hii ikoje ili kupatia ufumbuzi wa haraka janga hili katika mkoa wetu?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa vifo vingi
vya watoto wachanga vinatokana na kukosa na huduma upasuaji na huduma ya damu kwa ajili ya akinamama wajawazito; na kwa kuwa pia amesema kwamba wamewezesha vituo 159 nchi nzima bila kutaja katika hivyo 159 vingapi vipo Manyara na katika vituo vya afya 106 vilivyojengewa uwezo kwa njia ya mafunzo hajataja Manyara. Je, anaweza akaniambia kwamba hali ikoje katika kuwezesha vituo vya upasuaji katika mkoa wetu?

Name

Dr. Hamisi Andrea Kigwangalla

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nzega Vijijini

Answer

NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze sana Mama yangu mpendwa, Mheshimiwa Martha Umbulla kwa kufuatilia kwa ukaribu sana mambo yanayohusu Sekta ya Afya kwa Mkoa wa Manyara hususani mambo yanayohusu wanawake na watoto kwenye mkoa wake. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali lake la kwanza, halikuwa
swali per se, nikubaliane naye niko tayari kwenda Manyara wakati wowote atakapoona inafaa. Nimkumbushe tu kwamba toka nimeteuliwa kuwa Naibu Waziri nimeshafika Mkoa wa Manyara zaidi ya mara tatu na nimefika mpaka anapokaa yeye, jirani na nyumba anayoishi pale Dongobesh.
Mheshimiwa Spika, bahati mbaya yeye hakuwepo
lakini nimefika mpaka Dongobesh, nimefika mpaka kwenye kituo cha afya ambacho yeye Mbunge wa Viti Maalum na rafiki yangu Mheshimiwa Flatei Massay wanajenga na nikawapongeza sana kwa jitihada wanazofanya za kujenga kituo kile cha afya na kuleta hizi huduma za upasuaji karibu zaidi na wananchi wa Dongobesh. Niwashukuru kwa kunipa Uchifu wa pale Dongobesh na kunivalisha yale mavazi yenu ya kimila. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nilipofika pale niliguswa na nikajitolea mimi mwenyewe bati 100 kwa ajili ya kuwasaidia kwenye jitihada hizo. Kwa hivyo, akiniambia specifically nitaje vingapi, sikumbuki ni vingapi tulivyonavyo pale, lakini nafahamu Mkoa wa Manyara wanafanya jitihada kubwa sana za kuboresha huduma za Mama na Mtoto hususani kwa kupandisha hadhi zahanati zao kwenda kwenye vituo vya afya na mimi mwenyewe nimefika pale nikashuhudia mradi wao huu wa pale Dongobesh.
Mheshimiwa Spika, kwa msingi huo, niruhusu tu nifanye utafiti nitampa majibu ya statistics anazozitaka baadaye kwamba ni vituo vingapi hasa. Hata hivyo, azingatie agizo ambalo nililitoa mimi mwenyewe nikiwa Mwandoya kwa Mheshimiwa Mpina, ambapo nilisema kwamba, Halmashauri zote nchini wahakikishe wanapandisha hadhi vituo vyao vya afya ambavyo vilikuwa havitoi huduma za upasuaji sasa vianze kutoa huduma za upasuaji wa kumtoa mtoto tumboni. Hii ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kuna damu salama na kuna huduma za uchunguzi wa magonjwa katika ngazi ya kituo cha afya.
Mheshimiwa Spika, nilisema pia kwamba kama kuna kituo ambacho kitakuwa hakijakidhi matakwa haya ya sera, maana yake tutakishusha hadhi kiende kuwa zahanati badala ya kukiita kituo cha afya jina tu wakati hakitoi huduma za kituo cha afya. Nilitoa miezi sita ambayo inakwisha sasa hivi. Miezi hii mitatu inayofuata, natuma timu yangu ya wataalam kwenda kukagua kwamba ni Halmashauri zipi zimetekeleza agizo lile, agizo la Mwandoya. Ma– DMO, Wakurugenzi na Wakuu wa Wilaya wote nchini wanajua.
Mheshimiwa Spika, kwa hivyo, kituo ambacho kitakuwa hakijakidhi hayo masharti, nitakishusha hadhi. Kwenye lile agizo langu nilisema nitapeleka taarifa yangu kwa Mheshimiwa Rais mwenyewe kwamba hawa ndiyo wateule wake ambao wanakubaliana na vifo vya akinamama wajawazito kwa sababu hawataki kutekeleza agizo ambalo lingeokoa maisha yao. Nina uhakika Mheshimiwa Rais atachukua hatua. Nimejibu kwa upana ili kuwakumbusha.
Mheshimiwa Spika, swali lake la pili kuhusu upasuaji, kwa sehemu nimelijibu. Kuhusu damu salama, kwa Mkoa wa Manyara kwa ujumla wake kwenye bajeti hii inayokuja, tumeweka kama Mkoa wa kipaumbele kwa ajili ya kuanzisha Benki Salama ile kubwa.
Mheshimiwa Spika, nilipofika pale Manyara miezi sita iliyopita nilihakikisha wana damu ya kutosha, lakini niliona kuna RMO pale alikuwa anasinziasinzia hivi kutekeleza mpango huu, tulishauriana na wenzetu wa TAMISEMI na tulikwishamtoa.

