Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Hassan Elias Masala

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nachingwea

Primary Question

MHE. HASSAN E. MASSALA aliuliza:- Wilaya ya Nachingwea ina ardhi ya kutosha lakini vijana wengi bado wanakabiliwa na tatizo la ajira:- Je, Serikali inatoa kauli gani kuwasaidia vijana hawa kujikwamua kiuchumi?

Supplementary Question 1

MHE. HASSAN E. MASALA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana, lakini pia naomba nitoe pongezi kwa majibu haya ya Mheshimiwa Naibu Waziri. Sambamba na haya, naomba niulize maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, kwa sababu Nachingwea tayari tumeshatenga maeneo na kupitia fedha ya Halmashauri peke yake kwa hizi 5% haiwezi kutosha kuwafikia vijana wengi, sijajua Serikali inatuambia nini ili tuweze kuona namna gani tunaweza kunufaika na fedha zinazotolewa na Mifuko ya Vijana kupitia Taifa badala ya kuachia Halmashauri peke yake?
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini swali la pili, naomba nipate majibu juu ya jitihada gani ambazo zinafanywa kwa vijana wa Mikoa ya Lindi na Mtwara ukizingatia ziko baadhi ya Kanda tayari wameshaanza kuwasogezea huduma za kuwafungulia milango ya kupata ajira ikiwemo Kanda ya Ziwa, vijana wengi wanatakiwa waende kule kwa ajili ya kujiunga na vikundi vya kushona viatu. Lindi na Mtwara tunavyo Vyuo vya VETA, nini kauli ya Serikali juu ya vijana wa kanda hii na hasa vijana wanaotoka Nachingwea ambao hawana chuo cha namna hii? Ahsante.

Name

Anthony Peter Mavunde

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Dodoma mjini

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la kwanza amesema kwamba, tayari wameshatenga maeneo kwa ajili ya shughuli za vijana na nichukue fursa hii kwanza kabisa kuipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Nachingwea kwa sababu mwaka 2014 Wakuu wa Mikoa wote walikutana hapa Dodoma na likawekwa Azimio la kuhakikisha kila Halmashauri nchi nzima inatenga maeneo maalum kwa ajili ya shughuli za vijana ambayo tuliyapa jina la Youth Special Economic Zones. Mpaka sasa hivi ninavyozungumza tayari zimeshatengwa ekari 86,000 nchi nzima na Halmashauri ya Wilaya ya Nachingwea nayo ni mojawapo. Kwa hiyo, niwapongeze kwa hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini swali lake la msingi ni kwamba fedha ya Halmashauri haitoshi, ni kweli! Nataka nikiri kwamba fedha ile haiwezi kukidhi mahitaji. Hata hivyo, tunao Mfuko wa Maendeleo ya Vijana ambao umetoa mwongozo wa kukopesha SACCOS za vijana katika kila Halmashauri. Nimwombe Mheshimiwa Mbunge awaandae vijana wake, tushirikiane kwa pamoja, wabuni miradi, walete maombi kupitia mfuko ule tumekuwa tukitoa fedha kusaidia vikundi mbalimbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi ninavyozungumza tumeshakopesha takriban Sh.1,700,000,000 kwa vikundi mbalimbali nchini Tanzania. Ushahidi wa dhahiri kabisa ni katika Mkoa wa Simiyu chini ya uongozi wa Mkuu wa Mkoa wa Mheshimiwa Anthony Mtaka, tumekabidhi fedha kwa vikundi viwili vya kutengeneza chaki na maziwa katika Wilaya ya Maswa na Meatu, takriban Sh. 30,000,000 kwa kila kikundi. Kwa hiyo, nimwombe Mheshimiwa Mbunge afanye jitihada hizo, sisi tutakuwa tayari kumuunga mkono. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili anasema ni jitihada gani Serikali imezionesha katika Mikoa ya Lindi na Mtwara. Mheshimiwa Mbunge ni kweli, kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu tuna programu nyingi sana za vijana na sasa hivi tumetangaza programu ya vijana kwenda kupata mafunzo ya kutengeneza viatu na bidhaa za ngozi kule Mwanza lakini siyo kweli kwamba mikoa hii tumeisahau. Mwaka jana tumekuwa na programu kubwa sana katika Mikoa mitano ikiwemo Lindi na Mtwara ambapo tuliwafikia vijana takriban 9,100 kupitia programu inayoitwa Youth Economic Empowerment na mpaka ninavyozungumza hivi sasa vijana wengi wa Lindi na Mtwara walipata mafunzo kupitia VETA na sasa hivi wamejiajiri na wameajiri na vijana wengine. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tutaendelea kupanua wigo wa programu zetu ili ziweze kufika nchi nzima na vijana wote waweze kunufaika.

