Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Maulid Said Abdallah Mtulia

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kinondoni

Primary Question

MHE. MAULID S.A. MTULIA aliuliza:- Sera yetu ya Afya ni kuchangia gharama ili kupata huduma ya afya isipokuwa kwa wazee, mama na mtoto:- Je, ni fedha kiasi gani zimekusanywa kutokana na tozo za uchangiaji gharama ndani ya miaka mitano na ni nini matumizi ya fedha hizo?

Supplementary Question 1

MHE. MAULID S.A MTULIA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza. La kwanza, naungana naye katika umuhimu wa watu wetu kuchangia gharama, lakini anaonaje sasa Serikali dhana ya kuchangia gharama ikabaki katika kuchangia dawa pamoja na vipimo lakini wananchi wetu wakapata fursa ya kwenda kumwona Daktari bila kulipa pesa ya kumwona Daktari ili kuongeza idadi ya watu wanaokwenda kwenye vituo vya afya?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa kuna makundi yetu maalum ambayo kwa mujibu wa sheria yetu wanatakiwa wapate huduma za afya bure na kwa kuwa Wabunge wengi wamesimama hapa na mimi mmojawapo tunaonesha kwamba bado makundi haya hayapatiwi huduma ya afya bure. Je, Mheshimiwa Waziri atakuwa yuko tayari sasa kufuatana na mimi kwenda katika hospitali zangu za Jimbo la Kinondoni kwenda kusisitiza na kuhakikisha wananchi hawa wanapata huduma bure?

Name

Dr. Hamisi Andrea Kigwangalla

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nzega Vijijini

Answer

NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, ahsante. Swali lake la kwanza kuhusu wananchi kupewa ruhusa ya kwenda kununua dawa na vifaa tiba katika hospitali lakini wakaonwa bure na Madaktari, sisi kama Serikali hatuna utaratibu huo kwa sababu tunafanya kazi kwa mujibu wa sera lakini pia mipango mbalimbali ya kimkakati ya kuhudumia wananchi.
Mheshimiwa Spika, tunafuata Sera ya Afya ya mwaka 2007 pia Mpango wa Kimkakati wa Huduma za Afya Na.4 ambao unaanza 2015 - 2020. Pamoja na mikakati mbalimbali kama Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa na yote haizungumzii uelekeo huo.
Mheshimiwa Spika, kwa hivyo, mwongozo ambao tunaufuata sisi kama Serikali ni kuwahudumia wananchi zaidi kwa kutazama mipango hiyo na uelekeo wetu kwenye mipango yote hii ni kuelekea kwenye universal health coverage ambapo kutakuwa kuna bima ya lazima ya kila Mtanzania. Tukianza kutekeleza mpango huo kama Bunge lako Tukufu litatupitishia sheria ambayo tunakusudia kuileta muda si mrefu basi kila Mtanzania atalazimika kuwa na kadi ya bima ya afya ya namna moja ama nyingine iwe ni CHF ama iwe ni Social Health Insurance kama NHIF.
Mheshimiwa Spika, kila Mtanzania akishakuwa na hiyo kadi yake maana yake sasa atakuwa anatibiwa kwa kutumia kadi ya bima ya afya. Huo ndiyo uelekeo na sio uelekeo anaouzungumzia Mheshimiwa Mtulia. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kuhusu makundi maalum, hata hili suala la makundi maalum kuhudumiwa chini ya kiwango japokuwa tunalikubali, lakini dawa yake hasa ni huu mfumo wa kuwa na bima ya afya ya lazima kwa kila Mtanzanzia ambapo yale makundi maalum ambayo yanapewa msamaha kisera maana yake yatakuwa yanakatiwa bima kabla hayajaenda kutafuta huduma.
Mheshimiwa Spika, kwa hivyo, wazee wote ambao wanastahili kupewa msamaha wa kupata huduma za afya basi wanakatiwa kadi za bima ya afya na Serikali kwa sababu wao wanapewa msamaha anapokwenda pale kutibiwa huwezi kubagua yupi ana kadi na yupi hana kadi, kila mtu ana kadi. Yupi kadi yake ni ya msamaha na yupi kadi yake ni ya kulipia, kila mtu atakuwa ana kadi na kila kadi itaheshimiwa na kituo chochote kile cha kutolea huduma za afya.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kwa msingi huo hata haya makundi maalum anayoyazungumzia yatapata huduma zilizo bora. Kwenye Ilani ya Uchaguzi kwa kuwa tunaelekezwa kufanya hivyo, namhakikishia miaka hii mitano haitakwisha kabla hatujaleta hapa Bungeni mapendekezo yetu ya Sheria ya Single National Health Insurance ambayo ni compulsory kwa kila Mtanzania.
Mheshimiwa Spika, kuhusu kufuatana naye, anajua yeye ni rafiki yangu halina shida, tutafute muda twende Kinondoni tukatembelee, japokuwa mimi nimeshafika Kinondoni mara nyingi sana. Ahsante.

