Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Godfrey William Mgimwa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kalenga

Primary Question

MHE. GODFREY W. MGIMWA Aliuliza:- Tatizo la mawasiliano ya simu katika Jimbo la Kalenga bado ni kubwa:- Je, ni lini Serikali itapeleka minara ya simu kwenye vijiji vya Kaning’ombe, Ikungwe, Lyamgungwe, Igunda na Ikuvilo.

Supplementary Question 1

MHE. GODFREY W. MGIMWA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Kwanza nimshukuru sana Mheshimiwa Waziri kwa kazi nzuri anayoifanya kupeleka mawasiliano katika Jimbo langu.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, swali hili nimeuliza mwaka 2014 nikajibiwa kwamba 2015 nitapata majibu ya uhakika, sikupata majibu. 2015 nikapata nafasi ya kuuliza nikaambiwa 2016, leo hii ni 2017 naambiwa ni 2018. Naomba niweze kupata majibu ya uhakika leo kwamba ni lini sasa vijiji hivi vilivyoorodheshwa vitapata minara ya simu na wananchi wangu waweze kupata mawasiliano hayo ya simu? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; katika minara ya simu ambayo inajengwa katika maeneo mbalimbali katika Jimbo langu la Kalenga service levy hailipwi moja kwa moja kwenye Halmashauri, inaenda kulipwa kwenye makampuni yenyewe ambayo mengi yapo Dar es Salaam. Wananchi katika Jimbo langu wanakosa mapato ya ndani kutokana na minara hiyo ya simu. Ningependa kujua kutoka Wizarani, je, ni namna gani sasa wanaweza kuwapelekea fedha hizi wananchi ambao nao wanatakiwa kwa namna moja au nyingine waweze kupata faida kutokana na minara hii ya simu, kwa sababu inayotumika pale ni ardhi?
Je, Serikali ina mkakati gani kuhakikisha kwamba fedha ambazo yanapata makampuni haya au faida ambazo zinapata kampuni hizi zinakwenda pia kuwasaidia wananchi katika maeneo husika? Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.

Name

Eng. Edwin Amandus Ngonyani

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Namtumbo

Answer

NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, tunapojibu maswali hapa huwa tuna dhamira ya dhati ya kutekeleza kile tunachokijibu na kwa kawaida Wizara huwa tunajiandaa kujipanga kutekeleza kile ambacho tunakijibu hapa. Inapofika wakati wa bajeti inaweza ikatokea kama ilivyotokea kwa eneo hili kwamba Mfuko wetu wa Mawasiliano kwa Wote huwa unakosa fedha, unapokosa fedha tunatarajia tuifanye hiyo kazi mwaka unaofuata, hiyo inabakia dhamira yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimhakikishie kwamba dhamira yetu ni kuhakikisha vijiji hivi kama tulivyosema katika jibu la msingi, tunavitekeleza katika mwaka huu wa 2017/ 2018 na fedha tunatarajia kuziomba na tunaamini mtazipitisha.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali la pili, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba ile minara ya simu pale inapojengwa kwa kawaida yale makampuni yanaingia mikataba na ama vijiji au mwenye ardhi husika, kwa kawaida Wizara hatuingilii sana katika mikataba hii ya kulipa gharama za ardhi inayotumika na wawekezaji katika minara ya simu. Hata hivyo, nalichukua wazo lake au pendekezo lake ili tuangalie namna gani Wizara inaweza kusaidia katika kuhakikisha minara hii ambayo imewekwa katika Jimbo hili la Kalenga inatumika na inawanufaisha wananchi kupitia mikataba yao ambayo wameweka.

Name

Lucia Ursula Michael Mlowe

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. GODFREY W. MGIMWA Aliuliza:- Tatizo la mawasiliano ya simu katika Jimbo la Kalenga bado ni kubwa:- Je, ni lini Serikali itapeleka minara ya simu kwenye vijiji vya Kaning’ombe, Ikungwe, Lyamgungwe, Igunda na Ikuvilo.

Supplementary Question 2

MHE. LUCIA M. MLOWE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niulize swali moja la nyongeza. Kwa kuwa, katika Mkoa wa Njombe kuna matatizo makubwa sana ya mawasiliano hasa maeneo ya mwambao katika Wilaya ya Ludewa kama Rupingu, Ibumi. Je, Serikali ina mpango gani wa kuwapelekea minara watu wa maeneo hayo?

Name

Eng. Edwin Amandus Ngonyani

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Namtumbo

Answer

NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimshukuru sana Mheshimiwa Mbunge kwa namna anavyoshirikiana na Mbunge wa Jimbo la Ludewa katika kuhakikisha kwamba eneo la Mwambao linashughulikiwa kikamilifu. Kwa sababu swali hilo limeulizwa muda siyo mrefu na tumelijibu hapa likiulizwa na Mheshimiwa Deo Ngalawa na leo linaulizwa na Mheshimiwa Lucia Mlowe nawashukuruni sana kwa ushirikiano wenu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kama ambavyo nimekuwa nikilijibu kupitia Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo kwamba eneo hilo tutahakikisha tunajenga minara katika kipindi hiki na itakapofika mwaka 2020 tatizo hilo tutakuwa tumelitatua. Siyo hilo tu na lile lingine la kutoboa barabara katika ukanda ule wa Ziwa, tutakuwa tumeshashughulikia hayo matatizo.

Name

Sixtus Raphael Mapunda

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mbinga Mjini

Primary Question

MHE. GODFREY W. MGIMWA Aliuliza:- Tatizo la mawasiliano ya simu katika Jimbo la Kalenga bado ni kubwa:- Je, ni lini Serikali itapeleka minara ya simu kwenye vijiji vya Kaning’ombe, Ikungwe, Lyamgungwe, Igunda na Ikuvilo.

Supplementary Question 3

MHE. SIXTUS R. MAPUNDA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nami nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa, tatizo linalolikabili Jimbo la Kalenga linafanana vilevile na Kijiji cha Ruvuma chini, Kijiji cha Kihungu, Kijiji cha Mpepai, hao nao wanapata shida kubwa ya mawasiliano. Je, ni lini Serikali itahakikisha vijiji hivi navyo vinawekwa katika mpango na mwaka huu usipite wapate mawasiliano kama wanavyopata Watanzania wengine?

Name

Eng. Edwin Amandus Ngonyani

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Namtumbo

Answer

NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, vijiji hivyo alivyovitaja vya Ruvuma chini, Mpepai na eneo lote lile la ukanda wa Ziwa Nyasa pamoja na Mto Ruvuma, maeneo hayo yameingizwa katika mpango wa UCSAF, tunachohitaji ni kupata fedha ili tuweze kuyatekeleza hayo maeneo na nimhakikishie tutaendelea kufuatilia kama ambavyo Waziri wangu alimuahidi ofisini wakati alipokuwa akifuatilia hili suala.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimhakikishie kwamba tutalifuatilia hadi tunakamilisha mawasiliano katika maeneo hayo ili watu wetu wasiwe wanapata matatizo na mawasiliano ya nchi jirani na wakashindwa kuwasiliana kwa upande wa Tanzania.