Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Susan Anselm Jerome Lyimo

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. SUSAN A. J. LYIMO aliuliza:- Ugonjwa wa kipindupindu umeendelea kukatisha maisha ya watu wengi, japokuwa chanzo chake ni uchafu ambao ungeweza kuzuilika:- Je, Serikali ina mikakati gani ya kuhakikisha ugonjwa huu unatokomezwa nchini?

Supplementary Question 1

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu, najua kwamba vyanzo vya kipindupindu hasa ni uchafu na hasa katika maeneo ya mikusanyiko kama vile kwenye masoko. Kwenye haya masoko huwa watu wanalipa kodi, lakini Serikali inashindwa kufanya usafi au kuzoa takataka. Je, Serikali sasa haioni kwamba yenyewe ndiyo chanzo cha kipindupindu?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa sasa hivi kuna tahadhari kubwa sana ya ugonjwa wa homa ya zika ambayo homa hii sasa hivi iko kule Marekani ya Kusini, lakini Tanzania siyo kisiwa na wote tunajua kwamba zika ilianzia Uganda kwenye Milima ya Zika miaka hiyo ya 1920 au 1930 huko. Kwa hiyo, bado jana nimemsikia mtendaji mkuu wa World Health Organization akisema kwamba, kuwe na tahadhari.
Je, Tanzania kama nchi imejiandaaje hasa ukizingatia kwamba, wakati ugojwa wa ebola umetokea zile specimen zilipelekwa Nairobi, je, sasa hivi ukitokea hapa Tanzania tumejiandaje kama Serikali?

Name

Dr. Hamisi Andrea Kigwangalla

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nzega Vijijini

Answer

NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza Serikali yenyewe ndiyo chanzo cha kipindupindu si kweli na naomba niseme tu jukumu la usafi, ni jukumu la kila mtu, kuanzia usafi wa mwili wake, usafi wa nyumba yake, usafi wa mahali pake pa kazi,ni jukumu la kila mtu na si jukumu la Serikali. Serikali ni mratibu kwenye uteketezaji wa taka ambayo ni hatua ya mwisho ya usafi kwa ujumla. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kuhusu ugonjwa wa zika Serikali imejiandaaje? Serikali imekwishachukua hatua za awali za kufanya matayarisho ya kujikinga na ugonjwa huu. Kwanza, nitumie nafasi hii kuwatoa hofu Watanzania wote kwamba ugonjwa huu bado haujaingia kwenye nchi yetu wala kwenye nchi za jirani. Tahadhari kubwa ambayo tumechukua ni kwa Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwanza kutoa tamko la uwepo wa ugonjwa huu kwenye nchi nyingine. Hiyo ni hatua ya kwanza ya kiepidemolojia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hatua ya pili, ni kutoa taarifa za ukweli kuhusu ugonjwa yaani fact sheet, ambayo tayari Waziri wa Afya kwa mamlaka yake amekwishatoa taarifa sahihi zinazohusu ugonjwa wa homa ya zika na zimetawanywa nchi nzima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la tatu, ni kuweka mikakati ya kuripoti mtu yeyote yule ambaye atafika kwenye vituo vya kutolea huduma na ikaonekana ana dalili zinazofanana na ugonjwa wa homa ya zika kuleta taarifa hizo centre ili tuweze kuangalia kama anaweza akawa ameambukizwa na ugonjwa huu ama la.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hizi ndio taratibu za kiepidemolojia za kufanya udhibiti wa ugonjwa wa mlipuko katika hatua ya awali ambapo ugonjwa bado haujangia nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie kwa kuwatoa hofu Watanzania kwamba ugonjwa huu sio hatari katika viwango vya ugonjwa kama wa ebola, denge, ama West Nile fever kwa sababu ugonjwa huu unasababisha tu homa ndogo ndogo lakini una madhara makubwa kwa akinamama wajawazito walio kwenye first trimester, wenye mimba changa, kwamba wanaweza wakazaa watoto wenye vichwa vidogo. Nakushukuru.