Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Khatib Said Haji

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Konde

Primary Question

MHE. KHATIB SAID HAJI aliuliza:- Matukio ya wananchi kujichukulia sheria mkononi yamezidi kuongezeka siku hadi siku na kusababisha madhara na vifo kwa watu wasio na hatia:- Je, Serikali inafanya juhudi gani ili kupunguza au kuondoa kabisa ukatili huu?

Supplementary Question 1

MHE. KHATIB SAID HAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Tarehe 25 Septemba, 2015, Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kilitoa tathmini iliyoonesha kwamba vyombo vya dola vina asilimia 60 ya uvunjaji wa haki za binadamu katika nchi hii na asilimia 40 inafanywa na raia wa kawaida. Hivi Watanzania wamtegemee nani ikiwa vyombo vya dola vilivyopewa jukumu la kulinda usalama wa mali na raia ndiyo vinaongoza katika ukiukaji wa haki za binadamu katika nchi hii? Wamtegemee nani?
Swali la pili, dogo tu. Mheshimiwa Waziri, kule Zanzibar, takribani ni wiki ya pili sasa, kumekuwa na matukio ya maharamia wanaojifunika soksi kwenye nyuso wakisimamiwa na vikosi vya SMZ kufanya uharamia mbalimbali katika Mji wa Zanzibar. Mheshimiwa Waziri, jana alisema hapa hana taarifa, tunamwomba atoe tamko, wananchi wawashughulikie kwa mujibu itakavyofaa kwa sababu ni maharamia ambao huna taarifa kama wanafanya uharamia katika Visiwa vya Zanzibar. Atoe awaambie wananchi wawapige mawe na wachome gari zao moto ili tupate suluhu ya uharamia unaofanywa Zanzibar. (Makofi)

Name

George Mcheche Masaju

Sex

Male

Party

Ex-Officio

Constituent

None

Answer

MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kulishauri Bunge hili Tukufu kwamba, sisi Wabunge hapa tumeapa kuitii Katiba na sheria za nchi. Ibara ya 26 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano inasema kabisa kwamba kila mtu lazima aitii Katiba na kufuata sheria za nchi. Sasa hoja anayozungumza Mheshimiwa Mbunge kuhamasisha sheria za nchi zivunjwe siyo sahihi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Waziri hawezi akatamka kwamba watu wavunje sheria na sisi Wabunge ndiyo tunaozitunga hizi sheria tunapaswa tuwe wa kwanza kusimamia utekelezaji wake. Kwa hiyo, nashauri kwamba, Mheshimiwa Mbunge hilo tamko analotaka kutoka kwa Mheshimiwa Waziri haliwezekani kwa sababu Waziri hawezi kusimama mbele ya Bunge akahamasisha watu wavunje sheria.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS (UTUMISHI NA UTAWALA BORA): Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Kuhusiana na hoja yake kwamba, vyombo vya dola vinakiuka haki za binadamu, niseme tu kwamba, kwa kweli vyombo vya dola vimekuwa vikifanya kazi nzuri katika kuhakikisha kunakuwa na amani na utulivu na vinahakikisha kwamba vinafanya kazi yao kwa ufanisi mkubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, endapo anayo malalamiko au uthibitisho, akayawasilishe katika Tume ya Haki za Binadamu na upo mchakato wa namna ya kuwasilisha malalamiko hayo. (Makofi)

Name

Joseph Roman Selasini

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Rombo

Primary Question

MHE. KHATIB SAID HAJI aliuliza:- Matukio ya wananchi kujichukulia sheria mkononi yamezidi kuongezeka siku hadi siku na kusababisha madhara na vifo kwa watu wasio na hatia:- Je, Serikali inafanya juhudi gani ili kupunguza au kuondoa kabisa ukatili huu?

Supplementary Question 2

MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, matukio ya wananchi kujichukulia sheria mikononi yanasababishwa na mambo mawili. Jambo la kwanza, ni baadhi ya Askari Polisi kupewa taarifa za matukio na kutokwenda kwenye maeneo ya matukio kwa wakati unaotakiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sababu ya pili ni wahalifu kupelekwa vituoni na baada ya muda mfupi kuonekana wakirandarada mitaani bila kuchukuliwa hatua stahiki na Jeshi la Polisi. Sasa je, Serikali inawaambia nini Watanzania hasa kutokana na uzembe huu ambao unafanywa na baadhi ya Askari Polisi unaosababisha wananchi kukata tamaa na kujichukulia hatua mikononi?

Name

Eng. Hamad Yussuf Masauni

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kikwajuni

Answer

NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nianze kwanza tu kueleza jambo tu kwa kifupi sana kabla sijajibu hili swali. Ni kwamba Jeshi letu la Polisi ni jeshi ambalo linajitahidi kufanya kazi kwa mujibu wa sheria na weledi wa hali ya juu.
Hata hivyo, Jeshi letu la Polisi linakumbana na changamoto mbalimbali, kwanza idadi ya polisi ambao tunao hawatoshelezi, kwani sasa hivi Polisi mmoja anahudumia kati ya watu 300 mpaka 350, idadi ambayo ni kubwa ukilinganisha na kiwango cha Kimataifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini hata hivyo tumeona malalamiko mengi ya Waheshimiwa Wabunge kuhusiana na matatizo mbalimbali yakiwemo makazi, usafiri na kadhalika kutokana na hali ya uchumi wa nchi yetu kwa ujumla wake. Kwa hiyo, mbali ya changamoto hizi nyingi ambazo Jeshi letu la Polisi linakabiliana nazo lakini linajitahidi kadri ya uwezo wake kuweza kufanya kazi zake kwa kuzingatia maadili, weledi pamoja na sheria za nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, hiyo haiondoshi ukweli kwamba wakati mwingine inatokeza baadhi, kama ilivyo mtu mwingine wa sehemu nyingine yoyote, kwamba baadhi ya polisi wanaweza kuwa na upungufu wa hapa na pale. Kadri hali hiyo inavyojitokeza, hatua madhubuti za kisheria zimekuwa zikichukuliwa. Wapo baadhi ya polisi wamekuwa wakichukuliwa hatua za kisheria kupitia Mahakama za Jeshi la Polisi yenyewe, lakini na wale ambao wameweza kutenda makosa ya jinai vilevile sheria imekuwa ikifuata mkondo wake.