Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Devotha Methew Minja

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. DEVOTHA M. MINJA aliuliza:- Je, Serikali haioni kuwa kuna haja ya kupunguza gharama za upimaji viwanja ambazo ni kubwa sana ili kumwezesha kila Mtanzania kupata huduma hiyo na kuondoa migogoro ya ardhi?

Supplementary Question 1

MHE. DEVOTHA M. MINJA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nimesikiliza majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri ambapo amesema hivi sasa Serikali ime-stick kupima kwenye Sh. 300,000/= kwa hekta moja lakini pia amesema Serikali inashirikiana na wapima binafsi. Je, Serikali imeweka mikakati gani ya kuzuia hao wapima binafsi wasiendelee kuongeza bei kwa maana ya kuwaumiza wananchi ambao wanahitaji huduma hii ya kupimiwa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili, Serikali inasema nini juu ya wananchi wa Mtaa wa CCT Mkundi katika Manispaa ya Morogoro ambao walifuata taratibu zote za kupata hati, lakini hivi sasa wamevunjiwa nyumba zao na wengine wanalala nje huku wakiwa na hati zao mikononi. Je, Serikali ina mpango wowote wa kulipa fidia kwa wananchi hao ambao wana hati?

Name

Dr. Angeline Sylvester Lubala Mabula

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Ilemela

Answer

NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la kwanza ameuliza habari ya Serikali imeweka mikakati gani kuweza kudhibiti hawa wapima binafsi ili wasiwe na bei ambazo zinaumiza wananchi. Serikali inaweka viwango kutegemeana na hali halisi ya bei inayotakiwa kutozwa mwananchi wakati wa upimaji. Sekta binafsi nayo ipo na inafanya kazi hiyo kwa kushirikiana na Serikali na ndiyo maana juzi tu walikuwa na mkutano wao ambao uliwakutanisha wapima wote ambapo hili pia lilijitokeza kama kero kwa wananchi wengi ambao wanalalamika kwamba gharama zao ziko juu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kinachofanyika ndani ya Serikali, kwanza ni kuzungumza nao na pengine kuweza kuelekeza bei ambazo zitaweza kutumika ili kutompunja au kumuumiza zaidi mwananchi. Kwa sababu ukishaachia soko huria wale wanakwambia wana gharama nyingi na kubwa kama ambavyo tumesema vifaa vyao jinsi vilivyo, lakini kama Serikali hatuwezi kuwaachia waendelee kulitawala soko na wakati huohuo tunahitaji ardhi iwe imepimwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama Wizara tunajadiliana nao na nadhani Waziri aliongea nao na akaelekeza vizuri nini cha kufanya ili waweze kuja na taratibu ambazo hazitamuumiza mwananchi wa kawaida. Kwa sababu gharama za upimaji zinafahamika na wao wasiwe na visingizio vya kutaka kutoza fedha nyingi bila sababu ya msingi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kama tulivyokuja kwenye bei ya viwanja, vivyohivyo na gharama za upimaji lazima nazo zitakuwa na bei elekezi pamoja na kwamba ni soko huria, lakini ni bei ambazo zinalinda mlaji ili kuondokana na tatizo hili. Lengo letu ni kuhakikisha ardhi yote imepimwa. Gharama ni kubwa lakini na Wizara haiwezi kupima ardhi yote peke yake bila kushirikiana na taasisi binafsi, inaweza ikawa ngumu zaidi. Kwa hiyo, naomba mtupe muda, tunazungumza nao tuweze kufikia muafaka namna gani ya kuweza kutoza gharama za upimaji kwa maeneo yote hapa nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, ameongelea habari ya wale ambao wamevunjiwa na walifuata taratibu. Serikali ilishaelekeza, kama kuna watu walikuwa na hati na walizipata kihalali, watu wale walitakiwa kutambuliwa. Kwa sababu zoezi hili ni kama lile lililofanyika Dar es Salaam ambapo Wizara ilielekeza wale waliokuwa na hati za halali za umiliki walitakiwa kuleta hati zao Wizarani wakatambuliwa. Kwa hiyo, hili linaweza likafanyika hivyohivyo na Morogoro.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pale Morogoro tuna ofisi yetu, wapeleke hati zao tuweze kuzipitia, kama zilikuwa ni halali basi tutaona nini cha kufanya, kama ni viwanja vingine au kufuata utaratibu mwingine. Kwa sababu wakati mwingine kuna watumishi ambao hawakuwa waaminifu, anaweza akawa anasema ana hati kumbe hati yenyewe siyo halali. Kwa hiyo, tutazipitia zile hati zote, aliyekuwa na hati halali amevunjiwa kimakosa, basi taratibu za kisheria zitazingatiwa na atapata haki yake.