Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Amb Dr. Diodorus Buberwa Kamala

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nkenge

Primary Question

MHE. BALOZI DKT. DIODORUS B. KAMALA aliuliza:- Tulipoanza kutekeleza Umoja wa Forodha wa Afrika Mashariki, kuna bidhaa kutoka Kenya ziliwekwa kwenye kundi „B‟ ambazo zilikuwa zinatozwa kodi iliyokuwa ikipungua taratibu hadi ilifikia kiwango cha asilimia sifuri mwaka 2010. (a) Je, bidhaa hizo ziliongezeka kwa kiasi gani kuingia Tanzania kuanzia mwaka 2005 – 2015? (b) Je, viwanda vya Tanzania vinavyozalisha bidhaa za kundi „B‟ vilikabiliwa na changamoto zipi kutokana na kuondolewa kwa kodi iliyokuwa ikipungua taratibu hadi kufikia asilimia sifuri mwaka 2010?

Supplementary Question 1

MHE. BALOZI DKT. DIODORUS B. KAMALA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Nashukuru kwa majibu lakini ninayo maswali madogo mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, kwa kuwa kipindi cha mpito kilimalizika mwaka 2010 na kwa kuwa tathmini ya uhakika ilitakiwa ifanyike ili kuweza kujua changamoto zilizotokana na kutekeleza utaratibu wa kodi kupungua taratibu, je, ni lini Tanzania ilifanya tathmini ya uhakika kujua changamoto hizo?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa Kanda ya Ziwa, Mwanza, Tanga na Arusha kuna viwanda vingi ambavyo vimelazimika kufungwa kwa sababu ya ushindani wa bidhaa kutoka Kenya; viwanda kama vya mafuta ya kula, maziwa, sabuni na vinginevyo, siwezi kutaja vyote. Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha inasaidia viwanda hivyo kufufuliwa kwa sababu kufa kwake kumetokana na utekelezaji wa sera ambazo hazikufanyiwa tathmini na kuzirekebisha ili viwanda vyetu visiweze kufungwa?

Name

Dr. Susan Alphonce Kolimba

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI: Mheshimiwa Spika, swali la kwanza ambalo anataka kujua kwamba ni lini tathmini hiyo ilifanywa baada ya kipindi kile cha mpito cha kuanzia 2005 mpaka 2009, niseme tu maelezo niliyotoa yanatokana na tathmini ambayo ilitolewa katika tathmini ya mwaka 2015. Ndiyo maana unakuta katika maelezo yangu nimesema mbinu mbalimbali zimefanyika ili kuweza kuboresha viwanda vyetu na kuhamasisha wafanyabiashara wafanye kazi yao vizuri, kwa hiyo tathmini ilifanyika.
Mheshimiwa Spika, vilevile amezungumzia suala la kuhusu viwanda ambavyo baada ya kuruhusu Ushuru wa Forodha kufutwa katika bidhaa hizo zilizokuwa katika kundi „B‟, biashara nyingi au viwanda vingi vya Mikoa kama ya Kanda ya Ziwa ikiwemo Tanga, Mwanza, Rukwa na hata Arusha viliathirika na najua kabisa na yeye pia anajua kwa sababu katika thesis yake aliyoiandikia Ph.D ilikuwa juu ya hiyo.
Mheshimiwa Spika, niseme tu kwamba Serikali inaendelea kufanya mikakati mbalimbali ya kuhakikisha kwamba inaboresha mazingira ya ufanyaji wa kazi katika viwanda na kuwajengea capacity. Kuna mikutano, semina na hata kuangalia vigezo mbalimbali ili kuhakikisha kwamba viwanda vyetu vinafufuka.
Mheshimiwa Spika, mara zote hapa Waziri wa Viwanda na Biashara amekuwa akitoa mikakati mbalimbali ambayo Wizara yake inafanya ili kuhakikisha wafanyabiashara hao wenye viwanda waweze kufufua viwanda vyao. Moja ya mikakati ni kuweza kutambua viwanda gani ambavyo vimekufa na nani anavyo au kuna viwanda gani ambavyo vimeathirika na tatizo hilo la mambo ya ushuru ili viweze kuwezeshwa na kuanza kufunguliwa upya.
Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Wabunge ni mashahidi kwamba katika kipindi hicho cha 2009 mpaka 2010, viwanda vinavyozalisha bidhaa kama za saruji vilikuwa vimekufa, lakini kwa sasa hivi tunaona kwamba sehemu kubwa ya viwanda vinavyofanya vizuri ni pamoja viwanda ambavyo vinazalisha bidhaa za saruji pamoja na mafuta ya kupikia. Ahsante.