Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Allan Joseph Kiula

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Iramba Mashariki

Primary Question

MHE. ALLAN J. KIULA aliuliza:- (a) Je, ni lini Serikali itatoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa Mahakama ya Wilaya na kuteua Mahakimu wa Wilaya? (b) Je, kwa nini Serikali isiridhie Mahakama ya Mwanzo iliyopo ifanywe kuwa Mahakama ya Wilaya?

Supplementary Question 1

MHE. ALLAN J. KIULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nimshukuru Mheshimiwa Waziri kwa kutuahidi kwamba mwaka wa fedha 2017/2018 tutaanza kujengewa mahakama, lakini cha pili nimhakikishie kwamba kiwanja atapata, kiwanja kipo. Sasa naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu wananchi wa Mkalama wanapata adha kubwa na wanakwenda kilometa zaidi ya 100 kupata huduma hiyo Kiomboi, katika kipindi hiki cha mpito haoni umuhimu wa kuanzisha mahakama ya Wilaya ya mpito kwa maana kwamba hiyo mahakama ya Wilaya iliyopo inaweza kuhamishiwa katika mahakama iliyopo Gumanga au Iyambi, takribani kilometa 15, ambazo kilometa 15 ni ndani ya kilometa zinazokubalika ili wananchi waanze kupata huduma hiyo wakati wakisubiri hilo jengo jipya na la kisasa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, je, Waziri atakuwa tayari kutembelea Wilaya ya Mkalama katika kipindi hiki cha Bunge, maana tukitawanyika hapa tunakuwa hatuonani tena, ili aweze kujionea uhitaji wa Mahakama ya Wilaya na aone viwanja vilivyopo kwa wingi na huduma nyingine za Mahakama za Mwanzo?

Name

Dr. Harrison George Mwakyembe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kyela

Answer

WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, nianze na suala la kutembelea MkaLama, Mheshimiwa Kiula nakuhakikishia mkipata kiwanja, kama unavyosema mmepata, lakini chenye nyaraka zote, hata kesho mimi nakuja na nitajitahidi nije na viongozi wa Mahakama kuwathibitishia wananchi kuwa tumedhamiria kuwamalizia tatizo hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, naelewa pressure aliyonayo Mheshimiwa Kiula kuwapunguzia adha wananchi wa Wilaya mpya ya Mkalama. Namuomba Mheshimiwa avute subira, hiyo mikakati ya mpito haitakuwa na tija sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili yasijitokeze maswali mengine ya nyongeza, nimeona Wabunge wengi wamesimama, naomba niwatulize Waheshimiwa Wabunge wote kuwa katika mwaka huu wa fedha Mfuko wa Mahakama umetengewa jumla ya shilingi bilioni 46.76 kwa ajili ya miradi mbalimbali ya maendeleo, lakini katika fedha hiyo ujenzi wa mahakama ni shilingi bilioni 36; kwa hiyo ukiunganisha na pesa tuliyokuwa nayo mwaka 2015/2016 ya shilingi bilioni 12.3 tuna shilingi bilioni 48.3 kwa ujenzi wa mahakama. Fedha hizi zitatumika kujenga mahakama 40 nchini kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, miradi ya ujenzi kwa mwaka 2015/2016 na 2016/2017 kwa fedha hii niliyoitamka itakuwa kama ifuatavyo ili Waheshimiwa Wabunge msisumbuke kusimama tena. Tunajenga Mahakama Kuu mpya nne katika Mikoa ya Mara, Kigoma, Dar es Salaam na Arusha.
Tunajenga Mahakama za Mikoa sita za Hakimu Mkazi, katika Mikoa ya Simiyu, Geita, Katavi, Njombe, Songwe na Lindi. Makakama za Wilaya tunajenga 14 ambazo ni Bunda, Kilindi, Bukombe, Chato, Makete, Ruangwa, Kondoa, Kasulu, Nkasi, Sikonge, Chamwino, Namtumbo, Nyasa na Hanang. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mahakama za Mwanzo vilevile tunajenga mpya 16, tena katika kipindi kifupi. Tunajenga Mwanga, Makuyuni (Arusha), Ludewa Mjini, Longido, Lukuledi (Mtwara), Gairo (Morogoro), Nangaka (Nanyumbu), Makongorosi sasa hivi iko Mbeya, Ulyankulu (Tabora), Sangabuye (Nyamagana), Telati (Simanjiro), Mtowisa (Sumbawanga), Uyole (Mbeya), Kibaya (Kiteto), Mgandu (Wanging‟ombe) na Chanika (Dar es Salaam). (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie tu kwamba katika ujenzi wa mahakama hizi, Mahakama kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Ardhi na Baraza la Taifa la Ujenzi watatumia ujenzi wa gharama nafuu, lakini majengo yatakuwa bora.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumetumia teknolojia hii mpya kujenga Mahakama ya Wilaya ya Kibaha ambayo wengi mmeiona tena kwa gharama ndogo ya asilimia 40 chini ya bei ya kawaida ya hizi conventional methods tena kwa kipindi kifupi cha miezi mitatu tu na kwa kiwango kikubwa cha ubora wa jengo.