Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Stanslaus Shing'oma Mabula

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nyamagana

Primary Question

MHE. STANSLAUS S. MABULA aliuliza:- Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli wakati wa Kampeni za Uchaguzi Mkuu aliahidi ujenzi wa barabara ya lami kutoka Igoma – Kishiri – Kanindo kupitia Kata za Lwanhima na Bulongwa. Je, ni lini ujenzi wa barabara hiyo utaanza kutekelezwa?

Supplementary Question 1

MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Naomba niulize maswali mawili ya nyongeza, lakini pamoja na maswali mawili ya nyongeza, nikiri kwamba sijaridhishwa kabisa na majibu ya Mheshimiwa Waziri na wala sikubaliani nayo kwa sababu za msingi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sote tunafahamu, Nyamagana ndiyo kitovu cha Mkoa wa Mwanza na ni mji unaokua kwa kasi sana, barabara hii haijasemwa leo, imesemwa sana, sasa tukisema mwaka 2017/2018 ndiyo tuanze upembuzi yakinifu tunakuwa hatuwatendei haki wananchi wa Jimbo la Nyamagana.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nimwombe Naibu Waziri na akumbuke kwamba iko sasa hivi mikakati ya kuboresha miji ukiwemo Mji wa Mwanza, barabara hii itakuwa muhimu sana kwa mkakati wa Serikali wa ukusanyaji mapato, ni lini watakuwa tayari kutumia fedha za dharura kuhakikisha hii shughuli ya kufanya upembuzi yakinifu inafanyika kwa mwaka huu na mwaka ujao barabara hii ianze kujengwa? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, kwa sababu zilezile kwamba Mji wa Mwanza ni mji unaokua kwa kasi na mara nyingi tumekuwa tukitumia fedha nyingi wakati wa dharura, tunaposubiri mvua nyingi zinanyesha na kuharibu barabara. Je, ni lini sasa fedha hizi za dharura zitatumika kuimarisha barabara ikiwemo barabara ya kutoka Mkuyuni kwenda Nyangurugulu kutokea Mahina, Buzuruga, lakini ya kutoka Mkolani kwenda Saint Augustine University kupitia Luchelele na Nyegezi Fisheries?

Name

Dr. Selemani Said Jafo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kisarawe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nataka nimjulishe Mheshimiwa afanye rejea katika maeneo ambayo tunafanya mikakati kama Serikali kuboresha barabara zetu likiwepo na Jiji la Mwanza. Kupitia mpango wetu wa strategic cities Mwanza ni eneo ambalo tunajenga miundombinu hiyo ikiwa sambamba na Shinyanga, Arusha, Iringa, Mbeya na maeneo mengine.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, najua kwamba barabara hii ni kweli haijakamilika, lakini nimesema kila jambo lina mpango na Mheshimiwa Mabula, anafahamu Mheshimiwa Rais alivyokwenda pale alisema siyo hizo barabara za eneo la Mwanza isipokuwa hata kujenga daraja katika Ziwa Victoria, nalo linafanyika katika Jiji la Mwanza, mpango mkakati huo unapoenda maana yake kutakuwa na uboreshaji wa hizo barabara.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nimwambie Mheshimiwa Mbunge kwamba najua, amesema ni muda mrefu, lakini anakumbuka huko nyuma alikotoka wapi na hivi sasa yeye yuko wapi. Naamini uwepo wake sasa utasukuma mambo haya yaende vizuri zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba nimhakikishie kwamba Serikali imejipanga ile ring road itatengenezwa. Kwa mujibu wa Serikali ilivyojipanga ring road tutatengeneza na isitoshe na yeye anafahamu kule site kuna watu sasa hivi wanaboresha barabara za Jiji la Mwanza, naomba niwahakikishie watu wa Mwanza, Mheshimiwa Rais alivyotoa kwamba kujenga barabara mpaka kupeleka airport baada ya kuvunja sherehe maana yake hiyo ni commitment ya Serikali ili baadaye Watanzania wote wanufaike, amesema kwamba tuelekeze eneo hili kwa sababu ni eneo la mkakati, ni azma ya Serikali kuboresha miundombinu hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, naomba nimwambie kwamba katika kipindi cha sasa Serikali ilivyojipanga tutaboresha barabara za aina mbalimbali na katika hilo la kwamba kwa kutumia fedha za dharura tutafanya nini. Juzijuzi nilikuwa katika Jimbo la Mheshimiwa Mabula kule Ilemela, kuna baadhi ya barabara tumefanyia ukarabati.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia afuate rejea yangu ya kipindi kilichopita, kwamba tutafanya kila liwezekanalo barabara zilizoharibika kwa kadri rasilimali fedha itakavyopatikana tutaendelea kuiboresha. Kwa hiyo, nimwambie mtani wangu, asihofu, awaambie watu wa Mwanza kwamba wamempata jembe lakini Serikali itamsaidia kuboresha Jiji la Mwanza. (Makofi)

