Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Hawa Subira Mwaifunga

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. HAWA S. MWAIFUNGA Aliuliza:- Tumbaku ni moja ya zao la biashara ambalo ni muhimu sana kwa Mkoa wa Tabora, lakini ukaushaji wake umekuwa mgumu sana kwa wakulima kutokana na kulazimika kutafuta kuni kwa ajili ya kukaushia tumbaku jambo ambalo linaathiri afya za wakulima hao pamoja na mazingira. Je, ni lini Serikali itawasaidia wakulima wa tumbaku mkoani Tabora kupata nishati mbadala kwa ajili ya kukaushia tumbaku?

Supplementary Question 1

MHE. HAWA S. MWAIFUNGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Pamoja na majibu ya Naibu Waziri ambayo hayaridhishi vizuri, napenda nimuulize maswali madogo mawili ya nyongeza.
Je, Serikali haioni sasa kuna umuhimu wa kwenda kutoa elimu kwa wakulima hawa ili badala ya kutumia hayo magogo ambayo wanasema, basi waweze kutumia hayo matawi ili kuweza kukausha tumbaku zao?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, Serikali haioni sasa kuna umuhimu wa kuhakikisha wakulima hawa hawatumii tena kuni kwa sababu wanakata sana miti na badala yake walete hiyo nishati mbadala kwa haraka ili wakulima hawa waweze kuacha kukata miti?

Name

William Tate Olenasha

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ngorongoro

Answer

NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu elimu, Serikali imeendelea kutoa elimu kuhusu umuhimu wa kutumia majiko sanifu na vilevile athari za mazingira zinazotokana na ukataji wa miti. Kwa hiyo, ni kitu ambacho kimekuwa kikiendelea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, namsihi tu Mheshimiwa Mbunge pamoja na Wabunge wengine wanaotoka maeneo yanayolima tumbaku, waendelee kuwaelimisha wananchi wetu kuhusu umuhimu wa kutunza mazingira katika kilimo cha tumbaku kwa sababu tumbaku yetu inaweza ikawa na bei nzuri kwenye soko kama tutakuwa na tabia ambazo zinahifadhi mazingira. Inaitwa compliance, ni moja kati ya vigezo vinavyoangalia ubora wa tumbaku.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema, kwa sasa Serikali inahimiza matumizi ya majiko sanifu na kuanzia msimu huu unaokuja, haitaruhusiwa tena kutumia majiko ya aina nyingine; itakuwa ni lazima kila mkulima atumie majiko sanifu wakati wa kukausha tumbaku.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na nishati mbadala, kama nilivyosema, tayari tafiti zimeshafanyika kuangalia kama umeme na makaa ya mawe yanaweza yakawa nishati mbadala, lakini kwa sasa ilionekana kwamba nishati hizo zinakuwa na gharama kubwa kwa mkulima. Kwa hiyo, njia ambayo inaoneka ni ya gharama nafuu lakini vilevile ni rafiki kwa mazingira, ni kutumia majiko sanifu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunamwomba Mheshimiwa Mbunge na Waheshimiwa Wabunge wengine waisaidie Serikali kuendelea kuhimiza wakulima wetu watumie njia hiyo wakati wa kukausha tumbaku.