Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Khalifa Mohammed Issa

Sex

Male

Party

ACT

Constituent

Mtambwe

Primary Question

MHE. KHALIFA MOHAMED ISSA aliuliza:- Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) upo katika Awamu ya Tatu ya utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini ili ziweze kumudu mahitaji ya chakula, elimu, afya na lishe bora kwa watoto:- (a) Je, Serikali haioni ipo haja ya kuongeza viwango vya ulipaji kwa kaya maskini hasa ukizingatia upandaji wa bei za mahitaji ya kila siku na kuporomoka kwa thamani ya sarafu yetu? (b) Je, ni vigezo gani vya uhakika vinatumika ili kupata kaya maskini?

Supplementary Question 1

MHE. KHALIFA MOHAMED ISSA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, kwanza mimi na-declare my interest kwamba ni Mjumbe wa Kamati yako ya Kudumu ya Utawala na TAMISEMI. Kwa hivyo,
katika ziara zetu mbalimbali tumepata ushuhuda wa wanufaika wa kaya maskini na kiwango fulani wamenufaika kweli. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini pamoja na kunufaika kwao bado haijaondoa umuhimu wa kuweza kuongezewa hii ruzuku kwa sababu kama nilivyosema katika swali langu la msingi kila siku maisha yanapanda, shilingi yetu inaporomoka
na bei ya bidhaa inaongezeka. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri anaonaje basi wakaweza kupewa viwango hivi wanavyopewa kwa mkupuo walau wa miezi sita ili ile tija ya kuweza kuendesha biashara zao, kujenga makazi yao ikapatikana?
Mheshimiwa Spika, lakini swali la pili dogo, mimi
nashukuru katika Jimbo langu pia mradi huu katika baadhi ya shehia unaendelea lakini kuna usumbufu wale walengwa kutoka katika vijiji vingi wanakusanyika katika center moja.
Waziri anaonaje akaongeza vituo vya kulipia ili wale watu ambao wamekusudiwa kupewa ruzuku hii wasipate matatizo hasa ukizingatia wengine ni wanyonge sana, wengine ni watu wazima mno…
Mheshimiwa Spika, ahsante.

Name

George Boniface Simbachawene

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kibakwe

Answer

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS (MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA): Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi.

Mheshimiwa Spika, nimeeleza katika majibu ya swali langu la msingi. Kwanza kabisa, ukiangalia mradi huu, kabla hatujaanza uhawilishaji mwaka 2013 tulianza mpango wa majaribio mwaka 2008 kwa miaka mitano katika Halmashauri tatu za Chamwino, Bagamoyo pamoja na Kibaha. Katika mpango huo wa majaribio, kaya 26,000 zilishiriki katika mpango huu.
Mheshimiwa Spika, ukiangalia mwanzoni wakati
programu inaanza, wakati huo wa majaribio, kiwango cha juu kabisa kilikuwa ni Sh.17,500/=. Hata hivyo, tulipoanza mpango tulipandisha mpaka Sh.34,000/= na ilikuwa haiangalii watoto walioko katika kaya, haingalii watoto wanaopata huduma za kiafya na zinginezo. Nipende tu kumwambia Mheshimiwa Mbunge kwamba tumeongeza, kwa sasa hivi kiwango cha juu kabisa ni Sh.76,000/= vilevile wanapata fursa pia ya kupata ujira, kwa siku 60 kila mwaka wanapata takribani Sh.138,000 kwa Sh.2,300 kwa siku.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, napenda kusema
kwamba katika majaribio ilionekana ukiwapa kiwango kikubwa sana inawezekana wakabweteka na wasiweze kufanya shughuli zingine za ujasiriamali na wakajitegemea tu kupitia ruzuku hii. Kwa hiyo, ilionekana kwa kweli kiwango hiki kinafaa na tumefanya majaribio na wako wengi ambao wameweza kunufaika na kupata maendeleo katika maishayao.

