Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Juma Selemani Nkamia

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Chemba

Primary Question

MHE. JUMA S. NKAMIA aliuliza:- Je, Serikali ina mpango gani wa kununua mashine mpya za CT-Scan kwa ajili ya Hospitali ya Taifa ya Muhimbili?

Supplementary Question 1

MHE. JUMA S. NKAMIA: Mheshimwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza kwa rafiki yangu Mheshimiwa Dkt. Hamisi Kigwangalla, Naibu Waziri wa Afya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Naibu Waziri wakati anajibu swali anasema, Serikali ilifanya maamuzi lakini swali langu lilikuwa Serikali ina mpango gani wa kununua mashine kwa ajili ya Hospitali ya Taifa ya Muhimbili? Mashine anayoizungumzia Mheshimiwa Dkt. Kigwangalla ni mashine ambayo imechukuliwa kutoka Hospitali ya Benjamin Mkapa ya Dodoma, katika Chuo Kikuu cha Dodoma, ikahamishiwa Muhimbili. Swali la kwanza, je, anaweza kukiri kwamba ni kweli hiyo mashine anayoizungumzia ni ile iliyochukuliwa kutoka Hospitali ya Benjamin Mkapa katika Chuo Kikuu cha Dodoma kupelekwa Muhimbili? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, Dodoma pia kuna wagonjwa. Unapohamisha mashine ya CT-Scan kutoka Dodoma kupeleka Muhimbili na unakuja hapa unasema ziko mbili sasa, unataka watu wa Dodoma wafe? (Makofi)

Name

Dr. Hamisi Andrea Kigwangalla

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nzega Vijijini

Answer

NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSI, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwanza, nitumie nafasi hii kumshukuru na kumpongeza Rais wa Awamu ya Nne, Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete kwa kuonyesha mapenzi ya dhati na kuwajali watu wa Dodoma na Kanda ya Kati kwa ujumla wake kwa kujenga hospitali kubwa ya kisasa inayoitwa Benjamin Mkapa Ultra-Modern Hospital hapa Dodoma. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa muktadha huo pia nitumie nafasi hii kwa namna ya kipekee kumpongeza Rais wa Awamu ya Tano, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, kwa ziara ya kushtukiza aliyoifanya kwenye Hospitali yetu ya Taifa Muhimbili ambayo ilibaini upungufu mwingi wa vipimo na namna ya kuchunguza magonjwa kwenye hospitali hii kubwa ya Taifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa najibu swali ya Mheshimiwa Nkamia kama ifuatavyo. Kwanza, nakiri kwamba mashine ambayo imefungwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili ni mashine ambayo ilikuwa ifungwe kwenye Hospitali ya Benjemin Mkapa. Kwa sababu mbalimbali za kitaalamu ndani ya Serikali, majengo ambapo ilikuwa ifungwe mashine hii kwenye Hospitali ya Benjamin Mkapa iliyopo Dodoma yalikuwa bado hayajakamilika wakati huo hospitali kubwa kabisa ya Taifa pale Muhimbili kulikuwa kuna mahitaji ya mashine kwani mashine iliyokuwepo ilikuwa imeharibika. Mheshimiwa Rais alifika pale Muhimbili akajitolea fedha na matengenezo yakaanza lakini huduma ikawa haiwezekeni kutolewa kwa kuwa mashine haikupona kwa wakati. Kwa hivyo, ndani ya Serikali tuliona ingekuwa ni vyema kwa kuwa tuna uwezo wa kununua mashine nyingine mpya na tulikuwa tayari kununua mashine mpya kwa ajili ya kufunga Muhimbili tu-switch ile ambayo imeshafika nchini ambayo ilikuwa ifungwe hapa Dodoma ifungwe sasa Muhimbili. Sasa hivi tupo kwenye mchakato wa kununua mashine mpya kwa ajili ya kuja kufunga Benjamin Mkapa na majengo ya kufunga mashine hiyo kwa sasa yanaelekea kukamilika. (Makofi)

Name

Susan Anselm Jerome Lyimo

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. JUMA S. NKAMIA aliuliza:- Je, Serikali ina mpango gani wa kununua mashine mpya za CT-Scan kwa ajili ya Hospitali ya Taifa ya Muhimbili?

