Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Susan Limbweni Kiwanga

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Mlimba

Primary Question

MHE. SUSAN L. KIWANGA aliuliza:- Serikali inafanya zoezi la kimya kimya la utafutaji wa mafuta na gesi katika Jimbo la Mlimba bila kutoa taarifa rasmi kwa wananchi juu ya zoezi hilo:- Je, Serikali inatoa kauli gani juu ya mchakato huo?

Supplementary Question 1

MHE. SUSAN L. KIWANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Najua Naibu Waziri haya majibu amepata kwa wataalam, lakini ukweli ni kwamba katika Jimbo la Mlimba hakuna Kijiji kinachoitwa Ipela Asilia. Ipela Asilia ipo Wilaya ya Malinyi, Halmashauri mpya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilivyofuatilia Malinyi, Madiwani hawana taarifa yoyote, hata Baraza la Madiwani halina taarifa yoyote kuhusu hizi taarifa, wanaona tu watu wanaingia na kutoka. Ni kweli kabisa pale uwezekano wa mafuta upo mkubwa sana, wameshachimba kisima kimoja cha mfano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa swali langu; kwa kuwa eneo hilo ni eneo nyeti, wanapatikana wale wanyama wasiopatikana duniani (puku), lakini Serikali inakwenda kutoa kibali cha kuchimba hayo mafuta na wananchi wanaozunguka hili eneo wamekatazwa kabisa kufanya shughuli za kibinadamu katika eneo hili.
MHeshimiwa Mwenyekiti, nataka majibu ya Serikali,
ni lini sasa watakwenda kuwaelimisha hawa wananchi na kuwapa wao maeneo ambayo wanaweza wakaendeleza shughuli zao za kilimo wakati mradi huu unaendelea na elimu haijatolewa katika kijiji hicho ambapo ni Kata ya Njiwa na Kata ya Itete; nimezungumza na Madiwani usiku.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la msingi; kwa kuwa amesema Mlimba; Mlimba katika Kata ya Mofu, Bwawa la Kibasila kuna utafiti ulifanyika na Mzee Magoma alikuwa Mkalimani wa wale Wazungu na ukweli ni kwamba Bwawa la Kibasila Kata ya Mofu, Kijiji cha Ikwambi kuna uwezekano mkubwa wa kupata mafuta kwa sababu kuna mikondo miwili inayotoka Ihenga na Mofu na Ikwambi na mkondo mwingine unatokea Mngeta, inakutana pale, kwa hiyo, wakasema kuna uwezekano mkubwa wa kupata mafuta.
Sasa nauliza swali hili kuhusu Jimbo la Mlimba; ni lini
sasa Serikali itakwenda katika Jimbo la Mlimba ikibidi waonane na huyu Mzee Magoma awaambie hali halisi, kwa sababu kuna uwezekano mkubwa wa kupata mafuta, lakini leo wamenijibu swali la Malinyi. Kwa hiyo, swali langu bado halijakidhi vigezo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. (Makofi)

Name

Prof. Sospeter Mwijarubi Muhongo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Musoma Vijijini

Answer

WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nipande kusema tu kwamba hatutakwenda kwa mzee yeyote kumuuliza uwezekano wa mafuta kupatikana, kwa sababu hili ni suala la kitaaluma, tutachukua utafiti uliofanywa Seismic Surveys ambayo kuna 2D na 3D, hizo ndizo zitakazotupeleka kule. Kwa hiyo, hatutakwenda kwa mzee.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine tena, mbali ya mchanganyiko wa majina, tunaomba radhi kama tumechanganya majina, lakini utafutaji wa mafuta, nataka kumweleza Mheshimiwa Mbunge kwamba, sehemu nyingine duniani watu wametafuta mafuta wameyakosa, lakini baada ya kubadilisha mbinu na namna ya kutafuta mafuta, wengine wakaja wakayapata. Kwa hiyo, hili ni jambo la kitaaluma na kitaalam, halina mjadala wa mambo ya kisiasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.