Mheshimiwa Spika, katika swali lingine kwamba
wapewe sasa kwa mkupuo wa miezi sita, hoja yake Mheshimiwa tunaiona, napenda tu kusema kwamba tunaendelea kuifanyia kazi ili kuona kama inawezekana miezi sita au miezi mitatu na nini kinaweza kikafanyika. Kwa sasa nisiseme kama tumekubali, lakini niseme tunaona hoja ni ya msingi tuichukue twende tukaifanyie kazi.
Mheshimiwa Spika, kuhusiana na hoja ya kuongeza vituo vya kulipia fedha na yenyewe pia niseme tunaichukua ili kuona ni kwa namna gani tunaweza tukawarahisishia na kuwasogezea huduma karibu zaidi walengwa wetu.

Name

George Malima Lubeleje

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mpwapwa

Primary Question

MHE. KHALIFA MOHAMED ISSA aliuliza:- Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) upo katika Awamu ya Tatu ya utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini ili ziweze kumudu mahitaji ya chakula, elimu, afya na lishe bora kwa watoto:- (a) Je, Serikali haioni ipo haja ya kuongeza viwango vya ulipaji kwa kaya maskini hasa ukizingatia upandaji wa bei za mahitaji ya kila siku na kuporomoka kwa thamani ya sarafu yetu? (b) Je, ni vigezo gani vya uhakika vinatumika ili kupata kaya maskini?

Supplementary Question 2

MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili na mimi niulize swali moja la nyongeza. Kwa kuwa kila Halmashauri ya Wilaya ina Mratibu wa TASAF na waratibu ndiyo wameandikisha kaya
maskini, walijua kabisa kwamba kaya hii ni maskini. Hivi
karibuni kuna kaya ambazo zimeondolewa kwamba hazina sifa na wanaambiwa warejeshe fedha, wengine ni wazee kabisa. Mheshimiwa Waziri nani mwenye makosa, ni mratibu aliyeorodhesha au ni yule ambaye ameambiwa kwamba alipe hizo fedha?

Name

George Boniface Simbachawene

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kibakwe

Answer

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS (MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA): Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa nimpongeze kwa namna ambavyo amekuwa akifuatilia utekelezaji mzima wa mpango huu, lakini zaidi namna ambavyo amekuwa akifuatilia kaya zile ambazo zimeondolewa. Mpaka sasa tumeshaondoa kaya 63,819 katika maeneo 162 ya utekelezaji.
Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa, napenda tu
kusema kwamba, wale ambao wamelengwa kuondolewa katika uhakiki huu ni zile kaya ambazo hazikustahili kuingizwa katika mpango. Tumekuwa tukishuhudia pia katika zoezi hili, kama mnavyotambua wakati wa utambuzi na uandikishaji, chombo kikuu kinachoshiriki ni mkutano wetu mkuu wa kijiji au katika shehia lakini unakuta wengine waliwaingiza wenye uwezo matokeo yake baadaye wanajikuta wanakuja kuondolewa tunakuja tunasikia maneno kama hayo.
Mheshimiwa Spika, nipende tu kusema kwamba,
kama kweli kaya ilikuwa ni maskini, ikawa imejiboreshea maisha haikutakiwa kuondolewa bila kufuata vigezo vya msingi. Tumeanza kufanya zoezi hili, tumeshawaandikia Wakurugenzi wote tangu mwezi Februari waweze kupitia
kwa kina. Napenda tu kusema kwamba waratibu wengi pia walishiriki, hawakuwa makini katika ufuatiliaji na katika tathmini zao na ndiyo maana tayari tumeshawachukulia hatua waratibu zaidi ya 91 na tutaendelea kufanya hivyo kila ikibidi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, vilevile napenda tu kusema
kwamba, wale ambao tunawalenga ni wafanyabiashara, unakuta kuna mtu alikuwa ana bucha na mambo mengine ameingizwa, haiwezekani! Vilevile unakuta wengine ni watumishi wa umma wameingizwa katika mpango hawastahili kuanzia siku ya kwanza, hao ndio ambao tunawalenga. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, napenda tu
kuwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge kwa namna ambavyo wamekuwa wakifuatilia suala hili. Tutaendelea kuwafuatilia na tutaendelea kuchukua hatua. Kwa wale ambao ni maskini kweli kwanza wanatakiwa warudi kwenye mpango na si kumfuatilia aweze kurudisha fedha.

