Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Josephine Tabitha Chagulla

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. JOSEPHINE T. CHAGULA aliuliza:- Serikali ilipandisha hadhi Kituo cha Afya Kharumwa kuwa Hospitali ya Wilaya Nyang’hwale. Je, ni lini Serikali itaongeza majengo kwa ajili ya wodi za wagonjwa na wodi za wazazi katika hospitali hiyo?

Supplementary Question 1

MHE. JOSEPHINE T. CHAGULA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Nimshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri na ya kutia moyo wananchi wa Nyang’hwale.
Mheshimiwa Spika, Kituo cha Afya cha Kharumwa kilipopandishwa hadhi na kuwa Hospitali ya Wilaya ya Nyang’hwale lakini bado hakijapata watumishi wa kutosha kulingana na hadhi hiyo ya Hospitali ya Wilaya. Je, ni lini Serikali itapeleka watumishi wa kutosha pamoja na vifaa tiba vya kutosha katika Hospitali hiyo ya Wilaya ya Nyang’hwale?(Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kumekuwa na msongamano mkubwa sana katika Hospitali zetu hizi za Rufaa kama vile Bugando na kwingine ukitaka kuonana na Daktari Bingwa; je, Serikali, haioni ni muda muwafaka sasa kuweza kupeleka Madaktari Bingwa wa watoto pamoja na akina mama katika hospitali zetu za Wilaya, ili kuondoa usumbufu huo usiokuwa wa lazima kwa wananchi? (Makofi)

Name

Selemani Said Jafo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kisarawe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, ni kweli kama alivyosema Mheshimiwa Mbunge ndiyo maana kwa haja ya Waheshimiwa Wabunge wa Geita hasa ndugu yangu Mheshimiwa Hussein Omar na Mheshimiwa dada yangu Josephine, katika Kituo hiki cha Afya cha Kharumwa kwanza, jambo kubwa tutakalolifanya, licha ya zile bajeti ambazo wenyewe wamezitenga, hivi sasa tutaenda kufanya ukarabati mkubwa wa kituo kile, tutajenga theatre ya kisasa. Lengo kubwa ni kwamba, wale Wasukuma wenzangu wa pale waweze kupata huduma nzuri. Kwa hiyo tutawekeza juhudi hii ya kutosha katika kile, kwa hiyo Mheshimiwa Mbunge naomba nikutoe hofu katika hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo tunafahamu kwamba changamoto kubwa ni changamoto ya wataalam na bahati nzuri kama ninavyofahamu hata zoezi hili la uhakiki wa watumishi hewa kwenye maeneo mbalimbali tumepata ripoti kwamba idadi ya watumishi hasa katika sekta ya afya, imeathirika sana. Pamoja na watumishi hewa, lakini pia kuna suala zima la ku-forge vyeti. Sasa hivi Serikali iko katika harakati mbalimbali za kuwaajiri watumishi wapya. Naomba nikutoe hofu Mheshimiwa Josephine kwamba tutakapotoa ajira hizi mpya, ambazo si muda mrefu Wizara ya Utumishi watatoa maelekezo nini cha kufanya, tutaelekeza watumishi katika eneo letu hili la Nyang’hwale ili wananchi wa eneo lile waweze kupata huduma nzuri.
Mheshimiwa Spika, kuhusu hoja hii nyingine ya msingi hasa suala zima la madaktari bingwa ni kweli na ndiyo maana leo hii, hasa magonjwa yale ya akinamama, wakati mwingine watu wengi wanatoka mikoani wanaenda Dar es Salaam kwa ajili ya kwenda kuwaona gynecologists. Na kwa sababu hii Serikali yetu inaangalia jinsi gani itafanya ili kuweka uwiano mzuri katika kada mbalimbali zitakazoajiriwa, lakini lazima kuelekeza hawa wataalam katika maeneo mbalimbali.
Mheshimiwa Spika, tukifanya hivyo tutapunguza hii changamoto ya wananchi ambao wengi wao kwenda muhimbili au kwenda sehemu nyingine yoyote ya mbali kwa kujisafirisha inakuwa kazi kubwa. Kwa hiyo Mheshimiwa Mbunge nasema hoja yako imekubaliwa, na katika hili Serikali tutafanya kila liwezekanalo kuhakikisha kwamba tunapeleka watalaam bingwa katika maeneo yetu haya.

