Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Dr. Mary Michael Nagu

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Hanang'

Primary Question

MHE. DKT. MARY M. NAGU aliuliza:- Wilaya ya Hanang ni moja ya Wilaya ambazo ziko katika Bonde la Ufa na hivyo upatikanaji wa maji ni wa shida sana. Suluhisho la kudumu ni kuchimba visima virefu na kujenga mabwawa. (a) Je, ni lini Serikali itajenga bwawa la maji katika Kijiji cha Gidahababiegh ambalo lilibomoka kutokana na mvua? (b) Je, ni lini Serikali itarudia kuchimba visima katika Vijiji vya Hirbadamu, Dajameda, Mwanga, Gidika, Lalaji na Wandela ambavyo awali vilipata ufadhili kupitia Mradi wa Benki ya Dunia lakini maji hayakupatikana?

Supplementary Question 1

MHE. DKT. MARY M. NAGU: Mheshimiwa Spika, namshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa kujibu swali langu.
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, Bwawa la Gidahababieg siyo la umwagiliaji tu, maeneo yote yale hayana maji ya uhakika kwa hivyo litakuwa ni kwa ajili ya matumizi ya binadamu, mifugo pamoja na umwagiliaji ikiwezekana. Baada ya bwawa lile kuvunjika kutokana na athari za mvua mwaka 2006, nilifikisha suala hilo kwenye Serikali mwaka 2007 na mpaka leo hakuna lililofanyika. Nataka kujua kama ni kweli mchakato utaanza na bwawa hili lirudi kwa sababu ndiyo linakusanya maji ya mlima Hanang yanayomwagika na kupotea bure?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, Vijiji vya Hirbadaw, Dajameda, Mwanga, Gidika, Lalaji na Wandela vyote vilikuwa kwenye Mradi wa Benki ya Dunia na maji hayakuweza kupatikana. Naomba nijue ni lini vijiji hivyo vitaanza kutafutiwa vyanzo vingine ili watu wale waweze kupata maji kwani Bonde la Ufa halina maji? Nashukuru sana.

Name

Eng. Isack Aloyce Kamwelwe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Katavi

Answer

NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa niseme kwa bahati nzuri nimetembelea Wilaya ya Hanang na wakati nikiwa kule tulishirikiana na Mheshimiwa Mbunge tukazunguka maeneo yote ambayo yanahitaji huduma ya maji.
Mheshimiwa Spika, katika swali lake la kwanza ameonesha kwamba Bwawa la Gidahababiegh sio kwa ajili ya umwagiliaji tu na kweli nilikwenda kwenye lile bwawa likishakamilika litatumika kwa umwagiliaji, mifugo na maji yale yakichakatwa yatatumika pia kwa matumizi ya majumbani. Sasa anauliza ni kweli bwawa hili litatengenezwa? Nimuahidi tu Mheshimiwa Mbunge kwamba tayari tumetenga fedha katika robo ya pili ya mwaka wa fedha huu tulionao. Fedha tunazo tayari na wakati wowote wataalam watatumwa kwenda kule kwa ajili ya kufanya survey. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pili kwenye hivi vijiji ambavyo havikupata vyanzo vya maji, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tulitembea naye na kweli wakati tupo kwenye ziara tuliwaahidi wananchi kwamba haya maeneo ambayo hayakupata vyanzo vya maji kwenye bajeti ya mwaka 2017/2018 ambayo sasa hivi inaandaliwa tutahakikisha tunaweka fedha ili twende kukakamilisha miradi hiyo.