Name

Rev. Peter Simon Msigwa

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Iringa Mjini

Primary Question

MHE. KHALIFA MOHAMED ISSA aliuliza:- Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) upo katika Awamu ya Tatu ya utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini ili ziweze kumudu mahitaji ya chakula, elimu, afya na lishe bora kwa watoto:- (a) Je, Serikali haioni ipo haja ya kuongeza viwango vya ulipaji kwa kaya maskini hasa ukizingatia upandaji wa bei za mahitaji ya kila siku na kuporomoka kwa thamani ya sarafu yetu? (b) Je, ni vigezo gani vya uhakika vinatumika ili kupata kaya maskini?

Supplementary Question 3

MHE. MCH. PETER S. MSIGWA: Mheshimiwa Spika, nikushukuru sana kwa kunipa nafasi. Pamoja na majibu ya Mheshimiwa Waziri, toka mpango huu umeanza baadhi yetu
tuli-challenge sana kwamba haukuanza kubadilisha fikra za watu kabla ya kuwapa hela. Nataka nimuulize Waziri ni kwa kiwango gani anaweza akaliambia Bunge hili huu mpango
wa kugawa hizi fedha umeleta impact katika jamii, kwa sababu bado hali ya umaskini imeendelea kuwa kubwa katika Taifa letu.

Name

George Boniface Simbachawene

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kibakwe

Answer

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS (MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA): Mheshimiwa Spika, naamini, bahati nzuri wiki iliyopita tu tulikuwa na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa, tulikuwa
Iringa Mjini, tumetembelea walengwa wale na kaya zake. Sasa kama leo anasema kaya zile kweli hazijanufaika na hazijaondoka kwenye umaskini, kwa kweli inabidi hata wapiga kura wamwangalie kwa macho mawili, mawili.
(Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa ukiangalia
tumefanya tathmini kuangalia ni kwa namna gani fedha hizi zimeweza kuchochea mabadiliko. Vilevile ukiangalia katika TASAF Awamu ya I na II, kulikuwa hakuna ruzuku ya uhawilishaji lakini ilikuja kuonekana katika Watanzania asilimia 28.3 wenye pengo la umaskini walikuwa hawawezi
kumudu gharama za kupeleka familia zao katika matibabu, wengine watoto wao walikuwa wamedumaa, wengine walikuwa hawapati lishe ya kutosha, wengine walikuwa hata
shuleni mahudhurio hawahudhurii vizuri. Ukiangalia sasa hata Iringa peke yake zaidi ya asilimia 70 mpaka 90 mahudhurio yameimarika, wengine sasa zaidi ya asilimia 10 mpaka 15 wanaanza kukaribia kuondoka katika pengo la umaskini. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nipende tu kusema
wengi wameboresha mavazi, wengi ameboresha makazi yao, wengi sasa ukiangalia hata kwa zile kaya zilizokuwa zinajiweza ambazo zilikuwa haziwezi kuwavalisha watoto wao shuleni, wanaangalia kama mtoto maskini anaweza kuvaa nadhifu basi na yeye kidogo anajiongeza. Kwa hiyo, kwa kweli ni Mfuko ambao umekuwa na manufaa sana na nimwombe Mheshimiwa Msigwa aendelee kufuatilia kaya zake na aendelee kuziunga mkono. (Makofi)

Name

Kabwe Zuberi Ruyagwa Zitto

Sex

Male

Party

ACT

Constituent

Kigoma Mjini

Primary Question

MHE. KHALIFA MOHAMED ISSA aliuliza:- Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) upo katika Awamu ya Tatu ya utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini ili ziweze kumudu mahitaji ya chakula, elimu, afya na lishe bora kwa watoto:- (a) Je, Serikali haioni ipo haja ya kuongeza viwango vya ulipaji kwa kaya maskini hasa ukizingatia upandaji wa bei za mahitaji ya kila siku na kuporomoka kwa thamani ya sarafu yetu? (b) Je, ni vigezo gani vya uhakika vinatumika ili kupata kaya maskini?

