Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Nape Moses Nnauye

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mtama

Primary Question

MHE. NAPE M. NNAUYE (K.n.y. MHE. RASHID M. CHUACHUA) Aliuliza:- Mfumo mzima wa ununuzi wa zao la korosho kuanzia kwenye ngazi ya Vyama vya Msingi umegubikwa na dhuluma na ukandamizaji mkubwa wa haki za mkulima kwa kila hatua. Hali hiyo imesababisha malalamiko yasiyokwisha ya wakulima wa korosho kila mwaka. Malalamiko ya wakulima ni uwepo wa makato yanayomuumiza mkulima, kutokuwepo kwa uwazi katika kumpata mshindi wa tender, kujitoa kiholela kwa makampuni yanayosababisha kushuka kwa bei ya korosho, kutolipwa kwa bei halali inayouzwa mnadani kwa Vyama vya Msingi, rushwa katika kila ngazi, pamoja na njama kati ya benki na kampuni zinazonunua korosho. (a) Je, ni lini Serikali itaondoa na kushughulikia malalamiko ya wakulima wa korosho? (b) Je, ni lini Serikali itadhibiti usambazaji wa pembejeo za ruzuku kwa watu ambao sio wakulima wa korosho?

Supplementary Question 1

MHE. NAPE M. NNAUYE: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri na pamoja na kazi nzuri ambayo imeanza kufanywa ya kusaidia kuongezeka kwa bei ya zao la korosho kwa Mikoa ya Lindi, Mtwara na Pwani ambao ni wakulima wazuri wa korosho, naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwanza, je, Serikali haioni sasa umefika wakati wa kuweka kiwango cha elimu kwa viongozi wanaoongoza Vyama vya Msingi, kwa sababu ni moja ya changamoto kubwa sana ambayo imesababisha migogoro mikubwa kwenye Vyama vya Msingi na inasababisha hasara kubwa kwa wakulima wakorosho? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, moja ya changamoto kubwa kwenye biashara ya korosho ni utaratibu wa wanunuzi wa korosho kutengeneza cartel, kutengeneza muungano wa pamoja ambao unakwenda kuathiri bei ya mnada kwenye ununuzi wa korosho. Sasa Serikali inachukua hatua gani kukomesha utaratibu huu? Kwa sababu kwa kweli, kwa namna moja ama nyingine umeathiri sana wakulima wa zao la korosho na bei inaendelea kushuka kila kunapokucha na hata sasa ambapo bei imekwenda vizuri, msimu ujao mpango huu wa cartel ukiachiwa ukaendelea, wakulima wetu wataendelea kupata umaskini na nchi yetu haitasonga mbele.

Name

William Tate Olenasha

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ngorongoro

Answer

NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuungana na Mheshimiwa Nape kwamba zao la korosho ni zao la muhimu sana kwa mikoa inayolima hususan Mikoa ya Lindi na Mtwara. Katika msimu uliopita mikoa sita inayolima korosho, kwa uchache waliweza kuingiza shilingi bilioni 700 katika kipindi kifupi kwa ajili ya kuuza korosho. Yote imetokana na jitihada za Serikali ya Awamu ya Tano ya kuendeleza zao la korosho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunakubaliana na Mheshimiwa Mbunge kwamba, kiwango cha elimu kwa Watumishi wa Vyama vya Ushirika, ni kitu kikubwa. Kimsingi tunategemea kurekebisha sheria ili kuweza kuongeza kiwango hicho, lakini tunasisitiza vilevile kwamba elimu pekee siyo kigezo, tunahitaji watu waadilifu, lakini zaidi watu ambao wanafahamu taratibu za tasnia ya korosho inavyoendeshwa. Kwa hiyo, tutaleta marekebisho, lakini vilevile tutaangalia vitu vingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na namna ya kudhibiti cartel, kwa kutambua kwamba huko nyuma wanunuzi walikuwa wanatumia utaratibu huo wa cartel kuharibu bei ya korosho, kwa sasa tunaendesha minada kwa uwazi zaidi ili isitokee watu wakatengeneza utaratibu na watumishi wa Ushirika, vilevile na wa Vyama vya Ushirika wasio waaminifu ili kujitengenezea utaratibu ambao wanunuzi ni hao hao na hivyo kuweza kuharibu bei.
Kwa hiyo, kwa sasa kuna utaratibu wa kuuza korosho kwa uwazi zaidi, lakini vilevile pale mnunuzi atakaposhinda zabuni ya kununua korosho inatakiwa aweke dhamana ili baadaye asije akaacha kununua ili baei ije ishuke. Kwa hiyo, utaratibu huo unashughulikiwa.