Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Felister Aloyce Bura

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. FELISTER A. BURA aliuliza:- Serikali imeanzisha Benki ya Kilimo kwa lengo la kusaidia wakulima wakubwa na wadogo kupata mikopo ya pembejeo kwa haraka:- Je, ni lini Benki hiyo itaanza kutoa huduma kwa wakulima wadogo wadogo wa Mkoa wa Dodoma?

Supplementary Question 1

MHE. FELISTER A. BURA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza. Kwanza niipongeze Serikali kwa uamuzi wa kufungua Benki ya Maendeleo ya Kilimo Mkoani Dodoma na kukubali kutoa mafunzo kwa wakulima wadogo wadogo Mkoani Dodoma.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, kwa kuwa Benki ya Maendeleo ya Kilimo imeanzishwa kwa malengo ya kuwawezesha wakulima kupata mikopo kwa masharti nafuu na kwa haraka zaidi. Je, Serikali iko tayari kupunguza sasa riba ya Benki ya Maendeleo ya Kilimo ili wakulima wengi wapate kufaidika? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa Benki ya Maendeleo ya Kilimo ni mkombozi kwa wakulima. Je, Serikali iko tayari sasa kuhakikisha kwamba mikoa yote wanapata matawi ya benki hii ili wakulima wasihangaike kwenda Dar es Salaam na Dodoma kufuatilia mikopo?

Name

Dr. Ashatu Kachwamba Kijaji

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Kondoa

Answer

NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Felister kwa kuwa mbele katika kufuatilia miradi ya maendeleo ndani ya Mkoa wetu wa Dodoma. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la kwanza ameuliza kuhusu kupunguza riba. Kwanza nimkumbushe kwamba Benki hii ya Maendeleo ya Kilimo ilianzishwa kwa malengo makuu mawili. Moja ni kuchangia utoshelezi na usalama endelevu wa chakula nchini na pia kusaidia mapinduzi ya kilimo kutoka katika kilimo cha kujikimu na kwenda kilimo cha kibiashara.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kutimiza malengo haya, Benki ya Maendeleo ya Kilimo ili iweze kufanya kazi hizi ni lazima iwe na mtaji wa kutosha na pia imekuwa iki-lobby katika taasisi nyingine za kifedha ili ziweze kutoa mikopo katika sekta ya kilimo. Benki hii ili iweze kupata mtaji wa kutosha sasa hivi Serikali imeshairuhusu Benki ya Maendeleo ya Kilimo iweze kupata mkopo wa bei nafuu kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika na iko mbioni kuupata na nina uhakika itaweza kutoa mikopo hii kwa bei nafuu kwa wakulima wetu wadogo wadogo na wa kati.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili, ili kutimiza pia malengo haya Benki yetu ya Kilimo iliandaa mpango wa biashara wa miaka mitano ambao umeanza kutekelezwa kuanzia mwaka 2017 - 2021. Katika kutekeleza mpango huu wa biashara wa Benki yetu ya Maendeleo ya Kilimo imedhamiria kufungua ofisi sita za kikanda ndani ya Tanzania, ambazo ni Kanda ya Kusini, Kanda ya Kaskazini, Kanda ya Kati, Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Kanda ya Ziwa Viktoria pamoja na Zanzibar. Baada ya kufunguliwa ofisi hizi za kanda nchi nzima ni imani yetu sasa tutaweza kuwafikia wakulima wetu kule walipo.

Name

Amina Nassoro Makilagi

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. FELISTER A. BURA aliuliza:- Serikali imeanzisha Benki ya Kilimo kwa lengo la kusaidia wakulima wakubwa na wadogo kupata mikopo ya pembejeo kwa haraka:- Je, ni lini Benki hiyo itaanza kutoa huduma kwa wakulima wadogo wadogo wa Mkoa wa Dodoma?

Supplementary Question 2

MHE. AMINA N. MAKILAGI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuuliza swali moja la nyongeza. Kwa kuwa, wanawake wa Tanzania kwa kiwango kikubwa walio wengi ndiyo wakulima; na kwa kuwa wanawake wa Tanzania hawana fursa za kiuchumi zitakazowafanya wafikie Benki hii ya Wakulima kwa sababu ya kukosa dhamana. Napenda kujua Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha wanawake wengi ambao ni wakulima waishio vijijini wanafikia fursa hii ya kupata mikopo katika Benki ya Wakulima kwa lengo la kuwakomboa kiuchumi?

Name

Dr. Charles John Tizeba

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Buchosa

Answer

WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli wanawake wengi wa Tanzania ndiyo wanaojihusisha katika kilimo hapa nchini. Serikali kwa kutambua hilo imeweka mipango mbalimbali ikiwemo ukopeshaji wa vikundi vya akinamama katika uzalishaji kupitia Halmashauri zao lakini pia tunatoa kipaumbele katika Mfuko wa Pembejeo. Wanawake wanaokwenda kukopa katika Mfuko wa Pembejeo wanapata kipaumbele kwa sababu wao wanafahamika ndiyo wanaoshiriki zaidi katika shughuli za kilimo.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini sio Benki ya Kilimo tu inayotoa mikopo katika sekta ya kilimo, benki nne hapa nchini kwa sasa zinatoa fedha katika shughuli za kilimo. Utoaji wa fedha hizi hauko katika shughuli yenyewe ya kilimo tu, isipokuwa benki zinatoa fedha katika mnyororo mzima wa thamani katika kilimo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano Benki ya NMB mwaka huu pekee wa fedha imetenga shilingi bilioni 500 kwa ajili ya shughuli za kilimo na akinamama wana kipaumbele. Masharti ya mikopo katika benki ambazo tumezungumza nazo za NMB, Commercial Bank of Africa, CRDB, wote wamepunguza masharti katika mikopo ya kilimo ili kuwawezesha Watanzania wengi na hasa wale wasio na dhamana kuweza kupata mikopo hii kwa urahisi.

Name

Othman Omar Haji

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Gando

Primary Question

MHE. FELISTER A. BURA aliuliza:- Serikali imeanzisha Benki ya Kilimo kwa lengo la kusaidia wakulima wakubwa na wadogo kupata mikopo ya pembejeo kwa haraka:- Je, ni lini Benki hiyo itaanza kutoa huduma kwa wakulima wadogo wadogo wa Mkoa wa Dodoma?

Supplementary Question 3

MHE. OTHMAN OMAR HAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kwa mujibu wa Msajili wa Hazina, Benki ya Kilimo inawajibika kutoa huduma zake Tanzania nzima. Napenda kumuuliza Naibu Waziri, ni kwa nini benki hii haijafikisha huduma zake kule Visiwani Zanzibar?

Name

Dr. Ashatu Kachwamba Kijaji

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Kondoa

Answer

NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema kwenye jibu langu la Msingi, katika utekelezaji wa mpango wa biashara wa Benki hii ya Maendeleo ya Kilimo, imepanga kufungua ofisi sita za kikanda na Zanzibar ikiwemo. Ni imani yangu baada ya kufungua Ofisi ya Kikanda Dodoma, Ofisi ya Kikanda ya pili itakayofunguliwa ni Ofisi yetu ya Visiwani Zanzibar.