Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Stella Ikupa Alex

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. STELLA I. ALEX aliuliza:- Asilimia kubwa ya watu wenye ulemavu wana vipato duni sana kiasi cha kushindwa kumudu ghamara za matibabu. Je, Serikali haioni kuwa ni muda muafaka sasa wa kuwajumuisha Watanzania hawa wenye kipato duni na wenye ulemavu kwenye sera ya msamaha wa uchangiaji huduma za afya kama ilivyo kwa wanawake wajawazito, watoto chini ya miaka mitano na wazee?

Supplementary Question 1

MHE. STELLA I. ALEX: Mheshimiwa Spika, ahsante. Kutokana na majibu mazuri ya Serikali kuwa msamaha wa matibabu utatolewa kwa mtu mwenye ulemavu ambaye atabainika hana uwezo; ikumbukwe kuwa ugonjwa unampata mtu bila taarifa.
Je, Serikali ina utaratibu gani wa kuwabaini watu wenye ulemavu wasio na uwezo ili waweze kupata msamaha huu wa matibabu?
Swali la pili, je, Serikali ipo tayari kuziagiza mamlaka husika na kutoa waraka ili majibu yaliyotolewa hapa leo yaweze kutekelezwa?

Name

Dr. Hamisi Andrea Kigwangalla

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nzega Vijijini

Answer

NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, maswali anayozungumzia Mheshimiwa Stella ni muhimu sana kama ulivyosema wewe mwenyewe na ni maswali yanayohusu uwiano na usawa kwenye jamii yetu, ambapo kama Taifa ni lazima tutoe uwiano sawa kwa watu wote bila ubaguzi wa aina yoyote ile kama ambavyo waasisi wa Taifa letu waliweka misingi kupitia sera yetu ya ujamaa na kujitegemea.
Mheshimiwa Spika, ni kwa msingi huo, Serikali kupitia
Sera yake ya Afya ya mwaka 2007 inatoa matamko ya kisera ya namna ambavyo makundi maalum kwenye jamii yanalazimika kuhudumiwa ikiwemo kundi hili la watu wenye ulemavu.
Mheshimiwa Spika, sasa utaratibu wa utekelezaji unawekwa na sheria na taratibu mbalimbali ndani ya Serikali. Katika awamu hii ya tano, tunakusudia kuleta hapa Bungeni mapendekezo ya Bima ya Afya ya lazima kwa watu wote ambapo ndani yake tutakuwa tumeweka utaratibu mahsusi wa kuhakikisha uwiano huu tunaouzungumza unatekelezeka kupitia Bima ya Afya ambapo tutaweka utaratibu sasa kwamba watu wanaopewa msamaha kwa mujibu wa sera, basi wawe na kadi ya Bima ya Afya kuliko ilivyo sasa. Kwa sababu inajitokeza katika nyakati mbalimbali ana msamaha anastahili kupata huduma bure, lakini anapofika kwenye kituo cha kutolea huduma, anakosa dawa ama anakosa vipimo fulani na analazima kwenda kwenye private. Kwa hiyo, hata ile bure inayokusudiwa na sera yetu inakuwa haipo.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, sisi ndani ya Serikali tunaamini kama tutafanikiwa kupitisha sheria hii ya Bima ya Afya kwa wote, utaratibu utakuwa mzuri. Kwa hiyo, anachokizungumzia sasa hivi tumekianzisha kwa mfano tu kwa kujaribisha kwenye kundi la wazee wenye umri wa zaidi ya miaka 60 wasiojiweza ambapo Halmashauri zinalazimika kuwabaini wazee wote katika eneo lao na kuwawekea utaratibu wa kuwapa kadi za CHF ili kujaribisha utaratibu tunaozungumza.
Mheshimiwa Spika, kwenye kundi la walemavu, bado hatujaanza.