Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Rwegasira Mukasa Oscar

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Biharamulo Magharibi

Primary Question

MHE. OSCAR R. MUKASA aliuliza:- Kwa miaka ya hivi karibuni, kumekuwa na ongezeko kubwa la matukio ya ujambazi unaohusiana na uporaji wa fedha na ni muhimu sana Watanzania wakapata ufahamu kwa takwimu kuhusu ukubwa au udogo wa tatizo hilo kuliko kupata taarifa ya tukio moja moja:- (a) Je, ni zipi takwimu sahihi na mchanganuo wa matukio ya ujambazi unaohusiana na uporaji wa fedha ikiwa ni pamoja na vifo na majeruhi ya matukio hayo kuanzia mwaka 2013 hadi 2015 Kitaifa? (b) Je, ni mikoa gani miwili inayoongoza na mikoa gani miwili yenye matukio hayo machache?

Supplementary Question 1

MHE. OSCAR R. MUKASA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Pamoja na takwimu nzuri za Naibu Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu matukio ya uporaji kwa watu wanaotoka kuchukua fedha tasilimu benki, ni miongoni mwa matukio mengi yanayotokea hivi sasa na kwa kuwa kuna imani na minong‟ono miongoni mwa wananchi kwamba watumishi na wafanyakazi wa benki kwa namna fulani wanahusika na kuwezesha uhalifu huu. Serikali inatoa kauli gani kuhusu imani hiyo na minong‟ono ya Watanzania?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa baadhi ya matukio ya uporaji wa pesa, watu wanavyotoka kuchukua pesa tasilimu benki yanahusisha matumizi ya pikipiki na kwa kuwa pikipiki zinatoa ajira halali kwa vijana wa bodaboda, lakini wachache wanatumia kuichafua na kuumiza Watanzania. Serikali inasema nini kuhusu kushindwa kwake kuwadhibiti hao wachache ambao wanatumia vibaya vyombo vya usafiri ambavyo vinatoa ajira na masilahi mengine kwa Watanzania katika kudhibiti hili?
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru.

Name

Eng. Hamad Yussuf Masauni

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kikwajuni

Answer

NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na wizi wa benki ni kweli kumetokea na wimbi la kuiba benki katika kipindi cha karibuni, lakini wananchi wamechukua hatua madhubuti ikiwa ni pamoja na kufanya kazi karibu kabisa na benki hizo ili kuona kwamba kama kuna miongoni mwa wafanyakazi ambao sio waaminifu waweze kuchukuliwa hatua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile siyo tu miongoni mwa wafanyakazi ambao siyo waaminifu, lakini pia wale ambao wana kawaida ya kuchukua fedha nyingi, ni vizuri kabisa wakafanya utaratibu wa kuweza kuwasiliana na polisi ili waweze kuwapa ulinzi. Wakati mwingine taarifa hizi zinatoka miongoni mwa sehemu au makampuni ambayo yanajihusisha ya biashara mbalimbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba kutoa wito kwa makampuni yote au wafanyabiashara wote ambao wanaweza kusafirisha fedha nyingi kutoka sehemu moja kwenda sehemu nyingine, walitaarifu Jeshi la Polisi na Jeshi la Polisi litatoa ulinzi ili kudhibiti hali kama hiyo, wakati huo huo Jeshi la Polisi likiwa linafanya kazi ya ziada kuhakikisha kwamba, linawatia mikononi na kuweza kuwapeleka katika vyombo vya sheria wale wote ambao wanahusika kwa njia moja ua nyingine na limeshaanza kufanya kazi hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni kuhusiana na suala la pikipiki. Polisi haijashindwa kuwadhibiti hawa watu wachache ambao wanatumia vibaya fursa hii ya vijana ambao wana pikipiki, siyo tu bodaboda hata pikipiki za kawaida zimekuwa zikitumika katika uhalifu mbalimbali. Ndio maana sasa hivi kuna mazoezi mbalimbali yanaendelea nchini ikiwemo kuhakikisha kwamba wanazikagua pikipiki hizi ili kuweza kubaini uhalali wake, lakini pia uhalali wa wale ambao wanaendesha pikipiki hizi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nawaomba Waheshimiwa Wabunge tushirikiane kipindi hiki ambapo Polisi inaendesha zoezi la kuweza kuhakiki pikipiki hizi ili kuweza kuhakikisha kwamba, sheria zinafuatwa na waendesha pikipiki hizi iwe kwa utaratibu wa wafanya biashara kwa maana ya boda boda au utaratibu wa kutumia pikipiki kwa matumizi ya kawaida.