Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Ester Amos Bulaya

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. ESTER A. BULAYA (K.n.y. MHE. JOHN J. MNYIKA) aliuliza:- Mabaraza ya makundi maalum ya kijamii kama wanawake, vijana, wazee, watoto na walemavu ni vyombo muhimu katika kuwaunganisha kimaendeleo:- (a) Je, ni lini Serikali itawasilisha taarifa ya tathmini ya utendaji wa Mabaraza ya Watoto na Walemavu? (b) Je, Serikali imefikia hatua gani katika kuwezesha kufanya kazi kwa Baraza la Vijana la Taifa baada ya sheria yake kupitishwa? (c) Je, ni lini Serikali itawezesha kuundwa kwa Baraza la Wanawake la Taifa ili kuwaunganisha katika nyanja mbalimbali za kimaendeleo?

Supplementary Question 1

MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Serikali kuamua kufanya tathmini kwenye Mabaraza ya Watoto ni kwamba kuna changamoto ambazo zipo na kuyafanya Mabaraza hayo yasitetee haki za msingi za watoto hasa za watoto yatima.
Je, tunatambua kwamba kuna center za watu binafsi ambazo zinahudumia watoto yatima na zinafanya kazi kwenye mazingira magumu sana nchi nzima ikiwepo na Jimboni kwangu Bunda. Serikali ina mkakati gani wa kusaidia center hizi ili kusaidia watoto yatima waweze kulelewa vizuri na kupata huduma sahihi hasa za elimu kama wanavyopata wengine?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, mmesema Rais aliweka sahihi tarehe 22 Mei, 2015 na kwamba mpaka sasa hivi hamjakamilisha taratibu za kanuni. Ni jambo gani linawakwamisha, hamuoni kwamba kuna haja ya kukamilisha hizi kanuni mapema na mwaka huu wa fedha tutenge bajeti ili Baraza ili lianze na vijana wawe na chombo chao cha kuibana Serikali na kutetea vijana wao katika nchi hii?

Name

Dr. Hamisi Andrea Kigwangalla

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nzega Vijijini

Answer

NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nitumie nafasi hii kumpongeza muuliza swali Mheshimiwa Ester Amos Bulaya na aliyeuliza swali la msingi Mheshimiwa John John Mnyika kwa kuendelea kufuatilia haki na maslahi ya vijana wa nchi yetu. Pamoja na pongezi hizo naomba kujibu maswali yake ya nyongeza kama ifuatavyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, kwamba kuna changamoto zinazowakabili watu wenye taasisi ama vituo binafsi vinavyolea watoto yatima na kwamba Serikali inawasaidiaje.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ina majukumu ya kutengeneza mfumo wa kisheria ambao utaziwezesha taasisi mbalimbali zikiwemo za Serikali na za watu binafsi kutekeleza majukumu yake ya kutoa huduma kwa wananchi kama ilivyopangwa kwa mujibu wa sheria hizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa maana hiyo mfumo huo sasa upo na tunatengeneza Mabaraza haya kwa malengo ya kutoa ushauri kwa Serikali juu ya namna bora ya kuendesha taasisi mbalimbali za binafsi ama za Serikali zinazotoa huduma kwa watoto yatima ama watoto wanaoishi katika mazingira magumu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwamba tumechelewa kuunda kanuni. Ni miezi takriban sita tu toka sheria ile imesainiwa na Mheshimiwa Rais na sidhani kama tumechelewa. Imani yangu ni kwamba, kanuni zitatengenezwa haraka na zitaanza kufanya kazi kwa sababu mwaka 2015 ulikuwa ni mwaka wa Uchaguzi Mkuu na watu wengi walikuwa busy na kwa kipindi kirefu, hivyo Mawaziri wasingeweza kufanya kazi ya kutunga kanuni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa Serikali ipo kazini, naomba atuamini, tutatunga kanuni hizo haraka na tutawashirikisha wadau wote ili mawazo yao yaweze kuwemo humo ndani na mwisho wa siku tutunge kanuni zilizo bora ambazo zitaweza kuleta ustawi wa vijana wa nchi yetu.

Name

Dr. Elly Marko Macha

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. ESTER A. BULAYA (K.n.y. MHE. JOHN J. MNYIKA) aliuliza:- Mabaraza ya makundi maalum ya kijamii kama wanawake, vijana, wazee, watoto na walemavu ni vyombo muhimu katika kuwaunganisha kimaendeleo:- (a) Je, ni lini Serikali itawasilisha taarifa ya tathmini ya utendaji wa Mabaraza ya Watoto na Walemavu? (b) Je, Serikali imefikia hatua gani katika kuwezesha kufanya kazi kwa Baraza la Vijana la Taifa baada ya sheria yake kupitishwa? (c) Je, ni lini Serikali itawezesha kuundwa kwa Baraza la Wanawake la Taifa ili kuwaunganisha katika nyanja mbalimbali za kimaendeleo?

Supplementary Question 2

MHE. DKT. ELLY M. MACHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Napenda kumuuliza Mheshimiwa Waziri swali moja dogo la nyongeza, je, Waziri anaweza kulihakikishia Bunge hili kwamba katika hii bajeti ya 2016/2017, kutatengwa bajeti kwa ajili ya kuliwezesha Baraza la Ushauri kwa Watu Wenye Ulemavu kuanza kazi na programu zake kuwafikia watu wenye ulemavu? (Makofi)

Name

Jenista Joackim Mhagama

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Peramiho

Answer

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WALEMAVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, kwanza kabisa nianze kumpongeza sana Mheshimiwa Mbunge kwa uwakilishi wake mahiri na hasa katika kundi hili la walemavu katika nchi yetu ya Tanzania na swali lake ni swali lenye msingi wa hali ya juu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni azma ya Serikali sasa kuhakikisha kwamba pamoja na utungaji wa Sheria namba 9 ya mwaka 2010 ambayo imetoa maelekezo ya namna gani kundi hili muhimu katika nchi yetu ya Tanzania litaweza kuzingatiwa katika nyanja zote za maendeleo katika nchi yetu ya Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, Ofisi ya Waziri Mkuu inathamini na kuona umuhimu wa kundi hili maalum na hakika katika bajeti ya mwaka huu unaokuja wa fedha itazingatia kuona Baraza la Watu Wenye Ulemavu linatengewa fedha na linafanya kazi zake kwa mujibu wa sheria iliyotungwa, Sheria namba 9 ya mwaka 2010.