Name

Joseph Roman Selasini

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Rombo

Primary Question

MHE. HASSAN E. MASSALA aliuliza:- Wilaya ya Nachingwea ina ardhi ya kutosha lakini vijana wengi bado wanakabiliwa na tatizo la ajira:- Je, Serikali inatoa kauli gani kuwasaidia vijana hawa kujikwamua kiuchumi?

Supplementary Question 2

MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Wilaya ya Rombo ni moja kati ya Wilaya ambazo zina tatizo kubwa sana la uhaba wa ardhi hapa nchini. Mwaka 1974 Mwalimu Nyerere aliwachukua baadhi ya vijana kuwatafutia ardhi maeneno ya Mpanda kule Mikese na Tanga kule Kilindi. Vijana wa Rombo wana nguvu na wana tamaa ya kujiajiri katika kilimo. Mheshimiwa Waziri yuko tayari nikimletea vikundi vya vijana wa Rombo ambao wako tayari kujiajiri katika kilimo kuwatafutia ardhi maeneo mengine ya nchi ili na wenyewe waweze kushiriki katika kujitafutia ajira kupitia kilimo?

Name

Anthony Peter Mavunde

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Dodoma mjini

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, katika programu chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu, moja kati ya mkakati mkubwa ambao tumeuweka ni kuwapeleka vijana katika kilimo cha umwagiliaji na kilimo biashara na katika utekelezaji wa programu hii hatuchagui maeneo. Nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba niko tayari kushirikiana naye kwa wale vijana wa Rombo ambao wako tayari kufanya shughuli za kilimo tukawasaidia wakapata maeneo na sisi kama Serikali tukawa sehemu ya kuwawezesha ili haja yao itimie. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tunao mpango wa kitaifa wa kilimo kati ya Wizara ya Kilimo na sisi Ofisi ya Waziri Mkuu ambao lengo lake kubwa ni kwenda kuyatumia mashamba makubwa ya Serikali yale ambayo hayatumiki, yamekuwa mapori, kwa kuyatengenezea miundombinu ili vijana wengi sana waende kufanya shughuli za kilimo katika maeneo hayo. Kwa sasa tutaanzia eneo la Mkulazi Morogoro ambapo patajengwa Kiwanda cha Sukari kwa ushirika kati ya NSSF na PPF, maeneo yameshatengwa na hivi karibuni tutakwenda kuyasafisha yale maeneo na baadaye vijana watapewa maeneo hayo yakiwa yameshaboreshwa na miundombinu yake imekamilika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimwondoe hofu Mheshimiwa Mbunge, vijana wa Rombo wakiwa tayari anione tu niko tayari kumsaidia.

Name

George Malima Lubeleje

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mpwapwa

Primary Question

MHE. HASSAN E. MASSALA aliuliza:- Wilaya ya Nachingwea ina ardhi ya kutosha lakini vijana wengi bado wanakabiliwa na tatizo la ajira:- Je, Serikali inatoa kauli gani kuwasaidia vijana hawa kujikwamua kiuchumi?

