Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Willy Qulwi Qambalo

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Karatu

Primary Question

MHE. WILLY Q. QAMBALO aliuliza:- Katika kupunguza tatizo sugu la maji Wilaya ya Karatu baadhi ya vijiji kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wamechimba visima virefu 12 katika maeneo ya Basodawish, Endabash, Rhotia Kainani, Endamarariek, Getamock, Karatu Mjini, Gongali na kadhalika, visima hivyo vinaendeshwa kwa kutumia mashine za dizeli jambo ambalo linasababisha gharama kubwa za uendeshaji. Je, Serikali itawasidia lini wananchi hao kwa kuwaunganisha na nishati ya umeme katika visima hivyo ili kupunguza gharama za uendeshaji?

Supplementary Question 1

MHE. WILLY Q. QAMBALO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niulize maswali madogo ya nyongeza pamoja na majibu yenye matumaini ya Naibu Waziri.
Mheshimiwa Naibu Spika, kisima hiki cha Karatu Mjini kimeombewa umeme sasa ni mwaka mmoja na nusu lakini bado haujaunganishwa na nikiangalia fedha zinazoongelewa kukamilisha kazi ile ni shilingi milioni 33, naona hizi ni fedha kidogo sana kwa Serikali hii ya Awamu ya Tano Serikali ya Hapa Kazi Tu.
Mheshimiwa Waziri kwa nini Serikali isitafute fedha hizi shilingi milioni 33 ili kisima hiki kiweze kukamilika ili wananachi wapate huduma hii muhimu?
Swali la pili, Awamu ya Tatu ya REA inasubiriwa kwa hamu sana katika nchi yetu kwa sababu ni awamu ya kuiwasha karibu Tanzania yote. Hivi sasa tuko mwezi wa tatu ndani ya awamu hiyo; je, ni lini utekekezaji au ujenzi wa miundombinu ya umeme katika maeneo yetu utaanza ili wananchi wetu waweze kujiandaa? (Makofi)

Name

Dr. Medard Matogolo Kalemani

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Chato

Answer

NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli Mji wa Karatu Mjini kweli ulikuwa upelekewe umeme tangu awamu iliyopita lakini Serikali kulingana na kutoa vipaumbele imetoa shilingi bilioni 33.81 kama alivyosema Mheshimiwa Mbunge, nimhakikishie tu kwamba hizo fedha zitatosha na isipotosha Serikali bado itatafakari namna ya kuongeza pesa kwa ajili ya kukamilisha mradi huo. Kwa sasa nina uhakika hizo fedha zinatosha na mji wa Karatu Mjini utapata umeme wa uhakika na visima vya maji vyote vitapata umeme kwa kutumia mitambo ya maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimpongeze sana Mheshimiwa Qambalo tumekuwa tukishirikiana sana hata kwenye awamu ya Bunge lililopita. Vijiji alivyotaja ambavyo ni vijiji 21 ambavyo havijapata umeme, nimhakikishie Mheshimiwa Qambalo tumekupelekea umeme vijiji 27 bado vijiji 21 na kati ya vijiji 21 ambavyo bado vimebaki navitambua sana na nimeshafika eneo lile. Kijiji chako cha Endamarariek kitapata umeme, Kambi Faru vitapata umeme hata kule Mbuga Nyukundu itapata umeme kule Rhotia Mbulu kwenye kijiji chako Mheshimiwa Mbunge kitapata umeme pamoja na Mikocheni na Changarawe vyote vitapata umeme.
Kwa hiyo namhakikishia Mheshimiwa Mbunge vijiji vyake vyote ambavyo nimevitaja na ambavyo sijavitaja pia vitapata umeme na kwamba REA Awamu ya Tatu inaanza kuingia sasa site kuanzia mwezi wa Novemba na mwezi wa Disemba. Hivi sasa wakandarasi wameshapatikana wasimamizi wa kazi wameshapatikana, kazi iliyobaki sasa ni kuanza kutekeleza kwenye kipindi cha mwezi Novemba hadi Disemba. Nimhakikishie vijiji vyake vyote 27 hata kijiji chako Mheshimiwa kile Kijiji cha Kilimamoja kitapata umeme na Kilimatembo bado kitapata umeme. (Makofi)
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Willy Qambalo pamoja na majibu yote hayo sijayaona makofi au umepiga ni mimi nilikuwa sioni. Tunaendelea Waheshimiwa Mheshimiwa Musukuma Joseph Kasheku Mbunge wa Geita, swali lake litaulizwa kwa niaba na Mheshimiwa Lolesia Bukwimba.