Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Mohamed Omary Mchengerwa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Rufiji

Primary Question

MHE. MOHAMED O. MCHENGERWA Aliuliza:- Matatizo ya mipaka kati ya wanakijiji na maeneo ya hifadhi husababisha migogoro kati ya wanakijiji na watumishi wa hifadhi. Je, Serikali inachukua hatua gani kurejesha mahusiano kati ya watumishi wa hifadhi na wananchi?

Supplementary Question 1

MHE. MOHAMED O. MCHENGERWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sekunde moja naomba niendelee kutoa pole kwa wananchi wangu wa Rufiji hususan tukio la jana ambapo Mwenyekiti wa Kijiji cha Nyambuju alitaka kuuawa lakini alisalimika baada ya kukimbia kugundua majambazi wale wameshaingia nyumbani kwake,
taarifa ambazo nimezipokea muda huu.
Mheshimiwa Naibu Spika, nina maswali mawili tu ya nyongeza; la kwanza nimuulize Mheshimiwa Naibu Waziri migogoro baina ya wananchi na wahifadhi imechangiwa na kuondolewa kwa mipaka ya awali iliyokuwepo hususan katika Kata ya Mwaseni na wananchi kuzuiliwa kuvua samaki
wale ambao wapo katika vijiji vinavyopakana na hifadhi. Naomba kufahamu Serikali ina mpango gani sasa ili yale mabwawa matano niliyoyaomba kwenye Wizara ya Maliasili na Utalii yaweze kuchimbwa haraka katika Kata ya Mwaseni, Kata ya Kipugira hususan maeneo ya Nyaminywili, Kipo na Kipugila pia katika Kata ya Ngorongo? Naomba kufahamu Serikali inaharakisha vipi
mchakato wa uchimbwaji wa mabwawa ya samaki kwa wananchi wangu wa maeneo hayo?
Mheshimiwa naibu Spika, lakini pili……
Mheshimiwa Naibu Spika, ninafuta hilo swali la samaki, naomba la mgogoro wa mipaka libaki. Swali la pili, watumishi wa hifadhi wamekuwa
wakiweka beacons na alama kadhaa katika baadhi ya nyumba hususani katika maeneo ya Kipugila maeneo ya Nyaminywili na maeneo mengine.
Mheshimiwa Naibu Spika, mchakato wa uwekaji wa beacons unakiuka Ibara ya 13 ya Katiba, pia unakiuka Ibara ya 16 ya Katiba ambayo inazungumzia haki za msingi za wananchi ubinafsi wao, ufamilia wao pamoja na uhifadhi wa maskani zao. Ninaomba kufahamu je, Wizara hii ya Maliasili na Utalii imedhamiria kabisa kukiuka Katiba ya haki za msingi ya Ibara ya 13 na Ibara ya 16, katika kuweka beacons na kusababisha uhuru wa wananchi wa mnaeneo husika kukosa haki zao za msingi?

Name

Eng. Ramo Matala Makani

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tunduru Kaskazini

Answer

NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuanza na swali lake la pili. Uchukuaji wa hatua wa wawekaji mipaka kwenye maeneo yote ya hifadhi unafanyika hivyo kwa mujibu wa sheria. Kama tunavyofahamu zimetungwa na Bunge lako Tukufu jambo ambalo limefanyika pia kwa mujibu wa Katiba.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa ule ni utekelezaji wa sheria ambazo zipo kwa mujibu wa Katiba, napenda kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba hata mara moja Serikali kupitia Wizara ya Maliasili haiwezi kuvunja Katiba. Iwapo kuna jambo lolote mahususi ambalo anadhani kwamba linaweza kufanana na hicho anachokisema basi namkaribisha aweze kuja kuniona tuweze kulijadili na kuweza kulipatia ufumbuzi zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika swali la pili ambalo lilikuwa la kwanza la uwekaji wa mipaka au uwekaji wa alama. Uwekaji wa alama ni hatua inayochukuliwa baada ya kuwa tayari mipaka ilikuwepo miaka mingi iliyopita. Wakati wa utekelezaji wa zoezi la uwekaji wa alama Wizara
inafanya mazoezi haya kwa kushirikisha wananchi katika maeneo yanayohusika.
Mheshimiwa Naibu Spika, naamini katika maeneo
ambayo ameyataja Mheshimiwa Mchengerwa zoezi hili limefanyika kwa utaratibu huo wa kushirikisha wananchi, iwapo kuna hoja mahsusi zinazohusiana na alama hizo basi anaweza kuzileta kwa kutaja vijiji vyenyewe hasa ili tuweze
kuona namna ambavyo tunaweza kwenda kuona namna bora zaidi ya kwenda kuweka alama hizo. Nisisitize kwamba zoezi hili kwamba zoezi hili ni agizo la Serikali kupitia maagizo ya Viongozi Wakuu wa Serikali akiwemo Mheshimiwa Waziri
Mkuu na kwa hiyo litaendelea lakini jambo la msingi tutaendelea kushirikisha wananchi ili liweze kuwa zoezi rafiki.

