Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Stanslaus Shing'oma Mabula

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nyamagana

Primary Question

MHE. STANSLAUS S. MABULA aliuliza:- Fedha zinazotengwa na Halmashauri kutokana na mapato ya ndani; asilimia 10 ya fedha hizo zinatakiwa kwenda kwa vijana na wanawake na zinatakiwa ziwafikie walengwa kila mwaka bila kukosa. Je, Serikali iko tayari kutoa agizo la msisitizo kwa Halmashauri zote nchini kutenga fedha hizo na wala wasichukulie kama ni hisani?

Supplementary Question 1

MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Spika, naomba kuuliza maswali mawili madgo ya nyongeza.
Swali la kwanza, pamoja na jitihada kubwa ambazo zimeshafanywa na Halmashauri yangu ya Jiji la Mwanza, namshukuru sana tu Mkurugenzi kwa jitihada zake anazozifanya kuhakikisha anasaidia wanawake na vijana wa Jiji la Mwanza kujikomboa.
Mheshimiwa Spika, niulize tu kwamba inawezekana haya yanafanyika vizuri kwenye Halmashauri ambazo Wakurugenzi wengi wana utashi wa kusaidia makundi haya. Ni nini sasa mkakati wa Serikali kuhakikisha kwamba fedha hizi zinapaswa kutolewa siyo kwa hiyari, iwe ni kwa lazima kwa mujibu wa makusanyo ya mapato ya ndani ili kuwanufaisha vijana wengi zaidi? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pili, je, Serikali haioni sasa ni wakati muhimu wa kuongeza asilimia hizi kutoka 10 mpaka 15 kwa sababu ni ukweli usiofichika kwamba vijana na wanawake wanaendelea kuongezeka zaidi hasa katika masuala mazima ya kujitafutia riziki na familia zao pia ili waweze kujikwamua kiuchumi? Nakushukuru. (Makofi)

Name

Dr. Selemani Said Jafo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kisarawe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mbunge anauliza kwamba ni jinsi gani tutaweka uwe kama mkakati wa kisheria; ni kweli ukija kuangalia hata taarifa ya Mkaguzi wa Hesabu za Serikali ya mwaka 2013/2014, kuna outstanding ya fedha ambazo zilitakiwa zipelekwe karibu shilingi bilioni 37 hazikuweza kupelekwa. Ndiyo maana katika bajeti ya mwaka 2016/2017 tulitoa maelekezo mahususi kwa Wakurugenzi wote kama ndiyo miongoni mwa guideline kutengeneza bajeti ya Halmashauri.
Mheshimiwa Spika, vilevile tuseme kwa kuwa tumeona
kuna changamoto kwa Halmashauri nyingine kutoa hizi fedha, ndiyo maana sasa hivi katika marekebisho yetu ya Sheria ya Serikali za Mitaa Sura ya 290, tumeweka kifungu ambacho kinatoa maelekezo ya kisheria sasa kwamba tunavyoipitisha hapa kwamba Halmashauri sasa haina hiyari isipokuwa ina lazima ya kutekeleza jambo hilo la kisheria.(Makofi)
Mheshimiwa Spika, lengo kubwa ni kuwasaidia vijana
na akina mama na kuzikomesha Halmashauri zote zinazoona kwamba kupeleka ile fedha kama ni hisani, kumbe ni utaratibu. Lazima tunataka tuingize katika utaratibu wa kisheria ambapo nina imani sheria ile ikifika ha Bungeni, Wabunge wote tutashirikiana kwa pamoja kuipitisha kwa sababu ina maslahi mapana kwa wananchi wetu.
Mheshimiwa Spika, katika jambo la pili la kuongeza asilimia 10 mpaka 15; nadhani ukiangalia mgao wa own source, asilimia kumi nadhani tuiweke hapo hapo, kwa sababu hata hizo asilimia kumi Waheshimiwa Wabunge wengine humu walikuwa wanalalamika. Jambo la kuzingatia ni kwamba tuhakikishe ile asilimia kumi inafika.
Mheshimiwa Spika, najua Mheshimiwa Mabula ni mpiganaji wa wananchi wake na mpiganaji wa Machinga pale Mwanza. Na mimi najua tukisimamia vizuri hapa kwa pamoja, jambo hili litawasaidia sana vijana na akina mama katika maeneo mbalimbali kujiingiza katika shughuli za ujasiriamali.

Name

Aida Joseph Khenani

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Nkasi Kaskazini

Primary Question

MHE. STANSLAUS S. MABULA aliuliza:- Fedha zinazotengwa na Halmashauri kutokana na mapato ya ndani; asilimia 10 ya fedha hizo zinatakiwa kwenda kwa vijana na wanawake na zinatakiwa ziwafikie walengwa kila mwaka bila kukosa. Je, Serikali iko tayari kutoa agizo la msisitizo kwa Halmashauri zote nchini kutenga fedha hizo na wala wasichukulie kama ni hisani?

Supplementary Question 2

MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru.
Pamoja na agizo la Serikali kwenye Halmashauri kuagiza kutenga asilimia kumi kwa vijana na wanawake, kumekuwa na utaratibu wa Halmashauri kugawa pesa hizi kipindi cha Mwenge. Kwa sababu Halmashauri nyingine wanawake wanapata changamoto sana kipindi cha kilimo, Serikali haioni ni hekima au busara kutoa pesa hizi kipindi cha msimu wa kilimo?

Name

Dr. Selemani Said Jafo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kisarawe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, nilizungumza mara kadhaa hapa, fedha zile hazitoki kwa Mheshimiwa Dkt. Mpango, fedha zile zinakusanywa katika Halmashauri zetu na Kamati ya Fedha inakaa na kufanya maamuzi fedha zile ziende wapi na kwa akina nani?
Kwa hiyo, jambo hili naomba niseme wazi, kama sisi Wabunge na Madiwani wetu tukiwa committed kuwasaidia wananchi wetu, haitaleta shida kabisa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, najua concern ya Mheshimiwa Mbunge, lakini niwaelekeze sana ndugu zangu Waheshimiwa Wabunge, twende sasa tukazihakikishe Kamati zetu za Fedha zinapokaa katika ile ajenda ya mapato na matumizi, katika own source, tutenge kabisa pale pale, tuzielekeze kwa vijana na akina mama waweze kujikomboa kwa kadri Serikali ilivyopanga. Huu ndiyo mchakato wa wazi kabisa, kila mtu ataona ni jinsi gani ameshiriki vyema kuhakikisha jamii yake inakwenda vizuri zaidi.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, namshukuru Mheshimiwa Mbunge.