Name

Hamidu Hassan Bobali

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Mchinga

Primary Question

MHE. MAULID S.A. MTULIA aliuliza:- Sera yetu ya Afya ni kuchangia gharama ili kupata huduma ya afya isipokuwa kwa wazee, mama na mtoto:- Je, ni fedha kiasi gani zimekusanywa kutokana na tozo za uchangiaji gharama ndani ya miaka mitano na ni nini matumizi ya fedha hizo?

Supplementary Question 2

MHE. HAMIDU H. BOBALI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Sera ya Taifa ya Wazee ya mwaka 2003 miongoni mwa privilege ambayo inawapa wazee ni kutibiwa bure lakini hivi sasa imekuwa kama ni uamuzi wa Daktari wa Kituo cha Afya husika ambaye anakuwepo pale. Kwa hiyo, mara nyingi wazee wamekuwa wakinyanyaswa kutokana na kukosekana kwa sheria. Mheshimiwa Waziri anatuthibitishia kwamba ni lini atatuletea Sheria ya Wazee ili kwenda sambamba na Sera ya Wazee ili wazee wetu waweze kutibiwa isiwe sasa ni privilege au maamuzi ya Daktari katika kituo husika?

Name

Dr. Hamisi Andrea Kigwangalla

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nzega Vijijini

Answer

NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, ni lini tutaleta mapendekezo ya kutungwa kwa Sheria ya Wazee kwenye Bunge lako Tukufu, hatuna uhakika ni lini exactly, lakini tutaleta sheria hiyo. Hata hivyo, mpaka sasa kuna mchakato unaendelea ndani ya Serikali na pindi tutakapopata idhini ya Baraza la Mawaziri ya kuleta sheria hiyo hapa Bungeni basi itafika. Kwa sasa tuna mchakato ndani ya Serikali, sheria hii ni muhimu.
Mheshimiwa Spika, pamoja na kutokuwa na sheria hii, tayari tumeshaanza kutekeleza afua mbalimbali ambazo zinawahusu wazee hususan kwenye sekta ya afya. Kwa mfano, tuna mkakati niliusema hapa wiki iliyopita wakati nikijibu maswali wa ‘Mzee Kwanza, Mpishe Mzee Apite’ ambao tumeu--roll out nchi nzima na mkakati huu wazee wameupenda na wameufurahia sana.
Mheshimiwa Spika, pia tumetoa mwongozo kwa kila Halmashauri nchini kuhakikisha zinawakatia kadi za CHF wazee wote ili waweze kupata huduma za afya kwenye vituo vyao. Tunachokifanya sisi ni kufanya maboresho ya huu Mfuko wa Afya ya Jamii yaani CHF ili uwe na value zaidi, uweze kumsaidia mtu kupata huduma palepale kwenye zahanati yake kijijini ama kwenye kituo cha afya na kuzunguka mkoa mzima yaani awe anapata referral kwa kutumia kadi ya CHF.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kama Halmashauri zita-comply kutekeleza mapendekezo yetu ya kuwa na kadi ya CHF kwa wazee wote ambao wanastahili kupewa kadi hizo za msamaha kwenye Halmashauri zao maana yake katika miaka hii miwili huduma za afya kwa wazee zitaboreka sana.