Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Margaret Simwanza Sitta

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Urambo

Primary Question

MHE. MARGARET S. SITTA aliuliza:- Ujenzi wa Barabara ya Tabora – Ndono – Urambo ulikuwa unaendelea vizuri kabla ya shughuli hizo za ujenzi kusimamishwa ghafla kilomita tano nje ya mji wa Urambo kwa karibu mwaka sasa. Je, ni lini ahadi ya Serikali ya kujenga kilomita nane kupitia katikati ya mji wa Urambo itatekelezwa?

Supplementary Question 1

MHE. MARGARET S. SITTA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ili na mimi niulize maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri napenda kumwuliza maswali yafuatayo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Mkoa wa Tabora kwa muda mrefu umekuwa ukililia barabara hizi za lami; na tunaishukuru Serikali ya Mapinduzi imewezesha kwa kiwango ilichoweza. Sasa alipojibu Mheshimiwa Waziri kwamba tunategemea barabara ikamilike mwezi Juni. Je, haoni kuna umuhimu wa kutaja hapa ni lini fedha zinakwenda? Kwa sababu wakandarasi wapo, hawafanyi kazi kwa sababu hakuna fedha.
Naomba Serikali itamke hapa, ni lini fedha zitapelekwa ili kuiwezesha kampuni ya CHICO ifanye kazi ili kweli barabara ikamilike mwezi Juni? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pili, ni kweli kama alivyosema Mheshimiwa Waziri kwamba barabara ya Kilometa 6.3, kutoka nje ya mji kidogo, panaitwa Ndorobo, kufika mjini na kupitiliza hadi Seed Farm haikuwemo kwenye usanifu wa barabara kubwa, ile ya msingi inayokwenda mpaka Kigoma. Lakini alipokuja Rais wa Awamu ya Nne, Mheshimiwa Jakaya Kikwete, aliahidi mbele ya Mkutano wa hadhara kwamba barabara ile ya katikati ya Urambo itajengwa na Serikali. Pia alipokuja Mheshimiwa Magufuli ambaye sasa hivi ni Rais wa Jamhuri ya Muungano…
MHE. MARGARET S. SITTA: Mheshimiwa Naibu Spika, ndilo hili nauliza. Kwa kuwa ilikuwa ni ahadi ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wa Awamu ya Nne; na kwa kuwa pia Mheshimiwa Rais ambaye wakati huo alikuwa Waziri wa Ujenzi aliahidi kwamba barabara hiyo itajengwa kwa lami. Je, Serikali haioni kwamba kwa kuwa usanifu tayari na fedha zimeshatengwa, kwa nini wasiwape hao kampuni ya CHICO, inapomalizia kipande kile ambacho hakijamaliziwa, wakati huo huo wamalize na barabara inayopita katikati ya Urambo ili zote kwa pamoja zikutane eneo la Seed Farm? (Makofi)

Name

Eng. Edwin Amandus Ngonyani

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Namtumbo

Answer

NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu lini fedha zitakwenda, nadhani atakiri kwamba ndani ya Bunge hili Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano alishatamka kwamba fedha zimeanza kuja, tumeshapokea zaidi ya shilingi bilioni 280. Kwa kweli awamu hii naomba kumwakikishia kwamba hiyo kazi itafanyika na ahadi hiyo itatekelezwa kwa sababu fedha zimeanza kuja.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa swali la pili nadhani anaongelea masuala ya procurement. Nina uhakika, kwa sababu CHICO wako pale, vifaa wanavyo, inawezekana kwamba bei watakazozitoa, wao watakuwa na bei rahisi zaidi, kwa hiyo, uwezekano wa wao kushinda ni mkubwa zaidi kwa sababu tayari wana vifaa pale. Naomba tu tufuate taratibu za procurement, muda utakapofika, nina uhakika watu hawa watafikiriwa.