Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Joseph Michael Mkundi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ukerewe

Primary Question

MHE. JOSEPH M. MKUNDI aliuliza:- Ni zaidi ya miaka mitano sasa tangu Meli ya MV Butiama isitishe huduma zake katika Ziwa Victoria kati ya Mwanza na Nansio (Ukerewe) hali inayosababisha shida na usumbufu mkubwa wa usafiri kwa wakazi wa Ukerewe. (a) Je, ni lini meli hiyo ya MV Butiama itatengenezwa na kuendelea kutoa huduma kati ya Mwanza na Nansio? (b) Je, Serikali ina mpango gani wa kuleta meli mpya hasa ikizingatiwa kuwa meli ya MV Clarius imechakaa sana?

Supplementary Question 1

MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kunipa nafasi niulize maswali mawili ya nyongeza.
Baada ya MV Butiama kusita kufanya shughuli zake pale kulikuwa na meli ya MV Clarius ambayo nayo imesimama kufanya kazi na kuna taarifa kwamba itatengenezwa na watu wa MSCL ili iendelee kufanya shughuli zake lakini meli hii imekuwa chakavu, inahitaji matengenezo makubwa. Sasa kwa kuwa wenye jukumu la kutengeneza ni MSCL wenyewe lakini wanatatizo kubwa sana la fedha. Je, Serikali sasa haioni kwamba kuna haja ya kuwasaidia hawa MSCL kwa kuwapa fedha za kutosha ikiwepo pamoja na pesa za OC ili waweze sasa kutengeneza meli hii iweze kufanya kazi katika mazingira mazuri ikizingatiwa ni ya muda mrefu na katika hali halisi ya sasa kumsafirisha abiria kwa saa tatu majini akiwa amekalia viti vya mbao si kitu kizuri sana?
Swali la pili; ratiba za meli kutoka Mwanza kwenda Ukerewe zina mahusiano ya moja kwa moja na ratiba za vivuko vingine. Kwa mfano, Kivuko cha MV Nyerere kutoka Mgolola kwenda Ukala sasa kumekuwa na matatizo ya kutowiana kwa ratiba kiasi kwamba wasafiri wanakaa muda mrefu. Kwa mfano, akifika Nansio anakaa kwa saa tano ili apate usafiri mwingine wa kumpeleka kisiwa cha Ukala. Je, Serikali haioni sababu za msingi za kuainisha ratiba ya vivuko hivi ili kuondoa gharama kubwa ambazo wasafiri wanazipata wanapokuwa safarini? Nashukuru.

Name

Eng. Edwin Amandus Ngonyani

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Namtumbo

Answer

NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa swali lake la kwanza, nakubaliana naye kwamba kuna haja ya kuwaongezea uwezo wa kifedha ikiwa ni pamoja na fedha za OC ili MSCL waweze kutekeleza wajibu wao na hasa katika kuikarabati meli hii ya MV Clarius.
Kwa upande wa pili, ratiba nimepokea ombi lake, nitawasiliana na taasisi hizi mbili zinazohusika, TEMESA pamoja na MSCL waangalie kama kuna uwezekano wa kurekebisha ratiba zao, lakini kwa mazingira ninayoyafahamu, tukirekebisha kutakuwa na tatizo vilevile la kuwasumbua wale wa Ukala wakakaa muda mrefu sana kusubiri MV Clarius ifike, ilete abiria. Tutaangalia kama kutakuwa na uwezekano wa kutafuta njia nyingine kuweza hili kuliweka sawa ili wananchi waweze kunufaika na huduma hizo mbili za kivuko pamoja na Meli.