Supplementary Question 2

MHE. SUSAN A. J. LYIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipatia nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tarehe 20 Oktoba, 2015 aliyekuwa Rais wa Awamu ya Nne alipokea magari ya washawasha 399 kati ya magari 777. Kati ya magari hayo ni magari 50 tu yalitumika. Nime-google bei ya gari moja ni sawa kabisa na kipimo cha MRI na Scanner kwa maana ya kwamba gari moja ni kama dola 400 na hiyo mashine bei yake ni hiyohiyo.
MWENYEKITI: Dola 400?
MHE. SUSAN A.J. LYIMO: Dola 400,000. Je, ni kwa nini sasa Serikali haioni kwamba huo ni upotevu mkubwa wa fedha na kutokuwajali wananchi na kwamba fedha hizo zingetosha kununua Scanner na MRI kwa nchi nzima kwenye Hospitali zote za Rufaa? (Makofi)

Name

Eng. Hamad Yussuf Masauni

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kikwajuni

Answer

NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI (K.n.y. NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSI, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, si kweli kwamba magari ya washawasha yamenunuliwa na hayana tija. Magari ya washawasha yamenunuliwa ikiwa ni miongoni mwa ile programu ya kununua magari 777 kwa ajili ya matumizi ya Askari. Kwa hiyo, magari haya yamesaidia sana na bado mengine yatafika kwa ajili ya shughuli mbalimbali za kipolisi. (Makofi)

Name

Rashid Abdallah Shangazi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mlalo

Primary Question

MHE. JUMA S. NKAMIA aliuliza:- Je, Serikali ina mpango gani wa kununua mashine mpya za CT-Scan kwa ajili ya Hospitali ya Taifa ya Muhimbili?

Supplementary Question 3

MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kuniona. Naomba niulize swali kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Mlalo kama ifuatavyo:-
Je, ni lini Serikali itatuletea huduma za X-ray katika Kituo cha Afya cha Mlalo ambacho kinahudumia zaidi ya wakazi elfu sitini wa Jimbo la Mlalo?

Name

Dr. Hamisi Andrea Kigwangalla

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nzega Vijijini

Answer

NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii na namshukuru Mheshimiwa Rashidi Shangazi, Mbunge wa Jimbo la Mlalo, kwa swali lake la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, majibu ni kwamba, Serikali yetu ya Tanzania imeingia mkataba na Serikali ya Uholanzi ku-embark kwenye mradi mkubwa unaojulikana kama mradi wa sekta ya afya wa ORIO ambapo Serikali yetu itakuwa tayari kuchangia nusu ya Euro 22,000,000 kwa ajili ya kununua vifaa vya kufanyia uchunguzi wa magonjwa na kusambazwa kwenye hospitali zote nchi nzima. Tulikuwa tumelazimika kuchangia takribani Euro milioni 2.2 na mpaka tunavyoongea tulikuwa tumepungukiwa na kama Euro 818,000.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini wiki iliyopita, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dokta John Pombe Magufuli amemwelekeza Waziri wa Fedha kwamba fedha zilizokuwa zitumike kwa ajili ya semina elekezi kwa Mawaziri zielekezwe kwenda kukamilisha deni hilo la Euro 818,000 kwa ajili ya kukamilisha mchango wetu kwenye mradi huu mkubwa wa kununua vifaa. Hivyo, naamini kwamba hospitali mbalimbali nchini ikiwemo Hospitali ya Mlalo zinaweza zikapata vifaa hivyo pindi tutakapoanza utekelezaji wa mradi huu.