Name

Janet Zebedayo Mbene

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Ileje

Primary Question

MHE. JOSEPHINE T. CHAGULA aliuliza:- Serikali ilipandisha hadhi Kituo cha Afya Kharumwa kuwa Hospitali ya Wilaya Nyang’hwale. Je, ni lini Serikali itaongeza majengo kwa ajili ya wodi za wagonjwa na wodi za wazazi katika hospitali hiyo?

Supplementary Question 2

MHE. JANET Z. MBENE: Mhehimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi. Mazingira anayozungumzia Mheshimiwa Chagula hayana tofauti na mazingira mengi ya Wilaya zetu na mikoa yetu ya pembezoni.
Mheshimiwa Spika, Wilaya ya Ileje ilibahatika kupata fedha kwa ajili ya kujenga Hospitali ya Wilaya ambayo imejengwa na sasa hivi imesimama karibu miaka miwili. Nataka kuomba kuuliza, je, Wizara ya TAMISEMI iko tayari kuimalizia hospitali hiyo kwa sababu ni hospitali kubwa na kwamba kama ingetumika vizuri ingesaidia kiasi kikubwa sana. Sasa hivi wagonjwa wetu wa-referral wanakwenda Malawi. Kwa sababu Mbeya ni mbali zaidi, wanakwenda Malawi kutibiwa sasa hii si sahihi. Mheshimiwa Waziri atuambie, je, itawezekana kututengea fedha bilioni 1.3 kwa ajili ya kumalizia hosptali ile?

Name

Selemani Said Jafo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kisarawe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, naomba tulichukulie jambo hilo kwa uzito wake na nakumbuka Mheshimiwa Mbunge hata wakati tunajadili mambo mbalimbali hasa katika jimbo lake la Ileje na hata kituo chake cha kimoja cha afya alikuwa akizungumzia suala zima la changamoto ya afya katika Halmashauri ya Ileje. Naomba nikuhakikishie kwamba tutahakikisha tunakamilisha hizo Hospitali za Wilaya ili kupunguza changamoto hizi.
Mheshimiwa Spika, jambo hili liko maeneo mbalimbali, liko Mvomero, Kilolo na maeneo mengine hospitali zime-stack. Kwa hiyo Mheshimiwa Mbunge siweze kuthibitisha kwamba by kesho tutatoa fedha, tunachokifanya Serikali kwa sababu tulikuwa na mchakato mpana wa kuhakikisha tunakabati vituo vya afya vipatavyo 100 na zoezi hili la kukarabati vituo vya afya 100 katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania litaanza ndani ya mwezi huu au mwezi ujao.
Mheshimiwa Spika, vilevile tutapeleka maelekezo makubwa kwenye Hospitali za Wilaya ambazo hazijakamilika, na tukimaliza hili tutakuwa tumehakikisha kwamba jukumu la Serikali yetu katika kuwahudumia wananchi litakuwa limefika mahali pazuri.
Kwa hiyo Mheshimiwa Mbunge naomba nikuhakikishie kwamba kwanza katika zile fedha za LGDG ambazo mwanzo zilikuwa sasa hivi tutaelekeza na kuweka nguvu vya kutosha ili fedha zote zipatikane. Vilevile tutazisimamia vizuri ili tuhakikishe kwamba tunamaliza suala hili la miundombinu ili wananchi wetu waweze kupata afya bora.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo nikuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali itashikirikiana nawe katika jimbo lako kuhakikisha sekta ya afya inakwenda vizuri.