Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Amb. Adadi Mohamed Rajabu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Muheza

Primary Question

MHE. BALOZI ADADI M. RAJAB aliuliza:- Baadhi ya wakulima wa Tarafa ya Amani na Muheza wanalima kwa wingi viungo mbalimbali kama pilipili manga, karafuu, hiliki na mdalasini lakini hakuna viwanda kwa ajili ya kusindika mazao hayo. (a) Je, Serikali ina mpango gani wa kuwasaidia kupata kiwanda wakulima wa mazao hayo kwa ajili ya mazao yao? (b) Je, Serikali itakuwa tayari kuwatafutia wananchi hao wanunuzi wa uhakika wa mazao hayo?

Supplementary Question 1

MHE. BALOZI ADADI M. RAJAB: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu, lakini nina maswali mawili ya nyongeza. La kwanza, ni kweli kabisa kwamba viungo vina soko kubwa ndani na nje ya nchi kwa sababu mimi mwenyewe naona jinsi hawa wanunuzi wa kutoka nje wanavyohangaika wakati wa msimu pale Muheza.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la kwanza, ni lini Wizara itawapeleka wataalam hao kuhakikisha kwamba wanainua ubora wa wakulima hao waweze kujua namna ya kulima vizuri pamoja na kuhifadhi mazao hayo ambayo wanayazagaza nje nje tu?
La pili, kama ambavyo Wizara imesema kwamba imetenga fedha za kusaidia bustani pamoja na wakulima wa hivi viungo, mna uhakika gani kwamba wakulima wangu wa Amani na Muheza fedha hizo ambazo zimetengwa watazipata?

Name

William Tate Olenasha

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ngorongoro

Answer

NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu ni lini wataalam wa Wizara wataenda kushirikiana na wakulima katika Jimbo lake ili kuweza kuwa na kilimo cha tija, nimfahamishe tu Mheshimiwa Mbunge kwamba utaratibu wa kutoa taaluma na uelewa kwa wakulima ni utaratibu ambao ni endelevu kupitia Maafisa Ugani.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunajua kwamba kuna changamoto ndiyo zinawakabili, lakini katika bajeti yetu na ile ya TAMISEMI zimetengwa fedha kwa ajili ya kuhakikisha kwamba Maafisa Ugani wanafanya kazi na kuweza kuwafikia wakulima ili waweze kuzalisha kwa tija zaidi.
Vilevile labda nimuahidi Mheshimiwa Mbunge kwamba kwa sababu Pemba tuna kiwanda kizuri sana ambacho kinachakata viungo, tutashirikiana na Halmashauri ili kuona namna gani wakulima wanaweza vilevile wakaendelea kutembelea kiwanda hicho na kujifunza kinachofanyika ili pamoja na kushirikiana na Wizara ya Viwanda na Biashara, tuangalie ni namna gani tunaweza vile vile kuwa na kiwanda kinachoweza kuchakata viungo ili tufikie ufanisi kama walivyofikia wenzetu kutoka Pemba.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwamba tutafanya vipi kuhakikisha kwamba fedha zilizotengwa zinawafikia wakulima; nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali ya Awamu ya Tano inatembea katika ahadi zake. Kwa hiyo, yale yote ambayo tumepanga na kutenga kwa ajili ya wakulima wetu, tutahakikisha kwamba tunafuatilia ili ziweze kuwafikia bila kupotea.