Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Juliana Daniel Shonza

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. JULIANA D. SHONZA Aliuliza:- Je, Serikali ina mpango gani wa kuboresha miundombinu ya elimu vijijini kama nyumba za walimu pamoja na kulipa malimbikizo ya madeni ya walimu wanayoidai Serikali?

Supplementary Question 1

MHE. JULIANA D. SHONZA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu ya Waziri, lakini ni wazi kwamba kwa miaka mingi sana Serikali haijatoa kipaumbele kwa suala la nyumba za walimu. Kwa mfano, kwenye majibu ya Mheshimiwa Waziri amesema kwamba kwa mwaka wa fedha 2016/2017 Serikali imepanga kujenga nyumba 1,818, ukiangalia nikitumia Mbozi kama case study ya Mkoa wa Songwe, kuna uhaba wa nyumba za walimu 1,432. Je, ni lini sasa Serikali italeta mpango kabambe wa kumaliza tatizo la nyumba za walimu hasa wa vijijini ili iwe kama motisha?
Swali la pili, Mheshimiwa Waziri ambacho nilitaka kufahamu kwamba je, ni lini madeni hayo ya walimu yataanza kulipwa kwa sababu ukisema kwamba yamepelekwa tu Hazina bado haileti tija kwa walimu wa Tanzania. Ninataka kujua kwamba ni lini rasmi madeni hayo yataanza kulipwa?
Mheshimiwa Spika, ninakushukuru.

Name

Dr. Selemani Said Jafo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kisarawe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (TAMISEMI): Mheshimiwa Spika, najua Mbunge anaguswa sana na sekta ya elimu na nikupongeze sana kwa sababu ukiwa kijana lazima uguswe na elimu.
Mheshimiwa Spika, katika majibu yangu ya msingi na mkakati wa Serikali nimezungumza pale awali. Kwa vile tumebaini changamoto ya nyumba za walimu ndiyo maana Serikali katika bajeti ya mwaka huu tunaoenda nao imetenga takribani shilingi bilioni 13, hii ni kwa ajili ya nyumba za walimu wa shule za msingi peke yake, lakini shilingi bilioni 11 kwa ajili ya shule za sekondari. Hata hivyo, commitment katika mpango mwingine wa MMES II, nimezungumza hapa karibuni nyumba zipatazo140 tumeshazikamilisha.
Mheshimiwa Spika, naomba niwaambie Waheshimiwa Wabunge katika ziara zangu katika Mikoa mbalimbali, miongoni mwa mambo ninayoyatilia kipaumbele sana ni kukagua ujenzi wa nyumba za walimu. Naomba niwapongeze Wabunge wote kwa ujumla wetu katika maeneo yetu nilipopita nimekuta ujenzi wa nyumba za walimu kwa kweli unaenda kwa kasi sana. Kwa vile katika commitment ya Serikali imeshatenga hizi fedha, naomba niwaambie fedha tunaendelea kuzipeleka katika Halmashauri zetu, lengo kubwa walimu waweze kupata mazingira salama ya kuweza kuishi.
Mheshimiwa Spika, katika suala zima la madai ya walimu, nimesema kwamba sasa hivi tumeshahakiki deni la shilingi bilioni 26.04 na haya ni madeni yasiyo ya mshahara. Maana yake Serikali haiwezi kulipa madeni lazima kwanza kuweza kuhakiki, ndiyo maana nimesema zoezi la uhakiki limeisha Oktoba, 2016. Sasa hivi ni mchakato ambao upo katika Wizara ya Fedha kwa utaratibu wa mwisho wa kuweza kulipa. Kwa hiyo, naomba tuwe na subira tu kwa sababu kigezo kikubwa ni kwamba ni lazima deni lihakikiwe na madeni haya yameshahakikiwa na naomba niwaambie walimu wa Tanzania kwamba wawe na subira kipindi siyo kirefu, Hazina kwa kadri inavyojipanga, madeni haya yanaweza kulipwa walimu mbalimbali ili mradi wapate haki zao.

Name

Dr. Mary Michael Nagu

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Hanang'

Primary Question

MHE. JULIANA D. SHONZA Aliuliza:- Je, Serikali ina mpango gani wa kuboresha miundombinu ya elimu vijijini kama nyumba za walimu pamoja na kulipa malimbikizo ya madeni ya walimu wanayoidai Serikali?

Supplementary Question 2

MHE. DKT. MARY M. NAGU: Mheshimiwa Spika, ahsante sana.
Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa Serikali ningependa ijue kwamba kuna wananchi waliojitolea kwa kujua umuhimu wa walimu kujenga maboma kwa ajili ya nyumba za walimu, pamoja na madarasa.
Je, Serikali itatoa kipaumbele kwa wale wananchi ambao wameonesha umuhimu wa walimu na umuhimu wa elimu?