Name

Joshua Samwel Nassari

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Arumeru-Mashariki

Primary Question

MHE. MOHAMED O. MCHENGERWA Aliuliza:- Matatizo ya mipaka kati ya wanakijiji na maeneo ya hifadhi husababisha migogoro kati ya wanakijiji na watumishi wa hifadhi. Je, Serikali inachukua hatua gani kurejesha mahusiano kati ya watumishi wa hifadhi na wananchi?

Supplementary Question 2

MHE. JOSHUA S. NASSARI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kuniona na mimi niulize swali moja dogo la nyongeza. Migogoro ambayo imeendelea kuwepo baina ya vijiji ambavyo vinazunguka hifadhi haviko kwa Mheshimiwa Mchengerwa peke yake, pale Arumeru kuna Hifadhi ya Taifa ya Arusha (Arusha National Park) na imekuwa na mgogoro wa siku nyingi sana hususani kijiji cha Momela, kitongoji cha Momela na hifadhi. Hifadhi ya Taifa ya Arusha ni miongoni
mwa hifadhi changa ambazo zimekuja kuanzishwa miaka ya juzi juzi tu.
Swali langu kwa Mheshimiwa Waziri Makani ni kwamba ni lini basi atakuwa tayari tuende Arumeru ili tuweze kwenda kuhuisha mgogoro
ambao umekuwepo baina ya Kijiji cha Momela wananchi wa King’ori na wananchi wa Kiburuki na Hifadhi ya Taifa ya Arusha ili tuweze kurudisha mahusiano?

Name

Eng. Ramo Matala Makani

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tunduru Kaskazini

Answer

NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, kama ambavyo amesema ni kweli kwamba masuala yanayohusiana na migogoro ya mipaka baina ya maeneo yaliyohifadhiwa na maeneo wanayoishi wananchi yapo maeneo mengi katika nchi nzima.
Mheshimiwa Naibu Spika, Hifadhi ya Taifa ya Arusha (Arusha National Park) ni mojawapo tu ya maeneo hayo, lakini nilikumbushe Bunge lako Tukufu kwamba hivi tunavyozungumza ile Kamati ambayo tayari ilikwishaundwa inayoshirikishwa Wizara zaidi ya nne bado inaendelea na zoezi lake, watakapokuwa wamekamilisha kazi yao watakuwa wametoa ushauri Serikalini kuhusu namna bora zaidi ya kushughulikia migogoro hii ambayo tumekuwa tukiishughulikia kwa miaka mingi, lakini pengine tulikuwa hatujapata dawa ambayo ni sahihi. Sasa wakati tunasubiri kamati hii ikamilishe kazi yake pengine itakuwa si jambo
muhimu sana kwenda mahali ambapo pengine Kamati hii itakuwa imekwenda.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo nafikiri itakuwa ni bora zaidi mimi na Mheshimiwa Nassari baada ya kuwa nimewauliza Kamati wamefikia wapi kama ni suala la kwenda kuona mimi na yeye tunaweza kwenda kama itasema kwamba bado haijakamilisha zoezi hili kwenye eneo analolizungumzia.