Name

Halima Ali Mohammed

Sex

Female

Party

CUF

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. MARTHA J. UMBULLA aliuliza:- Vifo vya akinamama na watoto kwa takwimu za hivi karibuni Mkoani Manyara vinatisha:- Je, Serikali inatoa kauli gani ya mwisho ili kukabiliana na janga hili ikiwepo kuimarisha Vituo vyote vya Huduma ya Mama na Mtoto Vijijini bila kujali uwezo wa wanawake kulipia au kutolipia huduma hiyo?

Supplementary Question 2

MHE. HALIMA A. MOHAMMED: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba nimuulize Mheshimiwa Naibu Waziri kwamba, je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha kwamba kwa kila Hospitali ya Halmashauri kunakuwepo huduma nzuri za watoto njiti kuliko ilivyo hivi sasa? (Makofi)

Name

Dr. Hamisi Andrea Kigwangalla

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nzega Vijijini

Answer

NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, ahsante. Mkakati tulionao kama Serikali tumetoa mwongozo sisi kama Wizara ya Afya, ambao unazitaka Halmashauri zote ambazo zinamiliki Hospitali za Wilaya kuhakikisha wana chumba maalum kwa ajili ya watoto njiti lakini pia wana chumba maalum kwa ajili ya Kangaroo Mother Care ambayo ni njia ya kisasa ya kuwalea watoto wachanga ambao wamezaliwa chini ya umri.
Mheshimiwa Spika, kwa hivyo, mkakati ndio huo sasa Halmashauri kutekeleza hilo ni jambo lingine, lakini agizo letu kama Serikali ni kuzitaka Halmashauri zote kuhakikisha zinafuata mwongozo wa kuanzisha huduma za njiti katika hospitali zao.

Name

Martha Moses Mlata

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. MARTHA J. UMBULLA aliuliza:- Vifo vya akinamama na watoto kwa takwimu za hivi karibuni Mkoani Manyara vinatisha:- Je, Serikali inatoa kauli gani ya mwisho ili kukabiliana na janga hili ikiwepo kuimarisha Vituo vyote vya Huduma ya Mama na Mtoto Vijijini bila kujali uwezo wa wanawake kulipia au kutolipia huduma hiyo?

Supplementary Question 3

MHE. MARTHA M. MLATA: Mheshimiwa Spika, ahsante.
Kwa kuwa wanawake wanaoishi katika Manispaa ya Singida na maeneo yanayozunguka Manispaa hiyo wamekuwa wakipata huduma kwenye Hospitali ya Mkoa pamoja na Sokoine lakini idadi yao ni kubwa kiasi kwamba inawazidi wale watoa huduma hali kukiwa na Hospitali ya Rufaa ambayo imeshajengwa tayari lakini bado Wizara haijaleta huduma yoyote kuboresha pale ili huduma zianze na kuokoa maisha ya wanawake wengi. Ni lini sasa Serikali italeta huduma kwenye Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Singida ili kuokoa maisha ya wanawake? Ahsante. (Makofi)

Name

Dr. Hamisi Andrea Kigwangalla

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nzega Vijijini

Answer

NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwanza nimpongeze yeye lakini pia nimpongeze RMO wa Singida rafiki yangu Dkt. Mwombeki kwa jitihada mbalimbali ambazo wanazifanya kuboresha huduma za wana Singida. Wamekuwa wakifanya mikakati mbalimbali ikiwemo kujenga hiyo Hospitali ya Rufaa mpya, nzuri na ya kisasa kabisa.
Mheshimiwa Spika, pia wamekuwa mkoa wa kwanza kuanzisha huduma za outreach, huduma za kuwafuata wananchi na kuwapa huduma za kibingwa kwenye vijiji vyote. Naona Mheshimiwa Spika sasa hivi hata hapa mkoani kwako zimefika na juzi zilikuwa pale Kongwa lakini waanzilishi ni Mkoa wa Singida. Niwaombe Wabunge wote wa-support mpango huu, wawasiliane na RMO wa Mkoa wa Dodoma ili waone ni namna gani wanaweza wakazipeleka hizi huduma kwenye mikoa yao.(Makofi)
Mheshimiwa Spika, baada ya bashirafu hiyo, jibu langu ni kwamba tayari huduma zimeshaanza kwenye Hospitali ya Rufaa anayoizungumzia lakini tunakwenda kwa awamu. Katika hatua ya kwanza tumeanza kutoa huduma za outpatient lakini kadri tunavyoendelea kuboresha huduma na kupata pesa za kuweza kuijengea uwezo hospitali ile, ndivyo tunapanda ngazi na kuongeza huduma moja baada ya nyingine.
Mheshimiwa Spika, kuanzisha hospitali siyo jambo dogo, linataka muda, rasilimali na hatutaki kukurupuka kwa sababu tunataka tuitendee haki hospitali ile nzuri ambayo imejengwa chini ya usimamizi wa RC aliyekuwepo Mheshimiwa Parseko Kone. Ahsante.