Supplementary Question 3

MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili na mimi niulize swali moja la nyongeza. Kabla ya kuuliza swali, naomba niwape pole wananchi wa Kitongoji cha Chinyika na Kwamshango kwa maafa waliyopata ambapo watu watano wamefariki kwa kusombwa na maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa niulize swali. Kwa kuwa Mheshimiwa Naibu Waziri aliwahi kuwa Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa na anajua vijana wengi sana katika Wilaya ya Mpwapwa hawana ajira na hizo fedha zinazotolewa ni kidogo sana. Je, Naibu Waziri yuko tayari kuongeza fungu la fedha hizo ili vijana wengi waweze kupata ajira pamoja na wa Wilaya ya Mpwapwa?

Name

Anthony Peter Mavunde

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Dodoma mjini

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli tuna changamoto ya Mifuko hii ya Uwezeshaji ya Mitaji na Mikopo kwa vijana hasa kwa kushindwa kukidhi mahitaji ya vikundi vingi ambavyo vimekuwa vikiomba mikopo hii. Tunachokifanya kama Serikali ni nini? Sisi kazi yetu kubwa tunayoifanya kwanza kabisa ni kuwatambua vijana nchi nzima kutokana na mahitaji yao na kazi, pili ni kuwarasimisha na tatu ni kuwajengea uwezo wa kifedha kupitia mifuko mbalimbali ya Serikali lakini na kushirikiana na wadau mbalimbali. Nimwahidi tu Mheshimiwa Mbunge kwamba tunaendelea na jitihada za kuwa-invite wadau wengi zaidi wa maendeleo ya vijana ili watusaidie katika eneo hili la uwezeshaji na kuongeza mfuko wetu ili tuweze kuwafikia vijana wengi zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini la mwisho, Bunge hili ndilo ambalo tunapanga bajeti, muone pia haja ya kutuongezea fedha kwa ajili ya Mfuko wa Mendeleo ya Vijana ili tuwafikie vijana wengi zaidi nchi nzima.

Name

Venance Methusalah Mwamoto

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kilolo

Primary Question

MHE. HASSAN E. MASSALA aliuliza:- Wilaya ya Nachingwea ina ardhi ya kutosha lakini vijana wengi bado wanakabiliwa na tatizo la ajira:- Je, Serikali inatoa kauli gani kuwasaidia vijana hawa kujikwamua kiuchumi?

Supplementary Question 4

MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi hii. Kwa kuwa fedha hizi ambazo zimekuwa zikipelekwa katika Halmashauri ni kidogo sana kiasi kwamba hata hazitoi msaada mkubwa kwa wale vijana. Mheshimiwa Naibu Waziri, kuna ubaya gani kama vijana hawa ambao walio wengi hawana ajira hasa wale wanaotoka kwenye vyuo vikuu na sehemu nyingine wakaanzishiwa Benki ya Vijana ambayo itakuwa rahisi kui-control na kuwapata wale wahitaji ambao kwa kweli wanataka kutumia hizo fedha vizuri hasa sehemu kama za Kilolo na hasa hapa kwake Dodoma, je, atakuwa tayari?

Name

Anthony Peter Mavunde

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Dodoma mjini

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, mpango wa Serikali ni kuelekea katika uanzishwaji wa Benki ya Mendeleo ya Vijana lakini kabla hatujafikia hatua hiyo tukasema ni vyema kwanza tuwaanzishie vijana SACCOS mbalimbali ili tuanze kuwakopesha kupitia SACCOS hizo, wajifunze nidhamu ya fedha na matumizi yake na baadaye tutaenda kufikia katika uanzishwaji wa Benki ya Maendeleo ya Vijana wakati tayari tumeshaandaa kundi letu kubwa hili la vijana kwenda kushiriki katika masuala ya fedha. Vinginevyo, usipoanza na utaratibu huu wa kuwazoesha mwisho wa siku fedha ile ya mikopo inaweza kutumika katika mambo tofauti na ikawa haijamsaidia kijana huyu. Kwa hiyo, tumeanza katika SACCOS baadaye tutakwenda mpaka kwenye uanzishwaji wa Benki ya Maendeleo ya Vijana.