Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Boniphace Mwita Getere

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bunda

Primary Question

MHE. BONIPHACE M. GETERE aliuliza:- Eneo la Buhemba Holding Ground Farm (KABIMITA) linalomilikiwa na vijiji vitatu vya Magunga, Milwa (Wilaya ya Butiama) na Mekomarino (Wilaya ya Bunda) kwa ajili ya kilimo na ufugaji ambalo lilitolewa na Serikali tangu miaka 1970 na 1980 kama kituo cha kukusanyia mifugo (ng‟ombe) na kuwatibu kabla ya kupelekwa kwenye mnada wa ng‟ombe Bukoba; na sasa ni miaka 33 eneo hili linatumiwa na wakazi wa vijiji hivyo kwa ajili ya makazi, kilimo na ufugaji. Je, ni lini Serikali itatoa tamko rasmi kwamba eneo hilo ni mali ya vijiji hivyo kisheria ili kuondoa dhana ya kuwa eneo hili ni mali ya Serikali?

Supplementary Question 1

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Swali la kwanza, je, ni lini Serikali yetu sikivu itafanya tathmini ya hali halisi ya maeneo haya ambayo ukienda kwenye maeneo hayo kuona hali halisi; na kwa bahati nzuri katika eneo hili kwenye Bunge lililopita niliuliza swali na Waziri wa Kilimo enzi hizo, Mheshimiwa Mwigulu na Naibu mwenyewe nashukuru sana kwa kufika kwenye maeneo yangu; hali halisi ya eneo hilo halipo, watu wameshajenga. Sasa je, ni lini Serikali itafanya tathmini ya hali halisi kujua maeneo haya ambayo wanamiliki hewa kumbe wananchi wote walishakali na kujenga shule za msingi?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kutokana na Sheria Namba 17 na Namba 10 alizozitaja Mheshimiwa Naibu Waziri zimechelewa sana kwa wananchi wa Kijiji cha Mikomalilo, kwa sababu walishajenga na kulima mazao ya kudumu. Je, ushauri wake sasa haoni umechelewa sana ili kuwashauri watu walime mazao ambayo siyo ya kudumu?

Name

William Tate Olenasha

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ngorongoro

Answer

NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu umuhimu na haja ya kufanya tathmini kuangalia hali halisi ya eneo la Holding Ground husika, Serikali inafahamu tosha kwamba ndiyo wananchi wamekuwa wakilitumia hilo eneo tokea miaka ya 1980; lakini kwa sasa hata pamoja na kwamba kuna maeneo ambayo yamevamiwa, hata yale ambayo yamebaki bado sisi tunaona kwamba ni muhimu kwa ajili ya matumizi ya Wizara na tusingependa kutumia kigezo cha kwamba kimevamiwa kuruhusu sasa; kwa sababu itamaanisha kwamba katika maeneo mengine wananchi vilevile wanaweza kuvamia.
Kwa hiyo, jitihada iliyopo sasa ni kuangalia namna gani tunaweza kunusuru maeneo yaliyobaki.
Mheshimiwa Naibu Spika na Waheshimiwa Wabunge, tukiruhusu maeneo yote ya Serikali yachukuliwe na wananchi baadaye Serikali ikihitaji maeneo tunaanza tena ugomvi na mgogoro na wananchi kwa sababu Serikali mara kwa mara itahitaji maeneo kwa ajili ya maendeleo ya kiujumla kwa ajili ya maendeleo ya nchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, jibu hili la swali la kwanza la nyongeza, vilevile linajibu swali la pili kwamba tamko hili la kusema wananchi wasijenge, halijachelewa. Hata mwaka 1980 waliporuhusiwa, makubaliano ilikuwa ni kwamba wasipande mazao ya muda mrefu na wala wasijenge.
Kwa hiyo, wananchi wamekuwa wakifahamu na ndiyo maana hata Mheshimiwa Mbunge leo analiuliza hili swali wakati anafahamu kwamba huo ndiyo utaratibu uliokuwa ukitumika tokea mwaka 1980.
Kwa hiyo, sisi kama Wizara hatujachelewa, kilichotokea ni kwamba wananchi hawajafuata makubaliano ambayo tuliwekeana tokea eneo hilo lianze kutumika na wananchi mwaka 1980.