Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Ally Abdulla Ally Saleh

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Malindi

Primary Question

MHE. ALLY SALEH ALLY (K.n.y. MHE. MARYAM SALUM MSABAHA) aliuliza:- Wafanyakazi wa Kampuni mbalimbali nchini wamekuwa wakipata ajali wawapo kazini na baadhi yao kutopewa huduma ya matibabu na waajiri wao na kuishia kupata ulemavu wa kudumu:- Je, ni wafanyakazi wangapi wamepata stahiki zao baada ya ajali?

Supplementary Question 1

MHE. ALLY SALEH ALLY: Mheshimiwa Spika, ahsante. Majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri ni mazuri kabisa na juzi tu nilibahatika kupata mafunzo na Wajumbe wa Kamati ya Katiba na Sheria kuhusu Mfuko huu. Ni Mfuko mujarabu kabisa kwa watu wengi, lakini nina maswali mawili ya nyongeza. Kwanza Naibu Waziri anaonaje akieneza elimu ya Mfuko huu ambao mafao yake yametandawaa na yanaweza kuwafaa watu wengi sana? Anaonaje kukuza elimu ili wafanyakazi au waajiri wengi waweze kujiunga?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, je, Serikali haioni sasa ni wakati wa hata Wabunge kuingizwa katika Mfuko huu kwa sababu ya manufaa yake ambayo hayawi-covered na Bunge lenyewe au na Mifuko mingine ya kijamii? Ahsante.

Name

Anthony Peter Mavunde

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Dodoma mjini

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (KAZI, VIJANA NA AJIRA):
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza kuhusu elimu, Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi umeendelea kutoa elimu katika ngazi za Mikoa na mpaka Taifa na kuhusisha taasisi mbalimbali na lengo lake ni kuendelea kuwajengea umma wa Watanzania uelewa juu ya Mfuko huu na vilevile mafao yanayotolewa na Mfuko huu.
Mheshimiwa Spika, kwa taarifa tu ni kwamba Mfuko huu unakuja kutibu lile tatizo la miaka mingi ya malipo ya fidia kwa wafanyakazi ambapo kwa mujibu wa Sheria ya mwaka 1949 malipo ya mfanyakazi aliyekuwa akiumia kazini ilikuwa ni takribani kiasi cha Sh.108,000 lakini sasa sheria hii imekuja kutibu changamoto hiyo na tumeendelea kutoa elimu kuhusiana na Mfuko huu.
Mheshimiwa Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tutaendelea kutoa elimu zaidi ili wananchi na hasa wafanyakazi na waajiri wote wauelewe vema na waweze kuitii sheria hii.
Mheshimiwa Spika, swali la pili la nyongeza ameuliza kuhusu Wabunge kuingizwa katika utaratibu huu. Kwa mujibu wa Mwongozo wa Mfuko huu, una-cover both private sector and public sector. Tumepokea maoni ya Mheshimiwa Mbunge ambayo yanahitaji majadiliano, lakini kwa sasa niseme pindi pale jambo hili litakapofanyiwa kazi tutaona namna ya kushirikisha taasisi hizi mbili na kuona uwezekano wake.