Name

Rwegasira Mukasa Oscar

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Biharamulo Magharibi

Primary Question

MHE. STANSLAUS S. MABULA aliuliza:- Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli wakati wa Kampeni za Uchaguzi Mkuu aliahidi ujenzi wa barabara ya lami kutoka Igoma – Kishiri – Kanindo kupitia Kata za Lwanhima na Bulongwa. Je, ni lini ujenzi wa barabara hiyo utaanza kutekelezwa?

Supplementary Question 2

MHE. OSCAR R. MUKASA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Ipo ahadi pia ya Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli katika Mji wa Biharamulo ya kuweka kilometa nne za lami wakati akituomba kura. Kwa kuwa sisi habari ya kilometa nne haina mambo makubwa yanayojumuisha mpaka habari ya vivuko kwenye Ziwa Victoria, Naibu Waziri anatuambia nini kuhusu utekelezaji wa haraka na wa siku za karibuni wa ujenzi huo wa ahadi ya Rais?

Name

Dr. Selemani Said Jafo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kisarawe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naomba niwape pole watu wa Kagera kwa msiba mkubwa uliotupata na najua sio hilo tu, maana yake maeneo mbalimbali kule yatakuwa yameathirika hasa miundombinu ya barabara. Naomba nimhakikishie, kwa sababu ahadi hii ni ahadi ya Mheshimiwa Rais na ndiyo maana Mheshimiwa Rais amejielekeza katika ukusanyaji wa mapato ili mradi kuhakikisha ahadi zake zimetekelezeka.
Mheshimiwa Naibu Spika, imani yangu, kama mwenyewe anavyosema na kama Serikali yake inavyoonesha jinsi gani ukusanyaji wa mapato ulivyo, tutahakikisha barabara hii inatengenezwa, lakini sitaki kukwambia commitment ya tarehe, kwamba lini tutafanya hivyo, lakini katika kipindi hiki naamini itatengenezeka kwa sababu nguvu kubwa inaelekezwa kuhakikisha ahadi za Rais na utekelezaji wa ilani unatekelezeka katika kipindi hiki.

Name

Kiswaga Boniventura Destery

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Magu

Primary Question

MHE. STANSLAUS S. MABULA aliuliza:- Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli wakati wa Kampeni za Uchaguzi Mkuu aliahidi ujenzi wa barabara ya lami kutoka Igoma – Kishiri – Kanindo kupitia Kata za Lwanhima na Bulongwa. Je, ni lini ujenzi wa barabara hiyo utaanza kutekelezwa?

Supplementary Question 3

MHE. KISWAGA B. DESTERY: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Kwa kuwa matatizo ya Magu yanafanana sana na matatizo ya Nyamagana, Barabara ya Ngudu – Magu – Ngumarwa, usanifu umeshakwisha kukamilika, sambamba na Barabara ya Airport – Igombe – Kayenze – Kongolo – Nyanguge ili kupunguza msongamano wa kuingia Jiji la Mwanza na kwa sababu ni ahadi ya Mheshimiwa Rais, je, barabara hizi zitaanza kujengwa lini kwa kiwango cha lami? (Makofi)

Name

George Boniface Simbachawene

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kibakwe

Answer

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri sana yanayotolewa na Naibu wangu, Mheshimiwa Jafo, napenda kujibu maswali ya nyongeza yaliyoulizwa yanayofanana sana na Waheshimiwa Wabunge juu ya ahadi za Mheshimiwa Rais ya barabara zilizoko chini ya Ofisi ya Rais TAMISEMI.
Mheshimiwa Naibu Spika, tumezihakiki, tunazifahamu lakini pamoja na mipango ya halmashauri, Wizara yangu itakuja na mpango mkakati wa namna ya kuzitekeleza barabara hizo zote kabla ya mwaka 2020. Serikali hii ni Serikali ya vitendo, tuliahidi, ni lazima tutatekeleza na ahadi za Rais ni kipaumbele chetu.