Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Daniel Edward Mtuka

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Manyoni Mashariki

Primary Question

MHE. DANIEL E. MTUKA aliuliza:- Watanzania wengi wanahitaji umeme mjini na vijijini lakini wanashindwa kuvuta umeme kutokana na gharama kubwa ambapo service line ni shilingi 177,000 na zaidi na gharama ya nguzo ni shilingi 337,740 na zaidi:- (a) Kwa kuwa nguzo ni mali ya TANESCO, je, kwa nini nguzo hizi zisilipiwe na Serikali? (b) Je, Serikali haioni kuwa sasa ni wakati muafaka wa kupunguza service line costs kuwa shilingi 27,000 kama ilivyo kwa mradi wa REA?

Supplementary Question 1

MHE. DANIEL E. MTUKA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, ninayo maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza ni ombi, baadhi ya vitongoji ndani ya Mji wangu wa Manyoni havijapata umeme mpaka sasa hivi ninavyozungumza, ukitembea usiku utakuta pale umeme unawaka, pale umeme hauwaki, karibu nusu ya Mji wa Manyoni upo gizani na tatizo kubwa ni gharama za nguzo kuwa kubwa.
Mheshimiwa Spika, niiombe Serikali kwa bajeti ya kuanzia mwaka huu imtengee fedha Meneja wa TANESCO wa Wilaya ya Manyoni angalau aweze kununua nguzo na sisi tutaweza kuchangia gharama nyingine ndogo ndogo, hilo la kwanza.
Mheshimiwa Spika, swali la pili, mkandarasi anayetekeleza Mradi wa REA II katika Tarafa ya Nkonko yenye vijiji 25 hajakamilisha mradi huu mpaka sasa hivi ambapo ilitakiwa aukamilishe Septemba, 2015. Pamoja na juhudi za Mbunge, Naibu na Waziri kufuatilia zimegonga mwamba, mkandarasi huyu anaonekana ni mzembe na mvivu. Wananchi wa Manyoni wamenituma, wanasema hawataki kumuona hata kwa sura yule mkandarasi, Kampuni ya Spencon.
Je, ni lini Serikali itatuletea mkandarasi mwingine kwa sababu yule hatumtaki tena, hatufai kabisa? Ahsante.

Name

Dr. Medard Matogolo Kalemani

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Chato

Answer

NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Spika, kwanza nichukue nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Mtuka kwa jinsi anavyofuatilia maslahi ya wananchi kwa upande wa umeme. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge wa Manyoni Mashariki kwamba ni kweli kabisa vile vijiji ambavyo havijafikiwa na umeme, kulikuwa na shida ya nguzo kwa mkandarasi lakini nimhakikishie kwamba tumeanza kutekeleza Mradi wa REA III kuanzia tarehe 6 Januari, 2017. Nitumie nafasi hii kuwaarifu Waheshimiwa Wabunge wote pamoja na wananchi kwamba utekelezaji wa REA III umeanza tangu tarehe 6 Januari, 2017 na utaendelea kutekelezwa ndani ya miaka mitano ijayo.
Mheshimiwa Spika, tumeanza kutekeleza Mradi wa REA katika mikoa sita ikiwemo Mikoa ya Pwani, Tanga, Mara, Iringa, Arusha pamoja na Mbeya. Kadhalika tumeanza kutekeleza mradi huo katika mikoa mingine ambayo ilikuwa kwenye mikoa mama hapo awali ikiwemo Mkoa ya Songwe pamoja na Njombe.
Mheshimiwa Spika, sasa ili nijielekeze kwa swali la Mheshimiwa Mtuka, nimhakikishie vile vijiji 75 ambavyo havijapata umeme kikiwemo Kijiji chake cha Simbangulu, Makutupora, Mwembela na London vitapata umeme. Kwa hiyo, namhakikishie Mheshimiwa Mtuka kwamba vijiji vyake 75 vilivyobaki vitapata umeme bila mashaka. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali lake la pili kuhusiana na mkandarasi Spencon, nichukue nafasi hii kusema rasmi kwamba yule mkandarasi amesimama kazi tangu mwezi Novemba. Ni kweli kati ya wakandarasi tuliokuwa nao hakufanya kazi kwa ufanisi na kama Serikali tumeshachukua hatua. Hatua ya kwanza tuliyochukua tumeshikilia mshahara wake wa mwezi Novemba. Hatua ya pili, tumepeleka shtaka rasmi kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali ili tumshtaki mahakamani na hatua ya tatu hatumpi kazi tena kwenye kandarasi zinazofuata. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hatua nyingine tuliyochukua ni kuanza majadiliano na kumpeleka mkandarasi Octopus katika Mkoa wa Singida ili ianze kutekeleza mradi huu mara moja. Kwa hiyo, wananchi wa Singida watapata umeme haraka iwezekanavyo.