Name

Dr. Selemani Said Jafo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kisarawe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, jibu ni ndiyo Serikali itatoa. Ndiyo maana hivi sasa tumeshaleta fedha karibu awamu mbili za Capital Development Grand, ambapo katika baadhi ya Halmashauri imeshaanza kuweka kipaumbele kumalizia nyumba za walimu. Maeneo niliyofika zile fedha zilizofika, utakuja kuona yale maboma ambayo mwanzo yalibakia sasa hivi utakuta yanakamilishwa. Kwa hiyo, hiyo ndiyo commitment ya Serikali, naomba nikupongeze na hili ni jukumu la kwetu sote Wabunge zile fedha zinavyopita ni lazima tuzisimamie vizuri, tuende tukamalize haya maboma yaliyopo katika maeneo yetu.

Name

Esther Nicholus Matiko

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. JULIANA D. SHONZA Aliuliza:- Je, Serikali ina mpango gani wa kuboresha miundombinu ya elimu vijijini kama nyumba za walimu pamoja na kulipa malimbikizo ya madeni ya walimu wanayoidai Serikali?

Supplementary Question 3

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Spika, nashukuru, naitwa Mheshimiwa Esther Nicholas Matiko.
Mheshimiwa Spika, ni dhahiri kabisa kwamba ukosefu wa nyumba za walimu na kukaa mbali na shule unasababisha kutokuwa na kiwango kizuri cha ufundishaji kwenye shule zetu. Hivi karibuni tulisikia kauli ya Waziri Mkuu akitoa msisitizo kwamba walimu waishi kwenye shule ambazo wanafundisha. Kwa majibu ya Naibu Waziri ni dhahiri bado Serikali haijawa na mpango madhubuti wa kuhakikisha walimu wanakaa kwenye maeneo ambayo wanafundisha.
Ni nini mpango mkakati wa Serikali hasa kwa pale ambapo wananchi wamejenga maboma wanashindwa kuyamalizia ili watoto wetu waweze kupata elimu mbadala kwa Walimu kukaa maeneo ya shule. Napenda kupata mkakati ambao unatekelezeka siyo wa kuandikwa tu kwenye makaratasi, ahsante.

Name

George Boniface Simbachawene

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kibakwe

Answer

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali ya nyongeza na kuongezea kwenye swali la msingi pia ambalo limejibiwa na Naibu Waziri vizuri kabisa, Mheshimiwa Jafo, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli tuna mahitaji makubwa ya madarasa, tuna mahitaji makubwa ya nyumba za walimu. Kwa mfano, tuna upungufu wa madarasa katika shule ya msingi kwa sasa 127,745. Tuna upungufu wa madarasa kwa shule za sekondari 10,204. Hali kadhalika tuna upungufu wa nyumba za walimu. Mipango yote, mpango uwe mpango mkakati, uwe mpango wa haraka, uwe mpango wa dharura, inafanyika kwenye Halmashauri zetu. Tusitegemee kwamba tutakuja na mpango fulani nje ya mipango ile ya Halmashauri, kwa sababu Serikali kwa mujibu wa Katiba, kwa mujibu wa sheria, tunatekeleza dhana ya ugatuaji wa madaraka.
Mheshimiwa Spika, kugatua madaraka maana yake ni kwamba tupange vipaumbele sisi tulioko huko kwa wananchi. Kwa hiyo, nichukue nafasi hii kwanza kuwapongeza sana wananchi wote wa Tanzania wakiwemo Waheshimiwa Wabunge, kwa namna tulivyoshirikiana vizuri sana katika suala la kupunguza upungufu wa madawati. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, vivyo hivyo sasa, tuangalie namna ya kwenda kwenye mchakato wa kupunguza tatizo la nyumba za walimu na madarasa. Tukifikiri kuna njia nyingine nadhani tutakuwa tunajidanganya, ukweli ni kwamba lazima tujipange wenyewe kwa kutumia rasilimali zilizopo na ndiyo maana katika bajeti ya mwaka huu tunayoiandaa, msisitizo mkubwa ambao tumeelekeza Halmashauri sisi TAMISEMI ni kwamba wajipange sana kuweka fedha nyingi na mipango mikubwa kwenye madarasa na nyumba za walimu. Hii itatusaidia ili hata Serikali kama ikitoa fedha yoyote ile, itakwenda kwa njia hiyo ili kutekeleza upungufu uliopo.