Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Halima James Mdee

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. HALIMA J. MDEE aliuliza:- Jimbo la Kawe ni miongoni mwa Majimbo ambayo (baadhi ya maeneo) yamekuwa yanakabiliwa na changamoto za upatikanaji wa maji safi na salama kwa kipindi kirefu ambayo ni Kata ya Mabwepande (Mtaa wa Mbopo, Mabwepande na Kinondo), Kata ya Makongo (Mtaa wa Changanyikeni na baadhi ya maeneo ya Mtaa wa Makongo Juu), Kata ya Wazo, Mbweni na Mbezi Juu; na changamoto hii sugu ilitarajiwa kupungua na kumalizika kabisa baada ya mradi mkubwa wa maji wa Ruvu chini kukamilika ambao kwa sasa tayari umeshakamilika:- (a) Je, mikakati ya usambazaji maji pamoja na Mabomba (katika maeneo ambayo hayana mtandao wa mabomba) ikoje ili kutatua kero husika? (b) Je, ni miradi gani inayotarajiwa kutekelezwa, muda wa utekelezaji, gharama za kila mradi na nani anayewajibika katika utekelezaji?

Supplementary Question 1

MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye (b) ya swali langu niliuliza, ni miradi gani inayotarajia kutekelezwa, muda wa utekelezaji, gharama za kila mradi na nani anayewajibika katika utekelezaji? Sasa majibu ya Serikali hayajanielezea mradi, ila ameelezea maeneo ambayo mradi utatekelezwa. Sasa nataka niambiwe katika maeneo haya ambayo miradi itatekelezwa, kuna miradi gani specifically, kuna Kampuni gani specifically? Hilo la kwanza.
La pili, zimetajwa dola bilioni 32, nami nilivyouliza swali, nilikuwa nataka nijue gharama za kila mradi kwenye Jimbo langu. Sasa swali langu la pili: Je, hizi bilioni 32 ndiyo zote zinaenda kwenye mradi wa Jimbo la Kawe na kama siyo, nataka nijue Jimbo la Kawe specifically katika hii dola bilioni 32 mgao wake ni kiasi gani na kwa miradi ipi? Nadhani nimeeleweka.
Swali langu nataka uchambuzi ili wananchi wangu wanaosikia kila mmoja ajue kwake anastahiki gani. Sasa Serikali ikinipa kiujumla jumla nitashindwa kuja kuwabana.
Kwa hiyo, nataka uchambue, siyo unajibu kiujumla jumla.

Name

Eng. Gerson Hosea Lwenge

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wanging'ombe

Answer

WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa katika jibu la msingi, tumeshasema mradi ambao unaendelea, Mkandarasi anaitwa Jain Irrigation Company na tumesema gharama ya mradi ni US Dollar milioni 32. Tunapokuwa tunapanga miradi, huwa hatupangi Kijimbo. Tunapanga mradi kwa ajili ya Jiji la Dar es Salaam na sehemu kubwa ya mradi huu uko kwenye Jimbo lake.
Ndiyo maana tumetaja hayo maeneo ya Kawe, Mabwepande, yote yote yako kwenye Jimbo la Kawe. Kwa hiyo, tumelijibu kikamilifu kama alivyouliza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika sehemu yake ya pili alikuwa anataka kujua kama hizo US Dollar milioni 32 ni kwa Jimbo la Kawe tu peke yake? Hapana, siyo kwa Jimbo la Kawe peke yake, ni pamoja na bomba kubwa ambalo litaenda baadhi ya maeneo ya Wilaya ya Bagamoyo.