Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Pauline Philipo Gekul

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Babati Mjini

Primary Question

MHE. PAULINE P. GEKUL aliuliza:- Je, ni kwa nini Serikali imekuwa hairudishi katika Halmashauri zetu 30% ya mauzo ya viwanja?

Supplementary Question 1

MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi niulize maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, kama kuna maamuzi mabaya yalishawahi kufanyika ni maamuzi tuliyoyafanya katika Bunge la bajeti hii iliyopita ya 2016/2017 kwa kuondoa au kufuta vyanzo vikubwa ambavyo vinazipatia Halmashauri mapato na kuvipeleka Serikali Kuu.
Mfano kodi ya majengo ambayo mpaka sasa TRA wameshindwa kukusanya, kodi ya ardhi inapelekwa kwenye Mfuko Mkuu wa Hazina lakini mpaka sasa hazijarudishwa, Halmashauri hazina fedha. Swali, Mheshimiwa Waziri ni kwa nini msifikirie upya uamuzi huu na kurudisha vyanzo hivi kwenye Halmashauri zetu kwa sababu hata Serikali Kuu mkikusanya hamzirudishi kwa wakati? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, Mheshimiwa Naibu Waziri amekiri juzi hapa kwenye Bunge hili kwamba Halmashauri zetu nyingi hazina set za upimaji viwanja, hakuna vile vifaa na katika majibu yake amesema kwamba ataangalia utaratibu wa kurudisha fedha hizi. Ni kwa nini sasa hizi pesa zisitumike kununua vifaa vya upimaji katika Halmashauri zetu ilhali amekiri mwenyewe kwamba hakuna vifaa hivyo?

Name

Dr. Angeline Sylvester Lubala Mabula

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Ilemela

Answer

NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la kwanza ambalo ameanza na maelezo anasema kwamba kama kuna maamuzi mabaya yamefanyika ni Bunge la bajeti lililopita. Mimi niseme tu maamuzi ya Bunge yaliyopitishwa na yeye ni mhusika kwa sababu ni mmoja wa Wabunge waliopitisha.
Maana yake ni kwamba Bunge linapoamua Wizara inatekeleza yale ambayo yanakuwa yameamuliwa kwa sababu yanakuwa na manufaa kwa Taifa. Kwa hiyo, sisi tunatekeleza kile ambacho Bunge hili liliona kinafaa kuzingatiwa kwa ajili ya mustakabali wa maendeleo ya Taifa hili kwa ujumla wake. Kwa hiyo, hayo ni maamuzi ya Bunge na tunayafanyia kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili amezungumzia suala la gharama za vifaa na nilisema hapa wazi ni kweli na tulitaja mpaka na gharama zake kwamba ni kubwa. Katika utaratibu mzima wa kuziwezesha Halmashauri zetu, Wizara kama Wizara kwa sasa na juzi nilisema hapa kwamba tayari tumeshatangaza zabuni ya kununua vifaa vitakavyokwenda katika ofisi zetu za kanda na zitafanya kazi katika Halmashauri zile. Wizara kuwa na vifaa katika kanda haizuii Halmashauri zenyewe kuweka mpango wake wa kununua vifaa kwa ajili ya kufanya kazi. Wizara inasaidia kuhakikisha kwamba kazi zile zinafanyika katika maeneo husika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kwa sababu suala hili linaonekana ni tatizo na ni changamoto kubwa, ndiyo maana nimesema kwa utaratibu wa sasa Wizara yangu pamoja na Ofisi ya Rais, TAMISEMI tunaangalia namna bora ya kuhakikisha kwamba idara hii haishindwi kufanya kazi zake katika Halmashauri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, wakati Wizara inaangalia namna bora ya kufanya, basi pia ni jukumu la Halmashauri zetu kuona ni namna gani tutaliwezesha zoezi hilo ili tuweze kufanya kazi za upimaji na kazi za ardhi kwa ujumla ziweze kufanyika vizuri.