Supplementary Question 4

MHE. KABWE Z. R. ZITTO: Mheshimiwa Spika,
changamoto kubwa ya umaskini Tanzania ni kwamba idadi kubwa ya watu ama wako chini kidogo ya mstari wa umaskini au juu kidogo ya mstari wa umaskini. Kwa hiyo, hata wakipata fedha hizi za TASAF wakipata shock yoyote ya
kimaisha wanarudi chini kwenye mstari wa umaskini na wanakuwa maskini, kwa hiyo, juhudi zote hizi zinakuwa hazijaleta manufaa anayotakiwa. Serikali haioni kwamba umefikia wakati muafaka katika fedha hizi za TASAF kuwe na component ya social protection ili kuhakikisha kwamba baadhi ya watu hawa wanaingizwa kwenye hifadhi ya jamii, wanaweka akiba, wanaweza kupata mikopo midogo midogo ya kuendesha biashara zao, wanaweza wakapata bima ya afya, ili watakapopata shock wasirudi tena kwenye mstari wa umaskini? Haoni kuna haja ya kufanya hivyo sasa hivi kwenye TASAF inayoendelea?

Name

George Boniface Simbachawene

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kibakwe

Answer

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS (MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA): Mheshimiwa Spika, kwanza nimshukuru maana ni hoja ambayo amekuwa akiifuatilia mara kwa mara. Tulipofanya semina katika Bunge hili ambayo iliendeshwa na TASAF pia aliweza kuhoji swali kama hili.
Mheshimiwa Spika, napenda tu kusema kwamba,
lengo la conditional cash transfers kokote duniani ni kuhakikisha kwamba mwisho wa siku ni kuwa na social protection moja ambayo inaunganisha kuanzia mwanzo mpaka mwisho. Sisi kama TASAF tumeanza na sasa watoto wenye miaka sifuri mpaka tano, mpaka sasa hivi watu wazima
walau kuna hizo component tatu kwenye miradi ya ujira, tunatoa pia ajira za muda, tunatoa miradi ya miundombinu, tuna targeted infrastructure pamoja na mingine. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, napenda kusema,tunaiona hoja yake lakini kwa sasa ngoja tumalizie awamu ya kwanza ya awamu ya tatu. Tutakapokuja kusanifu sasa awamu ya pili itakayoanza mwaka 2019/2020 tutaweza kuona ni kwa namna gani swala hili linaweza kuzingatiwa.

Name

Salma Rashid Kikwete

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Mchinga

Primary Question

MHE. KHALIFA MOHAMED ISSA aliuliza:- Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) upo katika Awamu ya Tatu ya utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini ili ziweze kumudu mahitaji ya chakula, elimu, afya na lishe bora kwa watoto:- (a) Je, Serikali haioni ipo haja ya kuongeza viwango vya ulipaji kwa kaya maskini hasa ukizingatia upandaji wa bei za mahitaji ya kila siku na kuporomoka kwa thamani ya sarafu yetu? (b) Je, ni vigezo gani vya uhakika vinatumika ili kupata kaya maskini?

Supplementary Question 5

MHE. SALMA R. KIKWETE: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi hii ya kuuliza swali la nyongeza, lakini kabla ya kuuliza swali la nyongeza, naomba nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu na nimshukuru Mheshimiwa Rais wangu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuniteua kuwa Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali langu la nyongeza ni kuhusu huduma ya TASAF. Serikali ina mpango gani mahsusi wa kuongeza huduma hii hasa kwa watu wetu maskini kutoka katika Mkoa wetu wa Lindi?

Name

George Boniface Simbachawene

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kibakwe

Answer

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS (MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA): Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa nimpongeze kwa namna ambavyo amekuwa akifuatilia maendeleo ya jamii, lakini zaidi kwa siku ya kwanza tu ameweza kuuliza swali hili. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ukiangalia katika Mkoa wa Lindi nikitolea tu mfano kwa sasa tuko Lindi DC, Lindi Manispaa, Nachingwea, Ruangwa pamoja na maeneo mengine. Niseme tu kwamba tumepokea hoja hii, nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba kwa sasa tumefikia asilimia
70 tumebakiza asilimia 30 yenye vijiji 5,690 na tumepanga katika mwaka huu wa fedha unaokuja wa 2017/2018 tutaweza kutambua na kuandikisha kaya zilizobakia 355,000
na naamini Lindi pia itakuwa ni mojawapo.