Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Khatib Said Haji

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Konde

Primary Question

MHE. KHATIB SAID HAJI aliuliza:- Kumekuwa na ongezeko kubwa la mahabusu katika magereza hapa nchini kutokana na kuchelewa kwa upelelezi wa mashauri mengi. (a) Je, Serikali inachukua hatua gani za haraka ili kukabiliana na ucheleweshaji huo wa kesi zilizopo mahakamani? (b) Je, ni muda gani umewekwa kisheria pale upande wa mashtaka unaposhindwa kupeleka ushahidi mahakamani ili mahakama iweze kumuachia huru mshitakiwa?

Supplementary Question 1

MHE. KHATIBU SAID HAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, tunamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuijaalia nchi yetu kuwa miongoni mwa nchi ambayo haiko katika matishio ya kigaidi. Lakini cha kusikitisha sana katika mahabusu walioko magerezani miongoni mwao ni washitakiwa wa makosa ya kigaidi. Hivi nchi isiyo na tishio la kigaidi inawezaje kuwa na mrundikano wa mahabusu wanaotokana na makosa ya kigaidi? La kwanza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, Waziri wa Vikosi vya SMZ-Zanzibar na Makamu wa Rais wa Zanzibar wamewahi kunukuliwa wakisema kwamba wamewaleta Masheikh wa Uamsho kutoka Zanzibar ili wanyee kwenye ndoo katika magereza Tanzania Bara. Hapa katika jibu imeambiwa siku 60 inatosha kutoa ushahidi na kama ushahidi haukupatikana watuhumiwa waachiwe huru. Masheikh wa Uamsho wana miaka minne sasa wako katika magereza na ushahidi umeshindwa kupatikana. (Makofi)
Nataka kujua, familia za watuhumiwa wale wanataka kujua, dunia inataka kujua, Wazanzibari wanataka kujua watuhumiwa wale wanawekwa kwa amri ya viongozi wa SMZ au wanawekwa kwa sababu wana kesi ya kujibu? Ahsante.

Name

Eng. Hamad Yussuf Masauni

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kikwajuni

Answer

NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ambavyo nimejibu katika jibu langu la msingi kwenye jibu (b). Muda wa kisheria wa kuondoa shauri mahakamani kama upelelezi haujakamilika ni siku 60. Maswali yake mawili yote hayapingani na majibu yangu ya msingi kama ambavyo walitaka kueleweshwa Wabunge pamoja na wananchi ambao wanatusikiliza hapa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo kimsingi ni kwamba kesi za hawa watuhumiwa zote ziko mahakamani na kwa mujibu wa sheria zetu hatupaswi kuzungumza mashauri ambayo yapo mahakamani.


WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tu kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba swali alilouliza ni swali mtambuka ambalo liko chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi na vilevile Wizara ya Mambo ya Katiba na Sheria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba kusisitiza yafuatayo na siyo lazima upende jibu lake lakini ndiyo ukweli wenyewe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba nisahihishe kauli hatarishi sana kwa kwamba Tanzania haina tishio la ugaidi. Tumeshakabiliwa na matatizo ya kigaidi, umeshalipuliwa ubalozi wa nchi kubwa sana hapa nchini na baadhi ya Watanzania wamehusika, lakini leo hii tukiona kuna usalama nchi hii tuelewe kwamba vyombo vyetu vya ulinzi na usalama vinafanya kazi ndiyo maana huoni hayo matukio mara kwa mara. Naomba nichukue fursa hii kuvipongeza vikosi vyetu vya ulinzi na usalama kwa kazi nzuri ambayo vinafanya kuzima wimbi la ugaidi nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pengine ningemuomba Mheshimiwa Haji ajijibu mwenyewe lakini naomba mimi nijibu kama Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, suala la mtuhumiwa yeyote aliyeko mahakamni ni muda gani kesi yake ataruhusiwa kuendelea kukaa mahakamani kama upelelezi haujaisha? Naibu Waziri ameeleza ni siku 60. Lakini pale ambapo upelelezi haujakamilika Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa analeta maombi mahakamani na inaweza kuongezwa hizo siku lakini siyo hivyo tu, baada ya hapo suala linakuwa chini ya Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (DPP) ambaye kulingana na uzito wa suala lenyewe anaweza akaomba mahakama kuongeza muda na muda utaongezwa. Suala la ugaidi siyo suala dogo, ni suala ambalo upelelezi wake rahisi kwa sababu ni suala la kimtandao. Kutambua huo mtandao wa ugaidi siyo kitu rahisi tu. Usalama wa nchi hiiā€¦(Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata Mheshimiwa Mbunge leo aliyeuliza swali amekuja salama hapa kwa sababu kuna vyombo vya ulinzi vinamsimamia usalama wake.

