Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Taska Restituta Mbogo

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. TASKA R. MBOGO aliuliza:- Mkoa wa Katavi ni miongoni mwa mikoa ambayo ina vivutio vingi vya utalii kama vile Mbuga ya Katavi yenye wanyama wengi, kivutio cha pekee cha twiga weupe ambao hawapatikani mahali pengine popote duniani:- Je, Serikali ina mpango gani wa kukitangaza kivutio hiki pekee cha utalii?

Supplementary Question 1

MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Ninayo maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa ajili ya mahusiano ya ujirani mwema TANAPA Mkoani Katavi wamejitolea kuchimba visima kwenye vijiji vitatu ambavyo ni Kijiji cha Matandarani, Igongwe na Stalike lakini condition yao ni wanakijiji wachangie 30%. Gharama ya hivyo visima ni milioni 21, asilimia 30 itakuwa kama kwenye shilingi milioni saba, wanakijiji watatakiwa wachangie ili waweze kuchimbiwa hivyo visima vitatu. Je, TANAPA ili kudumisha mahusiano mema na Mkoa wa Katavi na ukizingatia kwamba kule mkoani kwetu vipato viko chini, wananchi hawana uwezo wa kuchangia hiyo shilingi milioni saba, inaonaje ikachukua hiyo gharama ikachimba bila kuwachangisha wananchi?Hilo swali la kwanza. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili, je, ni lini TANAPA itajenga hoteli ya nyota tatu katika Mkoa wangu wa Katavi ili tuweze kupata watalii kutoka nje na ndani ya nchi? Nauliza hivyo kwa sababu mkoa hauna hoteli ya nyota tatu ambayo inaweza kuwawezesha wageni kutoka nje kuja kutalii mkoa wetu na kuangalia huyo twiga mweupe ambaye hapatikani duniani kokote isipokuwa Mkoa wa Katavi?Ukizingatia kwamba sasa hivi uwanja wetu ni mzuri…

Name

Eng. Ramo Matala Makani

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tunduru Kaskazini

Answer

NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali lake la kwanza la uchangiaji kwenye utekelezaji wa miradi ya ujirani mwema na nafikiri niweke vizuri tu hapa kwamba, TANAPA hawajitolei bali wanatekeleza wajibu wao kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu kwamba pale ambapo kuna wananchi wanaishi jirani na maeneo ya hifadhi, mahali ambako utalii unafanyika tunao wajibu wa kuweza kutekeleza miradi mbalimbali chini ya utaratibu wa ujirani mwema.
Mheshimiwa Naibu Spika, mpango tulioweka wa kuchangia unawafanya wananchi waweze kwanza kushiriki moja kwa moja kwenye shughuli za uhifadhi lakini pia kujisikia kwamba na wenyewe ni sehemu ya uhifadhi lakini sehemu pia ya kufanya shughuli za maendeleo. Kwa hiyo, kwa kuwa utaratibu huu uko kwa mujibu wa kanuni, ikiwa Mheshimiwa Mbunge ana maoni bora zaidi ya haya aliyotuambia au ana namna bora zaidi ya kueleza kwa kirefu maoni hayo, basi anaweza kuyaleta Wizarani tukapitia utaratibu mzima wa utekelezaji wa miradi ya ujirani mwema.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali lake la pili, je, ni lini TANAPA itajenga hoteli ya nyota tatu Mkoani Katavi na kwa kweli anauliza kwamba kwa nini TANAPA wasijenge hoteli ya nyota tatu ili kuweza kuboresha shughuli za utalii Mkoani Katavi. Kwa ufupi tu ni kwamba, Serikali haijengi hoteli kwa ajili ya matumizi ya watalii au kwa ajili ya matumizi mengine yoyote kwenye sekta ya utalii.
Mheshimiwa Naibu Spika, jukumu la Serikali ni kuweka mazingira mazuri ya kuwawezesha wawekezaji ambao wanatoka private sector kuweza kuwekeza kwenye eneo hilo. Kwa hiyo, nimshauri tu Mheshimiwa Mbunge aungane na Serikali kuwashawishi wadau kutoka mahali popote pale waweze kuja kwenye Mkoa wa Katavi kuwekeza na kujenga hoteli si ya nyota tatu tu, hata kama wanaweza ya nyota nne, nyota tano, ili mradi kuwe na mazingira ambayo yatawawezesha watalii kuvutiwa na kuja kutalii wakiwa katika hali ambayo ni bora zaidi.