Name

Pauline Philipo Gekul

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Babati Mjini

Primary Question

MHE. KHATIB SAID HAJI aliuliza:- Kumekuwa na ongezeko kubwa la mahabusu katika magereza hapa nchini kutokana na kuchelewa kwa upelelezi wa mashauri mengi. (a) Je, Serikali inachukua hatua gani za haraka ili kukabiliana na ucheleweshaji huo wa kesi zilizopo mahakamani? (b) Je, ni muda gani umewekwa kisheria pale upande wa mashtaka unaposhindwa kupeleka ushahidi mahakamani ili mahakama iweze kumuachia huru mshitakiwa?

Supplementary Question 2

MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kunipa nafasi niulize swali moja la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti tarehe 12 Januari, 2017 nilifika kwenye Gereza la Babati nikakuta watuhumiwa wa kesi ya mauaji na dawa za kulevya wamekaa zaidi ya miaka minne na sheria haijaweka time frame, hizo siku 60 ni kwa makosa ya kawaida. Mheshimiwa Waziri tuambie ni lini mtafanya marekebsho ya sheria ili hata kwa makosa haya ya mauaji na dawa za kulevya watu wasikae magerezani au mahabusu kwa muda mrefu kama ilivyo sasa?

Name

Dr. Harrison George Mwakyembe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kyela

Answer

WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba kuna baadhi ya makosa na hata makosa mengine yanawafanya Watanzania wengi walioko magerezani kukaa huko kwa muda mrefu. Lakini swali hili lilikuwa linauliza tunachukua hatua zipi? Naomba kumuelezea Mheshimiwa Mbunge hatua ambazo Serikali imezichukua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, sasa hivi tunaangalia njia za kuboresha mifumo yetu ya adhabu mbadala ambayo mnafikiri wote Waheshimiwa Wabunge mnajua mmepitisha sheria nyie wenyewe hapa ya Parole, kuna suala la community service na vilevile kuna kitu kinaitwa extra mural penal employment, lakini vilevile ipo haja na hili ni suala pia linawahusu Waheshimiwa Wabunge tukiwaletea bajeti hapa kuongeza vikao vya Mahakama Kuu ambayo Mahakama Kuu ndiyo pekee inakaa kufanya sessions kwa ajili ya murder cases na wafungwa wengi kwa kweli, mahabusu wengi tunawakuta magerezani wa murder cases kwa kweli vikao vya mahakama ni vichache, inabidi tuongeze hiyo frequency.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini vilevile tatu, kuna tatizo sasa siyo tu kwa wale wanao-face murder cases hata kwa watuhumiwa wengine kwamba kuna tatizo la ucheleweshaji wa hukumu za mahakama na mwenendo wa mashitaka ambao unawafanya watuhumiwa waweze kwenda mahakamani au wafungwa au mahabusu kwenda mahakamani kudai haki zao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nitoe wito sasa hivi kwa mahakama ku-adhere, kuheshimu au kufuata, kutekeleza waraka namba moja wa mwaka jana wa Jaji Mkuu unaotaka mashauri yote na mwenendo wake unapokwisha ichukue siku 21 tu kila kitu kiweze kupatikana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tu nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba suala la mrundikano wa kesi mahakamani na watu kukaa ndani tumelifanyia kazi kubwa mno na tukiangalia record ya nchi hii miaka mitatu iliyopita tulikuwa na mrundikano wa kesi zaidi ya asilimia 60 za zamani, lakini leo mrundikano wa kesi umebakia ni asilimia 5.8 hivi na ambao ni kesi hizo za jinai kama alizoziongelea Mheshimiwa Gekul.